Kipa Ayoub Lakred ameanza kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha Simba, huku akikabiliwa na mtihani mgumu wa jicho la kiufundi kutoka kwa viongozi wa timu hiyo ambao wamemwagiwa sifa kwa kufanya usajili wa eneo hilo likiwa na makipa wazuri, japo mzimu wa Aishi Manula huenda ukamtesa.
Ayoub ameshacheza mechi mbili za mashindano, moja ikiwa ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos ya Zambia iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2 ugenini kisha kuisaidia Simba kushinda mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union katika Ligi Kuu Bara na kumfanya aandike ‘clean sheet’ yake ya kwanza Msimbazi.
Kupitia mechi hizo, watalamu wa soka wamemchambua kipa huyo kutoka Morocco na kuona ana kibarua kigumu cha kuthibitisha ubora, kwanza dhidi ya kipa namba moja aliyeanza kujifua kutoka majeruhi, Aishi Manula na rekodi ya makipa waliowahi kupita ndani ya kikosi hicho cha Wekundu wa Msimbazi.
Kocha wa makipa wa Mtibwa Sugar, Patrick Mwangata aliyewahi kuidakia Simba enzi akicheza, alisema kazi ya kwanza aliyonayo Ayoub ni kuhakikisha anajua ubora wa Manula ambaye tangu ajiunge na Simba akitokea Azam, amedhihirisha kiwango hadi kuibeba Taifa Stars na mashabiki kufurahia huduma aliyoitoa hadi leo.
“Ukiangalia historia ya Simba kwenye kusajili makipa ipo vizuri tangu miaka ya nyuma, walikuwepo kina Mohamed Mwameja, Idd Pazi, Juma Kaseja, Ivo Mapunda hao ni baadhi na walifanya vizuri sana, akaja Manula ambaye pia aliwapa changamoto wengine kama Beno Kakolanya aliyeondoka, Deogratius Munishi, Said Mohamed ‘Nduda’, sio wabaya ila ushindani ulikuwa mkali,” alisema Mwangata na kuongeza;
“Hilo ni mtihani kwa Ayoub (Lakred) kujua Simba ina wachezaji gani kwenye nafasi yake, ingawa bado ni mapema kujua ni wa aina gani mechi alizocheza ni chache, kwa maana ya kuzoea Ligi Kuu na kujijengea kujiamini, hivyo kocha kuendelea kumpanga anaendelea kumjengea ujasiri.”
Hoja yake iliungwa mkono na kocha wa makipa wa Ihefu, Peter Manyika Sr, alisema Ayoub angalau anahitaji mechi zaidi kujua uwezo na changamoto zake, kutokana na kucheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza.
“Ukiachana na hilo, ajue ukubwa wa Simba, kisha ajaribu kuangalia ubora wa makipa alionao kikosini kwa sasa na wale waliopita, itamsaidia kujituma na kuongeza umakini zaidi, ili aepuke kupigiwa kelele na mashabiki wake,” alisema Manyika, huku kipa wa zamani Yanga, Benjamin Haule alisema Ayoub ana kazi kubwa kuthibitisha ubora kama kipa wa kigeni, akitaka afanye zaidi ya wanachokifanya wazawa.
“Mfano mzuri Yanga, Diarra Djigui anachokifanya kinawapa amani mashabiki na kuona hawajapigwa kwenye usajili wa eneo hilo, kajitofautisha na wazawa, anajiamini ana uwezo wa kutuliza timu, kuanzisha pasi... najua kila mchezaji ana ujuzi wake, Ayoub (Lakred) anapaswa kuonyesha,” alisema.