Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mzee Baraka Kitenge na maajabu ya enzi zake Yanga

Baraka Kitenge Said Mzee Baraka Kitenge na maajabu yake Yanga

Wed, 20 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baraka Kitenge alizaliwa mwaka 1942 mkoani Tabora na alianza kucheza soka akiwa na umri wa miaka 8 akiwa shule ya msingi Town School.

Alijiunga na shule ya sekondari ya Kazima iliyopo Tabora na kuchaguliwa kwenye timu ya shule pamoja na kuchezea timu ya Young Boys ya Tabora aliyoiwakilisha katika michezo ya ligi.

Wakati huo alikuwa akichezea nafasi ya mshambuliaji namba 9 ingawa pia amewahi kucheza kama winga ya kulia, beki wa kati na beki wa kulia nafasi aliyoichezea hadi alipostaafu.

Wapenzi wa kandanda walimwita 'Askari au Zagallo' wakimfananisha winga wa Brazil enzi hizo, Mario Jose Lobo Zagallo, kwa uwezo wake wa kuwahangaisha washambuliaji.

Mwishoni mwa 1965 baada ya kumaliza kidato cha nne alitimkia Dar es Salaam na kuajiriwa na Shirika la East African Cargo Handling Services, sasa TPA). Mara tu alipowasili Dar es Salaam viongozi wa klabu za soka walianza kumshawishi ajiunge na timu zao, kwani hakuwa mgeni kwao na alijiunga na Yanga SC mnamo 1966.

Mwaka huo huo alichaguliwa kuunda timu Kombaini ya Dar es Salaam kwa ajili ya kugombea Kombe la Taifa pamoja na wanasoka wengine mashuhuri kama Emmanuel Albert Mbele 'Dubwi', Abrahaman Lukongo, golikipa Kitwana Ramadhan Manara 'Popat' ambaye baadaye alikuja kubadilisha nafasi na kuwa mshambuliaji hatari wa Yanga na Taifa Stars, Arthur Mambetta, Mustafa Choteka, na wengineo.

Mwaka 1967 aliliwakilisha taifa katika mashindano ya Kombe la Afrika Mashariki na Kombe la Mataifa Afrika), Madagascar na hapa nyumbani na aliendelea kuichezea Taifa Stars kwa miaka mitatu.

Katika moja ya mahojiano enzi za uhai wake Kitenge alifichua kuwa mchezo mgumu kuliko yote ambayo amewahi kucheza ni kati ya Yanga na Asante Kotoko ya Ghana mwaka 1969 kuwania Kombe la Klabu Bingwa barani Afrika.

Katika mchezo huo wa robo fainali timu zilikwenda sare baada ya dakika 210 nyumbani na ugenini. Sheria ya penati tano tano ilikuwa haijaanza kutumika hivyo Asante Kotoko walipata ushindi wa shilingi.

Baraka Kitenge ambaye pia ni baba wa mtangazaji maarufu Maulid Baraka Kitenge alitundika daluga mnamo 1971 baada ya kuitumikia Yanga kwa miaka mitano. Alifariki dunia Agosti 20, 2013 akiwa na umri wa miaka 74.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live