Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mzimu wa Dragan Popadic unavyoitesa Simba SC

Dragan Popadic (19).jpeg Mzimu wa Dragan Popadic unavyoitesa Simba SC

Sun, 19 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mabosi wa Simba kwa sasa wanakuna kichwa kwa ajili ya kumpata kocha mkuu wa kuchukua nafasi ya Mbrazili Roberto Oliveira ‘Robertinho’ a.k.a Beto waliyemfurusha hivi karibuni baada ya kipigo cha Yanga.

Simba iliamua kumtema Robertinho sambamba na wasaidizi wake wawili, Ouanane Sellami na Cornelly Hategekimana baada ya timu hiyo kufungwa mabao 5-1 na watani wao kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa Novemba 5 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Hicho kilikuwa kipigo cha kwanza kwa Simba msimu huu na cha kwanza kwa Robertinho katika Ligi Kuu tangu alipojiunga na Simba Januari mwaka huu na cha kwanza kwa miaka zaidi ya miaka 50 tangu ilipofungwa 5-0 na Yanga mnamo Juni Mosi, 1968. Kwa sasa Simba inanolewa na kaimu kocha mkuu, Mhispania Daniel Cadena aliyetua Msimbazi msimu huu kama Kocha wa Makipa chini ya Robertinho

Licha ya kumtimua kocha huyo, hali ya utulivu ndani ya Simba bado haijatulia kwani kuna shinikizo kubwa kutoka kwa mashabiki wakitaka mabosi nao wajitafakari kwa kilichotokea kwa kuamini tatizo ni wao kwa kusajili wachezaji wasio na kiwango bora na kuifanya timu kwa msimu huu ionekane ya kawaida sana.

Hata hivyo, wakati mabosi hao wa Simba wakikomaa na kuanza harakati za kusaka kocha mpya, bado wanakabiliwa na jinamizi la muda mrefu linalowatesa makocha wa kigeni wanaoajiriwa kisha kufurushwa kitatanishi wakishindwa kufikia malengo ya klabu hiyo.

SIKIA SASA

Hakuna ubishi Simba kama ilivyo kwa watani wao, Yanga au Azam FC ni miongoni mwa klabu za soka za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ambazo zimekuwa zikipata huduma toka kwa makocha wa kigeni katika miongo kadhaa.

Makocha mbalimbali wa kigeni wamekuwa wakipokezana kuingia na kutoka ndani ya klabu hizo, wengine wakiletwa kwa mbwembwe kabla ya kutimuliwa kwa fadhaha kubwa kama ilivyowahi kumkuta Tom Saintfiet, Ernie Brandts na Marcio Maximo walioinoa Yanga.

Miongoni mwa makocha hao wa kigeni ambao wamekuwa wakivuna fedha nyingi katika klabu hizo wapo wanaotoka ndani ya Bara la Afrika na wale wanaotoka barani Ulaya na Amerika.

Simba yenyewe imewahi kupata huduma ya makocha mbalimbali toka ndani ya mabara hayo tatu, yaani Afrika, Ulaya na Latin Amerika alikotoka Robertinho baada ya Zoran Maki kuondoka kitatanishi baada ya kukaa na timu hiyo kwa siku chache na kutimkia Al Ittihad ya Misri.



MZIMU UNAOTESA

Pamoja na Simba kupambana kuleta kila aina ya kocha kutoka Afrika, Ulaya na Amerika, tatizo lipo kwenye mzimu unaotesa makocha hao wa kigeni.

Dragan Popadic, kocha wa kigeni aliyewahi kuinoa timu hiyo miaka ya katikati ya 1990 aliacha alama kubwa klabu hapo kwa kutwaa mataji mengi kuliko kocha yeyote wa kigeni akimfunika hata hayati James Siang’a aliyeipeleka Simba kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza 2003.

Kama hujui ni kwamba Simba ikiwa mikononi mwa Popadic, timu hiyo iliweza kutetemesha soka la Afrika Mashariki na Kati. Timu zilizokuwa zikicheza na Simba enzi hizo zilikuwa zikiogopa kufanya madhambi katika eneo la  hatari au kutoa mipira ya kona. Kocha huyo alijiunga mwaka 1994, mwaka mmoja baada ya Simba kufika fainali ya Kombe la CAF 1993 ikiwa chini ya mzawa Abdallah Kibadeni na Mhabeshi Etienne Eshette.

