Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mzee Msekwa aeleza upekee katiba mpya

Msekwa Dss Mzee Pius Msekwa

Mon, 12 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwanasiasa mkongwe nchini, Pius Msekwa ameeleza upekee wa mchakato wa katiba mpya ambao Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeazimia kuufufua.

Msekwa amesema kitu cha kipekee kilichomo kwenye mchakato huo wa kupata katiba mpya ulioanzishwa na Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, ni utaratibu wa wananchi kupiga kura za maoni za kuidhinisha pendekezo hilo la katiba lililotolewa na Bunge la Katiba.

Akizungumza na waandishi wa habari wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) nyumbani kwake Ukerewe mkoani Mwanza hivi karibuni, Msekwa alisema anachotaka kufanya Rais Samia ni kufufua mchakato huo ukamilike.

Alisema utaratibu wa kupiga kura, ndio jambo jipya tofauti na katiba zote mpya za nyuma, ikiwamo Katiba ya Jamhuri ya Tanganyika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo hazikwenda kwenye kura za maoni bali zilikwenda kwenye Bunge la Katiba.

Alisema Bunge la Katiba likishapitisha, katiba inaanza kufanya kazi mara moja. “Rais wa sasa anaufufua mchakato ili ukamilike, ndiyo maana yake halisi na ndiyo maana ya jambo hili, si kwamba linaanza upya. Hapana. Lilishaanza, halikukamilika, sasa Rais wa Awamu ya Sita analikwamua ili liweze kukamilika,” alisema.

Aliongeza, “sasa litaanzia pale tulipoishia au litaanza upya kabisa, hayo ni mambo mengine, lakini kimsingi anaendeleza mchakato ulianzishwa na mtangulizi wake Rais Kikwete wa kuwa na katiba mpya ya nchi hii.”

Mmomonyoko maadili

Kuhusu mmomonyoko wa maadili, Msekwa alisema taifa halijakosea mahali popote bali ni tatizo la kibinadamu kama uhalifu mwingine wowote.

“Mtu hawezi kuhoji leo kuwa watu wanaiba mali za wenzao hivyo taifa limekosea wapi? Hapana, wapo binadamu wana hulka ya wizi tu tangu dunia ilipoumbwa,…huwezi kusema tulikosea kuanzia mahali fulani,” alisema.

Aliongeza, “mauaji, watu kuua wenzao hayajaanza leo wala jana au tarehe fulani, mauaji yamekuwepo tangu dunia ilipoumbwa, hata maandiko ya Biblia yanatuambia Kaini alimuua Abeli, sasa hiyo huwezi kuhoji wanaoua baada ya yeye wanakosea wapi.”

Msekwa amewataka Watanzania kuzingatia kuwa hayo ni matatizo ya kibinadamu na yamekuwepo siku zote. Alisema ni kosa kuanza kulaumu kizazi fulani kuhusu mmomonyoko wa maadili.

“Napenda kushawishi kwamba tusikimbilie kudhani taifa limekosea mahali fulani, halijakosea mahali popote, … mimi napenda tulione jambo hili kwa usahihi wake, hakuna kizazi cha kulaumu, hakuna mahali tumekosea,”alisisitiza.

Msekwa alisema hakuna namna ya kuzuia makosa bali njia pekee ni kuwaadhibu wakosaji ili kuweka tishio kwa wengine wenye mawazo au nia ya kufanya hivyo wajue kuwa wakifanya watakamatwa na kuadhibiwa.

Alisisitiza, “narudia kwamba hakuna kizazi cha kulaumu na wala hakuna sababu ya kulaumu kwa sababu ndivyo mambo yalivyo katika jamii ya binadamu tena si katika nchi moja.”

Alisema mambo hayo yapo katika nchi zote na si maalumu kwa Tanzania pekee. “Kila nchi ina matatizo ya wizi, mauaji, ubakaji na kukiuka maadili,” alisema.

Afurahia nchi inavyokwenda

Akizungumzia nchi kwa ujumla, alisema anatamani kuendelea kuiona Tanzania yenye amani, utulivu na maendeleo kwa kuwa mambo hayo yanapokuwapo kila mtu anafurahi.

Alisema hadhani kama kuna mtu anaweza kutamani zaidi ya mambo hayo matatu.

“Natamani tuwe kama wengine wote, natamani tuwe na Tanzania yenye amani, utulivu na maendeleo, vitu hivyo ndiyo kila mtu anavitamani, vinapopatikana kila mtu anafurahi na kusifia walioviwezesha kuwepo, sidhani kama unaweza kutamani zaidi ya hapo,”alisema.

