Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mzee Ruksa alivyochangamsha michezo

Mwinyi Afariki Mzee Ruksa alivyochangamsha michezo

Sat, 2 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mzee Ruksa ameumaliza mwendo. Miaka 98 ya uhai wake duniani imefikia tamati juzi Februari 29 baada ya kutangazwa amefariki dunia. Alikuwa amekabakisha miaka miwili tu kutimiza karne moja. Sio haba na shukrani ni kwa Mungu aliyempa umri mrefu ambao watu wengi wanautamani.

Leo hii mwili wa Rais huyo wa Serikali ya Awamu ya Pili ya Tanzania, Ali Hassan Mwingi utahifadhiwa katika nyuma yake ya milele. Ni kweli hatutamuona tena kipenzi chetu.

Hakuna ubishi, Mzee Ruksa ameondoka. Ameondoka akituachia upweke, lakini akituachia pia alama nyingi za kukumbukwa katika sekta mbalimbali ikiwemo michezo na burudani katika kipindi cha utawala wake uliodumu kwa miaka 10.

Awamu ya pili ya uongozi wa Mzee Ruksa kwa waliosahau ilianza Novemba 5, 1985 baada ya Rais wa Awamu ya Kwanza na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kung'atuka na iliishia Novemba 23, 1995 alipompisha Benjamin Mkapa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu ambaye kama ilivyo kwa watangulizi wake, naye amelala kaburini kwa sasa.

Kama hujui ni kwamba katika kipindi cha Mzee Ruksa kuna matukio mengi yaliyobaki katika kumbukumbu ya wanamichezo nchini, kuanzia kwenye michezo hadi katika burudani na ndipo kulipoibuka ule msemo wa 'Tanzania Kichwa cha Mwendawazimu' aliyoitoa Mzee Mwinyi baada ya kukerwa kutokana na kufanya vibaya kwa timu zetu.

Wakati Watanzania hususani wanamichezo na wasanii wakiendelea kumlilia na kumuomboleza Rais huyo kipenzi cha wengi, Mwanaspoti inakuletea baadhi ya matukio muhimu yaliyofanyika enzi za utawala wa Mzee Ruksa na ambayo yataendelea kukumbukwa milele wakati mwili wake ukiandaliwa kwenda kuhifadhi baada ya jana kuagwa kwenye Uwanja wa Uhuru (zamani Taifa) wenye historia kubwa dhidi yake enzi za uhai wake katika sekta hizo.

KICHWA CHA MWENZAWAZIMU

Hii ni moja ya kauli iliyokuwa maarufu iliyodumu kwa muda wa miaka 25 aliyowahi kuitoa Mzee Mwinyi enzi za uhai wake, baada ya kushuhudia Simba ikipoteza mchezo wa pili wa fainali ya michuano ya Kombe la CAF 1993 mbele ya Stella Abidjan ya Ivory Coast uliopigwa Novemba 27, mwaka huo kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru).

Simba iliandika rekodi ya kuwa klabu ya kwanza kipindi hicho kufika fainali katika michuano ya CAF kwa ngazi ya klabu na ilicheza mechi ya kwanza dhidi ya Stella, mjini Abidjan na kutoka suluhu kiasi kwamba aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Amri Bamchawi kuanza kupanga kabisa sehemu zitakazotembezwa taji hilo, kwa kuamini ingelitwaa katika mchezo wa marudiano ambao Mzee Ruksa enzi hizo akiwa ndiye Rais wa Tanzania alikuwa mgeni rasmi.

Jeuri hiyo ilitokana na ukweli kwamba Simba ilikuwa imekamilika kwelikweli na hadi kufika fainali ilivitoa vigogo kweli kweli tena kwa idadi kubwa ya mabao na ndio maana walimualika Mzee Mwinyi ili ashuhudie historia ikiandikwa kwa timu hiyo kubeba ndoo ya kwanza ya Afrika katika mchezo huo wa marudiano.

