Dar es Salaam. Baba mzazi wa Mbwana Samatta, Ally Samatta amesema mwanae kuvaa beji ya unahodha wakati timu yake KRC Genk ikicheza na Napoli, Ligi ya Mabingwa Ulaya imemuongezea thamani ya kazi yake.
Mzee Samatta alisema haijalishi KRC Genk kutoka suluhu katika mchezo huo, jambo kubwa ni kijana wake kupewa heshima ya kitambaa, jambo analoamini linaendelea kumpa thamani mbele ya timu zinazomuhitaji.
Alisema Samatta kwa sasa anatazamwa na klabu mbalimbali za Ulaya hivyo kocha wake wa KRC Genk, kumpa dhamana ya kitambaa anamsaidia kumtengenezea heshima kubwa zaidi.
"Napoli ni klabu kubwa, naamini Samatta atajivunia kuvaa beji ya unahodha na anaendelea kujiwekea rekodi ambazo zitakuwa zinakumbukwa, mfano kuwa Mtanzania wa kwanza kuwa nahodha wa mchezo huo."
"Huwa nazungumza naye baada ya mchezo, jambo kubwa namsisitiza kujituma hata yeye mwenyewe ananiambia malengo yake kupitia Ligi ya Mabingwa Ulaya," alisema Mzee Samatta.