Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mzimu wa penalti wamtesa Mmarekani

Melis Medo Dadama Jiji.jpeg Kocha wa Dodoma jijiu Melos Medo

Sat, 24 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kipigo cha mabao 2-0 ilichokipata Dodoma Jiji juzi dhidi ya Tanzania Prisons huku nahodha wake, Mbwana Kibacha akikosa penalti kimemfanya kocha, Melis Medo kuanza kuumiza kichwa.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya ilishuhudiwa mzimu wa kikosi hicho wa kukosa penalti ukiendelea kutokana na mastaa wao wengi kushindwa kuweka mpira kimiani.

Akizungumza na Mwanaspoti, Medo alisema suala hilo limekuwa likimshangaza mara kwa mara kutokana na nyota anaowateua kushindwa kufunga penalti licha ya kufanya vizuri wakiwa kwenye uwanja wa mazoezi.

“Ni jambo ambalo linatokea kwa mchezaji yeyote lakini inasikitisha kuona kwenye mazoezi wamekuwa na ujasiri mkubwa wa kupiga tofauti na kwenye mechi,” alisema Medo na kuongeza;

“Muda mwingine hutokana na presha ya mchezo husika na mchezaji kutaka kuonyesha kiu yake ya kufunga akiwa na matarajio makubwa hali ambayo inamfanya kumtoa mchezoni,” alisema.

Medo aliongeza licha ya wachezaji wake wengi kushindwa kufanya vizuri kwenye mapigo huru, ataendelea kuwaamini kila mmoja wao kutokana na kile watakachokionyesha mazoezini.

Dodoma Jiji ndiyo timu inayoongoza kwa kupata penalti nyingi msimu huu ambapo hadi sasa imepata tano. Katika hizo tano imefunga moja tu ya mshambuliaji wake, Collins Opare, aliyoipiga dhidi ya Polisi Tanzania Novemba Mosi, wakati timu hizo zilipofungana bao 1-1 kwenye Uwanja wa Ushirika, Moshi.

Nne zilizobaki ambazo zilikoswa zilikuwa ni za Paul Peter kwenye mchezo wao na Mtibwa Sugar waliokubali kichapo cha bao 1-0, Oktoba 25 kwenye Uwanja wa Liti Singida.

Collins Opare, alikosa pia walilala 1-0 dhidi ya Namungo Nov 26, sawa na Aman Kyata aliyekosa licha ya timu hiyo kushinda mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting Desemba 3 na ile ya juzi.

Chanzo: Mwanaspoti