Kikosi cha Simba kinaendelea kujifua jijini Ismailia, Misri huku mastaa wa timu hiyo wakizidi kuimarika, lakini beki wa zamani wa Yanga ametuma salamu Jangwani akisema staa mpya wa Wekundu wa Msimbazi, Augustine Okrah sio mtu mzuri na lazima wajipange vizuri kwa msimu ujao.
Beki huyo Mghana Joseph Tetteh Zutah, aliyewahi kukipiga Yanga msimu wa 2015-2016 akisajiliwa kutoka Medeama ya Ghana, aliliambia Mwanaspoti kwa njia ya simu kitendo cha Okrah kutua Simba sio habari njema kwa Yanga na timu pinzani nyingine hasa akiangalia uwepo wa mastaa wengine wa maana kikosini.
Zutah, aliyecheza na Okrah msimu uliopita katika Ligi Kuu ya Ghana alisema kiungo mshambuliaji huyo ni fundi wa kupangua mabeki, hivyo atasumbua sana msimu unaoanza Agosti 17.
“Najua Okrah yupo Simba, ni mchezaji bora sana, sio kitu rahisi kwa mchezaji wa hapa kuwa na nafasi hata ya kucheza Black Stars B au ile ya CHAN, ni mchezaji ambaye akiwa na mpira mguu wa kushoto lazima beki ushtuke na ajipange kumzuia,” alisema Zutah.
“Naijua Ligi ya Tanzania ina ushindani zipo timu ngumu lakini Okrah atasumbua kama hawatajajipanga kumzuia, ni mchezaji fundi na ana nguvu za kupambana.”
Alisema Okrah mbali na kujua kuwasumbua mabeki pia anajua kufunga mabao ambayo ameyafunga msimu uliopita yanatosha kujieleza juu ya ubora wake.
“Amefunga mabao mengi hapa msimu uliopita, na amekuwa akibadilishwa nafasi tofauti, anajua pia kutoa pasi za mabao, kuna wakati amekuwa akifunga mabao wakati makipa hawajajipanga.
Msimu uliopita akiwa Ligi Kuu ya Ghana Okrah amefunga mabao 14 huku akitoa pasi tatu za mabao na tayari katika mechi mbili za kirafiki alizocheza akiwa na jezi ya Simba kiungo huyo mshambuliaji ameshafunga bao moja.