Kocha huyo fundi kutoka Yugoslavia ya sasa (sasa Serbia), aliwafundisha wachezaji wa timu hiyo jinsi ya kupiga faulo na kona. Baadhi ya wachezaji waliocheza chini ya Popadic ni Mohammed Mwameja, Mwanamtwa Kihwelu, Kasongo Athuman, Mustafa Hoza, Thomas Kipese, Godwin Aswile, George Masatu na Iddi Selemani.

Wengine ni Athuman Abdallah ‘China’, Edward Chumila, Abdul Ramadhani ‘Mashine’, Juma Amir, Bakar Idd ‘Beka Joe’, Dua Said, George Lucas ‘Gazza’, Abdallah Mwinyimkuu, Said Mwamba ‘Kizota’, Mchunga Bakar ‘Mandela’, Nteze John na Madaraka Seleman ‘Mzee wa Kiminyio’.

REKODI ZILIVYO

Kwa kipindi cha kuwepo kwake Msimbazi, aliiwezesha Simba kunyakua mataji saba tofauti, mawili ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kagame) 1995 na 1996. Pia aliiwezesha kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara mbili mfululizo, 1994 na 1995. Akaipa taji la Ligi ya Muungano mwaka 1994 na 1995 baada ya awali kuwapa ubingwa wa Kombe la Nyerere 1995.

Kabla ya hapo Simba ilikuwa imewahi kunyakua ubingwa wa Kagame mara mbili mfululizo 1991 na 1992 na taji la mwisho katika michuano hiyo ni la mwaka 2002.

Hata hivyo Simba bado ndiyo mabingwa vinara wakitwaa taji mara nyingi zaidi ya klabu zote zilizowahi kutwaa tangu 1974.

Klabu hiyo imenyakua ubingwa huo mara sita ikizizidi Yanga na AFC Leopards ya Kenya ambao wametwaa mara tano kila moja.

Ingawa Simba imekuwa ikitumia mamilioni ya fedha kuleta makocha wa kigeni hasa wazungu, lakini haijawahi kunufaika na makocha hao kama ilivyokuwa kwa Popadic.

Kocha huyo aliyezaliwa Februari 4, 1946 mjini Belgrade, Yugoslavia ya zamani (Sasa Serbia) mara baada ya kuondoka Simba, alienda Uganda na kujiunga na Express ya Uganda aliyoiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo mwaka 1996 na kuwapa taji la Kombe la Uganda 1997.

Mafanikio aliyopata kocha huyo aliyewahi kufundisha soka pia katika nchi za Angola, Ghana, Libya, Qatar, Hungary na Oman ni kama amewafunika wazungu wote waliowahi kutua Simba tangu yeye alipojiondokea zake baada ya kutibuana binafsi na mmoja wa mabosi wa Msimbazi kipindi hicho.

Baada ya hapo kila kocha wa kigeni akitua Msimbazi anaendelea kusumbuliwa na jinamizi la kocha huyo mwaka 2019 alirejea nchini kuinoa Singida United, lakini alitimka kutokana na mazingira ya kufanyia kazi.

KOCHA MPYA

Hata kama Simba itafanikiwa kumpata kocha mpya wa kigeni, bado kocha huyo ajaye atakuwa na kazi kubwa ya kupambana na jinamizi hilo la Popadic, kwani hakuna kocha aliyedumu kwa muda mrefu na kubeba mataji mengi kama mwamba huyo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 77.

Ingawa wapo makocha wa kigeni waliojitutumua kuifanya Simba itishe uwanjani kama ilivyokuwa kwa Siang’a, Patrick Ausseum, Sven Vandenbroeck na wengineo, lakini bado rekodi za Popadic zinaendelea kudumu, japo ipo siku isiyo na jina kuna kidume kimoja kitakuja kufuta kila kitu na kuweka rekodi yake. Tusubiri!

Chanzo: www.tanzaniaweb.live