Hata hivyo, kilichotokea ni kwamba Simba ilikufa mabao 2-0 yaliyofungwa na Boli Zozo kisha Stella ikaondoka na taji hilo ikikabidhiwa na Mzee Ruksa ambaye baadaye akikaririwa kwenye hotuba zake akisema Tanzania imekuwa kama 'kichwa cha mwendawazimu', akimaanisha kila mtu anaitumia kujifunzia kunyoa kutokana na timu za Tanzania kufanya vibaya katika michuano ya kimataifa.

Kauli hiyo ya mwaka 1993 iliendelea kuzitesa timu za Tanzania hadi alipotangaza mwenyewe kuifuta Mei 9, 2021.

Mzee Mwinyi aliifuita kauli hiyo kwenye hafla ya utoaji wa tuzo za Simba 'Mo Simba Awards' alipoalikwa kama mgeni rasmi wakati akiikabidhi tuzo ya heshima iliyochukuliwa na kocha msaidizi wa sasa wa Simba, Selemani Matola kisha kuondoka ukumbini.

TANZANIA KUNG'ARA Licha ya kauli hiyo ya Mzee Mwinyi aliyoitoa enzi hizo kabla ya kuja kuifuta, lakini kipindi cha uongozi wake timu za Tanzania zilitamba Afrika Mashariki na Kati pamoja na Afrika kwa ujumla kwa kufika hatua mbalimbali kwenye michuano ya kimataifa.

Ni katika kipindi cha Mwinyi ndipo iliposhuhudiwa timu za Tanzania zikitwaa ubingwa wa michuano ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kagame) mara nyingi zaidi kuliko awamu nyingine zote.

Simba na Yanga zilitwaa mfululizo taji hilo kwa misimu mitatu kuanzia 1991, 1992 na 1993 kisha zikapozi kwa msimu mmoja kabla ya kubeba tena 1994. Miaka ya 1991, 1992 na 1995 Simba ndio waliobeba taji na ule wa mwaka 1993 lilibebwa na Yanga tena katika ardhi ya Kampala, Uganda ikiwa ni klabu ya kwanza na pekee kubeba taji hilo nje ya Tanzania.

Hiyo ilikuwa ni rekodi kwani katika Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Nyerere, klabu za Tanzania zilitwaa taji hilo mara mbili 1974 na 1975 kupitia Simba na Yanga, huku Awamu ya Tatu ya Benjamin Mkapa zilitwaa mara tatu 1996, 1999 na 2002, kupitia pia Simba (1996 na 2002) na Yanga (1999, ikibeba tena Kampala Uganda).

Wakati wa utawala wa Awamu ya Nne wa Jakaya Kikwete, timu za Tanzania kutwaa Kagame Cup ilikuwa pia ni mara tatu 2011, 2012 lililobebwa na Yanga na 2015 ilipobeba Azam na kwa Awamu ya Tano ya Dk John Magufuli ilikuwa ni mara moja 2018 ikiwa ni Azam pia.

Sio kwenye michuano ya Kagame tu, lakini hata katika michuano ya CAF ndipo rekodi zilipoandikwa kwa Simba kufika fainali za Kombe la CAF na pia kutinga robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa) mwaka 1994.

Ni mwaka huo pia ambao Malindi ya Zanzibar nayo ilifika robo fainali ya Kombe la Washindi kabla ya Yanga kufanya Malindi pia iliandika historia ya kuwa klabu ya kwanza ya Zanzibar kufika nusu fainali ya michuano ya Afrika baada ya kufanya hivyo mwaka 1995 katika michuano ya Kombe la CAF ambayo ilikuja kuunganishwa na ile ya Washindi mwaka 2004 na kuzaliwa Kombe la Shirikisho Afrika la sasa.

Hata upande wa timu za taifa za Tanzania Bara na Zanzibar zilitwaa ubingwa wa Nchi za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) Kombe la Chalenji mwaka 1994 ikiwa ni miaka 20 tangu (Bara) ilipokuwa imetwaa mara ya mwisho 1974 enzi za Mwalimu Nyerere na msimu uliofuata ilipokewa na ndugu zao wa Zanzibar iliyobeba 1995.

