Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mziba, Boban waichambua Ligi Kuu Bara

Yangasc Kombe 2024 Mziba, Boban waichambua Ligi Kuu Bara

Fri, 31 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya msimu wa Ligi Kuu Bara kumalizika Jumanne ya Mei 28, 2024, mastaa wa zamani na makocha wamechambua ubora na mambo ya kufayafanyia marekebisho kwa ajili ya msimu ujao.

Mwanaspoti limezungumza na wataalamu wa soka hao kwa nyakati tofauti, kitu kikubwa walichokitaja kinahitaji maboresho ni ukarabati wa viwanja pamoja na ratiba izingatie ramani za timu.

Ikumbukwe kwamba, msimu wa 2023/24 Yanga imetetea ubingwa wa ligi hiyo, Azam ikishika nafasi ya pili. Timu hizo zinakwenda kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Simba na Coastal Union zitashiriki Kombe la Shirikisho Afrika kutokana na kumaliza nafasi ya tatu na nne.

Geita Gold na Mtibwa Sugar zimeshuka daraja kwa kukamata nafasi ya 15 na 16, huku JKT Tanzania na Tabora United zikienda kujiuliza kwenye play-offs.

Hata chini ni baadhi ya makocha na mastaa wa zamani waliowahi kutamba katika Ligi Kuu Bara walivyoichambua msimu huo uliomalizika kwa kushuhudiwa wakongwe Mtibwa Sugar na Geita Gold zikishuka daraja, huku JKT Tanzania na Tabora United zikiangukia mechi za play-offs.

ABEID MZIBA

Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Abeid Mziba 'Tekelo' anasema kitendo cha vitendawili vingi kusubiri dakika 90 za mwisho za msimu ili kuteguliwa kinathibitisha ubora wa ligi.

Ukiacha Yanga iliyotwaa ubingwa mapema kabla ya mechi tatu na Mtibwa Sugar iliyoshuka daraja kabla ya mechi moja, maswali mengi kama kutojulikana nafasi ya pili angekuwa Simba au Azam FC, vita ya kiatu cha ufungaji bora na kipa bora, timu ya kuungana na Mtibwa kushuka daraja, timu 10 kutokuwa na uhakika wa kubaki Ligi Kuu, yote yalisubiri dakika 90 za mechi za mwisho ili kupata majibu.

"Ligi imekuwa bora, dakika 90 kwenye mechi za mwisho zimeamua Azam FC kushika nafasi ya pili ikiipiku Simba, Stephane Aziz Ki kumshinda Feisal Salum 'Fei Toto katika vita ya muda mrefu ya kiatu cha dhahabu, Geita Gold kushuka daraja na Tabora United kucheza mtoano," anasema.

HARUNA MOSHI 'BOBAN'

Kiungo wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Haruna Moshi 'Boban' anasema ligi ya msimu huu, ilikuwa bora na ushindani wa wachezaji wa kigeni na wazawa.

"Kitu ninachokiona cha kuboresha ni kuongezeka kwa dhamini ili timu zote zijiweze kipesa, itasaidia wachezaji kubadili mtazamo wa kuona Simba, Yanga na Azam ndizo zinazoweza kuwatoa kimaisha," anasema.

ABDI KASSIM 'BABI'

Mshambuliaji wa zamani wa Yanga na timu za taifa Stars na Zanzibar Heroes, Abdi Kassim 'Babi' kwa upande wake anaona maboresho yafanyike kukarabati viwanja, ili eneo la kuchezea liwe zuri, kuwarahisishia wachezaji kuonyesha ubora wa viwango vyao.

"TFF iweke mfumo wa kuwasomesha viongozi wa mpira, ili kujua majukumu ya mpira kama kuishi na wachezaji, maana kuna baadhi ya nidhamu mbovu za wachezaji zinasababishwa na baadhi yao.

"Viongozi wakipata elimu ya uendeshaji wa majukumu yao kisoka, kesi za wachezaji kuwashitaki CAF, FIFA zitapungua, katika hilo wawemo na waamuzi kupata mafunzo ya mara kwa mara na ikiwezekana walipiwe kozi, pamoja na hayo yote, nawapongeza rais wa TFF, Wallace Karia na katibu Wilfred Kidau, wamefanya kazi kubwa ya kuboresha ligi.

Kwa upande wa mchezaji bora wa msimu, kura yake aliitoa kwa kiungo wa Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto', akitoa sababu ya mabao yake ni juhudi binafsi, akitofautisha na Aziz Ki aliyezungukwa na wachezaji wengi wazuri ndani ya kikosi cha Yanga.

