Mauricio Pochettino anapewa nafasi kubwa ya kuchukua mikoba ya kuinoa Chelsea msimu ujao. Kocha huyo Muargentina anapewa nafasi hiyo baada ya Julian Nagelsmann kujiondoa kwenye mchakato huo huo wa kuchukua kazi ya ukocha Stamford Bridge.
Kwa sasa Pochettino ndiye anayeshika namba moja kwenye orodha ya makocha watatu wanaopewa nafasi kubwa ya kuinoa Chelsea, huku wengine ni Vincent Kompany na Ange Postecoglou. Kocha Luis Enrique naye anahusishwa na kibarua hicho cha Stamford Bridge.
Pochettino akitua Chelsea, atakwenda kutambulisha soka la kushambulia kama alivyokuwa Tottenham. Jambo hilo litawafanya Chelsea kuachana na fomesheni yao pendwa ya 3-4-3, ambayo ilikuwa ikipendelewa na kocha Antonio Conte alipokuwa hapo mwaka 2016.
Hicho, Pochettino atakuja na fomesheni ya 4-2-3-1 na kwamba atatoa nafasi kwa vijana, huku Kepa Arrizabalaga akitarajia kuwa kipa wake na Reece James na beki wa kulia na Ben Chilwell atacheza kushoto.
Thiago Silva na Kalidou Koulibaly watakaa benchi kuwaacha vijana Wesley Fofana na Benoit Badiashile kucheza kwenye beki ya kati. N'Golo Kante ataendelea kubaki kwenye eneo la kiungo sambamba na Enzo Fernandez.
Noni Madueke atarejea kwenye kikosi cha The Blues wakicheza winga ya kulia na Mykhailo Mudryk atakuwa kushoto. Christopher Nkunku ambaye atatua Stamford Bridge akitokea RB Leipzig, atasimama kwenye nafasi ya mshambuliaji wa kati, huku Romelu Lukaku na Pierre-Emerick Aubameyang watabaki kwenye benchi kuongeza nguvu.
Mfumo mwingine ambao Pochettino anaweza kutumia ni 4-3-3, ambapo Chelsea itatumia itakapowasajili Victor Osimhen na Harry Kane, ambao imekuwa ikihusishwa nao.