Cha Ajabu mara zote iliziangusha Uganda The Cranes katika mechi hizo zikifanyika nje ya Tanzania. Kilimanjaro Stars ilibebea Nairobi, Kenya na Zanzibar ilitwaa ikiwa Uganda.

MISS TANZANIA Kipindi cha Mzee Ruksa ndipo shindano maarufu la Miss Tanzania lilirejea baada ya kufungwa na serikali mwaka 1968 ikiwa ni mwaka mmoja tangu lilipoasisiwa 1967 enzi za Awamu ya Kwanza.

Shindano hilo lilirudi mwaka 1994 na kushuhudia kwa mara ya kwanza mrembo Aina Maeda akitwaa taji hilo kisha kufungua neema kwa wadau mbalimbali wa fani hiyo wakiwamo wasichana walioshiriki na wale waliokuwa wakiratibu na kupromoti shindano hilo ambalo kwa sasa limepoteza ule umaarufu uliokuwapo.

Shindano hilo ndilo lililowaibuka mastaa mbalimbali ambao leo wanatamba kwenye siasa, uigizaji na sekta nyingine kama Wema Sepetu, Basila Mwanukuzi, Saida Kessy, Hoyce Temu, Jacqueline Ntuyabaliwe, Happiness Megese. Faraja Kota, Nancy Sumari, Lisa Jensen, Happiness Watimanywa, Irene Uwoya, Aunty Ezekiel na wengineo.

WAFADHILI MICHEZONI Ni kweli miaka ya nyuma kuna wafadhili mbalimbali walijitokeza na kusaidia maendeleo ya michezo hasa klabu za soka kama kina Tabu Mangara, Sam Mdee na wengine, lakini hakuna kipindi kilichokuwa cha neema kwa wachezaji kama enzi za utawala wa Mzee Ruksa ambapo wafanyabiashara walijitosa katika michezo.

Watu kama kina Azim Dewji, Murtaza Dewji, Ramnik Patel 'Kaka', Mohammed Viran, Abbas Gulaman, Ramesh Patel, Ramesh Patwa, Mohammed Naushad na wengineo walitetemesha kwenye soka la Tanzania kupitia klabu mbalimbali kama Simba, Yanga, Pan African, Tukuyu Stars na Malindi.

Wapo wengine walijitosa kwenye ngumi na kuchangia kuamsha ngumi za kulipwa chini ya kina Philemon Kyando zilizoendezwa zaidi kipindi cha Awamu ya Tatu ya Mkapa ikiwa na kina Dioniz na Jamal Malinzi kupitia DJB Promotion waliowaibua kila Rashid Matumla aliyekacha ngumi za ridhaa kuingia za kulipwa na kuiletea heshima kubwa Tanzania kimataifa aliyebeba mikanda mikubwa inayotambulika.

Ni kipindi hicho kwa wafanyabiashara hao ambao wachezaji walikuwa wakilipwa fedha nyingi kama wachezaji wa kulipwa kutoka kucheza michezo kama burudani tu, ndio maana ilishuhudiwa wachezaji wa mataifa mbalimbali wakisajiliwa kwa fujo na klabu za Tanzania na kuzifanya kuwa tishio Afrika.

Utabisha nini wakati Naushad na Malindi yake ikimleta beki wa kimataifa kutoka Zambia, Maldon Malitoli na Julian Albertov kutoka Bulgaria, mbali na wakali wengine wa Tanzania Bara walioifanya klabu hiyo kuandika rekodi kadhaa katika michuano ya CAF, mbali na nyota wa Simba kufikia hatua ya kuzawadiwa televisheni na magari kipindi ambacho vifaa hivyo vilionekana ni anasa kubwa.

FANI YA MUZIKI Kipindi cha utawala wa Mzee Ruksa hata kwenye fani ya muziki mambo yalikuwa mambo kwani ndipo kulikowaibua madansa mbalimbali waliokuwa wakichuana kwenye mashindano ya disko hata kama fani hiyo ilianza tangu utawala wa Awamu ya Kwanza.