Anaongeza “Sisi wote ni viumbe wa Mwenyezi Mungu, mengi yanatokea kama anavyotaka yeye, kwa hiyo sisi tunaamini hivyo na tunaendelea kuamini hivyo, matakwa au matamanio ya mtu mmoja hayana nafasi kabisa katika hilo.”

“Kwa msingi huo, mimi sina ninachokitamani, ninachokiona leo kinaniridhisha, ninachokiona leo amani, utulivu na maendeleo yanaridhisha kabisa, naomba Mwenyezi Mungu atujalie tuendelee hivyo hivyo.”

Alisema anafurahi kuona Tanzania inakwenda vizuri chini ya kila kiongozi na inakwenda vizuri zaidi chini ya kiongozi wa Awamu ya Sita, Rais Samia Suluhu Hassan.

Msekwa alisema anaungana na wengi wanaotoa maoni yao kwenye vyombo vya habari kusifia awamu mbili za uongozi wa Rais John Magufuli kwa kuanza kuendeleza mambo makubwa aliyoyaanzisha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Asifu uendelezaji miradi

Miradi hiyo mikubwa ni pamoja na Bwawa la kufufua umeme la Julius Nyerere katika Mto Rufiji na ujenzi wa Ikulu ya Chamwino iliasisiwa na Mwalimu Nyerere lakini ikakwama kutokana na sababu zinazojulikana za uwezo wa nchi kifedha.

Alisifu hatua ya Rais Magufuli kuanzisha miradi hiyo kwa nguvu na kisha Rais Samia kuiendeleza kwa nguvu na kasi ileile na kuanzisha mingine mipya. Alisema hayo yote yanafanyika kwa manufaa ya maendeleo ya nchi.

“Kwa kweli sisi tulio wengi tunaridhika kwamba mambo ya nchi yetu yanakwenda vizuri sana hasa yale ambayo yaliachwa na Mwalimu Nyerere, angekuwepo hai leo angetamka mwenyewe furaha yake kwamba yale aliyoyaanzisha yamewezekana, ndiyo hali halisi tunavyoiona sisi wastaafu,” anasema.

Jicho la wastaafu

Wakati huo huo Msekwa ameeleza kanuni ambayo viongozi wakuu wa nchi wastaafu wamejiwekea ya kutoingilia kazi za waliopo madarakani kwa maana ya kuwasimamia au kuwakosoa, isipokuwa kutoa ushauri endapo wanaona mambo yanaweza kuharibika.

Alisema jambo ambalo halijulikani kwa watu wengi ni kwamba, viongozi wakuu wastaafu wakiwemo wenyeviti wa CCM taifa ambao ni marais wa nchi na Makamu Wenyeviti wa CCM, ndio wanaojulikana kama viongozi wakuu wa nchi.

Alisema kwenye Katiba ya CCM, kipo kifungu kinachosema kuwa kutakuwa na Kamati ya Viongozi Wakuu wa chama ambao kazi yao ni kutoa ushauri kwa chama kuhusu mambo yanavyokwenda.

Kutokana na hilo, anasema anayo nafasi kwenye kamati hiyo kwa kuwa aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara wakati Mwenyekiti akiwa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kwa miaka yote 10.

Alisema yeye pamoja na marais wastaafu wa Muungano na Marais wastaafu wa Zanzibar, ni wajumbe wa kamati hiyo na kikatiba, marais wa Zanzibar moja kwa moja wanakuwa Makamu Wenyeviti wa CCM.

Msekwa alisema Rais Samia hajaingia kwenye jopo hilo kwa kuwa bado yupo madarakani. “Kwa hiyo nina nafasi binafsi si ya kutoa ushauri na kuyatazama mambo kwa mtazamo wangu peke yangu bali tunayatazama kwa pamoja,” alisema.

Aliongeza; “Ila tumekubaliana tusiingilie kazi za waliopo madarakani, sisi muda wetu umepita, tutatoa ushauri pale ambapo tunaona mambo kweli yanaweza yakaharibika tusipoyazungumza.”

Aliongeza; “Vinginevyo tuache walio madarakani wafanye kazi zao, isiwe kazi yetu kuwasimamia au kuwakosoa, hapana, tuna msimamo huu, ni kanuni tumejiwekea.”

Alisema: “Ni mara chache, huwa wanatoa maoni ya kusaidia walioko madarakani katika jambo fulani na hii inatokana na hoja hiyo hiyo kwamba wawaache walio madarakani wafanye kazi zao kwa utulivu.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live