KIPANYA MALAPA

Mchezaji wa zamani wa Yanga na Singida United, Kipanya Malapa anasema: "Kwanza naipongeza Yanga kwa kuchukua ubingwa mara tatu mfululizo, imeonyesha jinsi ilivyosajili wachezaji wazuri, hilo liwe mfano kwa timu nyingine kujipanga, kilichonifurahisha zaidi ni vita ya ufungaji baina ya Aziz Ki na Fei Toto pia nafasi ya pili kati ya Azam na Simba.

AMIR MAFTAH

Beki wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Maftah anasema ligi ilikuwa ngumu yenye ushindani ambao ulikuwa unatoa burudani kwa mashabiki, hivyo anaamini msimu ujao, timu zitajipanga zaidi kwa usajili na kuwania taji ambalo Yanga imelichukua mara tatu mfululizo.

"Niipongeze Yanga kwa kuchukua ubingwa, inatoa changamoto kwa timu nyingine kujipanga na kusajili vizuri, kitu kizuri kingine nilichokipenda mechi za mwisho ndizo zilizotoa picha ya timu inayomaliza nafasi ya pili, timu nyingine iliyoshuka baada ya Mtibwa Sugar na zinazocheza mtoano.

"Changamoto ilikuwa kwa baadhi ya viwanja, unaona kabisa vinapunguza ufanisi wa wachezaji kuonyesha vipaji vyao halisia, pia ratiba iendane na ramani za timu, mfano kama Prisons inakwenda kucheza Dar es Salaam, basi imalizane na timu zilipo mkoa huo."

MAKOCHA HAWA HAPA

Kocha wa zamani wa Azam FC, Prisons, Mashujaa, meja mstaafu, Abdul Mingange anasema: "Ligi ilikuwa bora, nimeona ushindani wa wazawa na wageni, ila kitu cha kufanyiwa marekebisho ni baadhi ya viwanja."

BONIFACE MKWASA

Kocha wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa, anasema ligi ya msimu ulioisha, ilikuwa ya ushindani, timu iliyowekeza na kusajili vizuri imefanikiwa kuchukua ubingwa.

"Kwa upande wa changamoto vipo viwanja havikuwa bora, ratiba hazikuangalia uelekeo wa timu, kwani zipo zilikuwa zinapata shida kusafiri, maeneo hayo yanapaswa kurekebishwa msimu ujao," anasema.

JAMHURI KIHWELO

Kocha wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo 'Julio' anasema: "Ligi ilikuwa ngumu, imetoa funzo kwa timu kujipanga kwa ajili ya msimu ujao ninaoutarajia utakuwa mzuri zaidi, jambo linalotakiwa kwa sasa, timu zilizopata nafasi za kucheza michuano ya CAF, zijipange ikiwezekana zichukue taji kabisa."

SUNDAY KAYUNI

Kocha mkongwe Sunday Kayuni, anasema kinachozisumbua timu nyingi hazina falsafa ya timu, hivyo alizishauri zijenge utaratibu huo ili zinaposajili makocha wanakuwa wanaingia kwenye mifumo yao.

"Ulaya timu zina falsafa zake, hivyo zinakuwa zinaajiri maskauti wanaotafuta wachezaji wanaoendana na falsafa za klabu, hata wakitafuta kocha anakuwa wa aina hiyo, zikifanya hivyo naamini zinazopata nafasi za kucheza michuano ya CAF, itakuwa rahisi kuchukua ubingwa."

"Pamoja na hayo yote ligi ilikuwa nzuri na ya ushindani, nimeona namna ambavyo ilikuwepo vita ya kuwania kiatu cha dhahabu cha mfungaji bora, nafasi ya pili, pia zilizokuwa zinashuka daraja."

Kayuni ni kocha aliye na rekodi ya kipekee, aliyetwaa ubingwa nje ya nchi mwaka 1998 aliipa ubingwa AFC Leopards ya Kenya.

DONDOO MUHIMU

Timu iliyofunga mabao mengi: Yanga (71)

Timu iliyofunga mabao machache: Geita Gold (18)

Timu iliyofungwa mabao mengi: Mtibwa Sugar (54)

Timu iliyofungwa mabao machache: Yanga (14)

Timu yenye clean sheets nyingi: Yanga (19)

Timu iliyoshinda mechi nyingi: Yanga (26/30)

Timu iliyopoteza mechi nyingi: Mtibwa (19/30)

Timu iliyopoteza mechi chache: Yanga (2/30)

Timu iliyotoa sare nyingi: JKT Tanzania (14)

Timu iliyotoa sare chache: Yanga (2)

Chanzo: Mwanaspoti