Majina makubwa kama ya Black Moses, Athuman Digadiga, Bosco Cool J, MC Cool J, Kadet Bongoman, Cocorico, Fatuma Timbanga, Maxi, MCD, Super Ngedere, Mitikas na wengineo waliofikia hatua ya kuchuana na madansa kutoka nchi jirani za Kenya na Uganda kama kina Kanda Kid yaliibukia hapo na kila kijana alitamani kuwa dansa.

Mapromota mbalimbali wa muziki wa dansi waliibuka na kuifanya miji kutikisika kila wikiendi kwa mashindano mbalimbali ya madansa majina makubwa zaidi yakiwa ya kila John Ng'ogo na wengineo, huku kwenye muziki wa dansi nako mambo yalikuwa moto kwelikweli kwa wanamuziki kununuliwa na kugombewa kwa bei mbaya.

Ushindani wa makundi ya muziki wa dansi ulihamia hata kwenye muziki wa taarabu kutokana mazingira yaliyotengenezwa na uongozi wa Awamu ya Pili yaliyoleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi baada ya muwambo wa hali ngumu iliyowaumiza wananchi iliyochangiwa zaidi na Vita vya Kagera vilivyopiganwa mwaka 1978-1979.

Ni kipindi hicho ndipo bendi na makundi mbalimbali yaliyoasisiwa na kuongeza ajira kwa Watanzania kuanzia wasanii wenye vipaji hadi wamiliki na wadau wengine wakiwamo wamiliki wa makundi mbalimbali za burudani.

Hata fani ya uigizaji nayo haikuachwa nyuma katika utawala wa Mzee Ruksa kilichokuwa kipindi ca soko huria ambapo ndipo ilipoasisiwa Bongo Movie.

Filamu kama Shamba Kubwa, Unga Adui zilizopigwa miaka ya 1994 na 1995 chini ya kina J Plus ni kati ya historia inayoendelea kuishi kama kumbukumbu isiyofutika ya utawala wa wa Awamu ya Pili ya Mzee Mwinyi, kwani ndio iliyofungulia fani hiyo inayoendelea kutamba kwa sasa nchini kupitia vituo mbalimbali.

Wasanii kama kina Bi Chau, Mzee Small, King Majuto, Mwanachia, Qudrat Olomoda 'Chombeza' na wengineo walianza kuonekana kupitia runinga baada ya vituo mbalimbali vya televisheni kuanzishwa nchini enzi za utawala huo kama vile CTN, CEN, DTV, ITV na vinginevyo vilivyoleta maonyesho ya redioni na majukwaani yaliyokuwa yakifanyika enzi za Awamu ya Kwanza kuhamia huko na kutangaza zaidi fani ya uigizaji na uchekeshaji.

ALIKUWA MNYAMA Licha ya kwamba mwenyewe enzi za uhai wake hakuwahi kutamka hadharani, lakini wanaomjua kwa undani wanasema Mzee Ruksa alikuwa 'Mnyama' kwelikweli na aliumizwa pale Simba ilipopata matokeo mabaya.

Mwenyewe aliwahi kukaririwa alipotembelewa hivi karibuni na wakongwe wa zamani katika kuadhimisha miaka 98 ya umri wake, akisema aliwahi kucheza soka enzi za ujana akiwa ni beki wa kati, kuonyesha jinsi gani soka ni kitu alichopenda kama kule kufanya mazoezi.

Inaelezwa katika maisha yake hadi anakumbwa na mauti alipenda sana kufanya mazoezi ndio maana alionekana ngangari kulinganisha na umri mkubwa aliokuwa nao.

Hata hivyo, ameondoka akiwa anakumbukwa kutokana na uwanja wa kwanza wa kisasa nchini wa Ali Hassan Mwinyi uliopo mjini Tabora uliopewa jina lake.

Kwa hakika Mzee Ruksa ameacha pengo kubwa kwa familia ya wanamichezo na burudani, lakini pia kwa kuwa kazi ya Mungu haina makosa tumuombee kila la heri katika safari yake, kwani sisi ni waja wa Mola na kwake tutarejea.

Chanzo: Mwanaspoti