Kiungo wa Simba, Mzamiru Yassin ameonekana kuwa kwenye kiwango bora siku za hivi karibuni na kuisaidia timu kucheza vizuri jambo lililomuibua kocha wake Juma Mgunda na kufichua siri ya ubora huo.
Mzamiru amekuwa moja ya wachezaji wenye namba ya uhakika ndani ya kikosi cha Simba tangu ameingia Mgunda mwanzoni mwa msimu huu na kuwaweka nje viungo wengine wanaocheza eneo lake wakiwemo, Jonas Mkude, Victor Akpan, Nassor Kapama na Nelson Okwa na hapa Mgunda anafunguka siri ya mafanikio hayo.
“Mzamiru ni mchezaji mzuri sana. Anajua nini afanye akiwa ndani ya uwanja kwa kufuata maelekezo na anaelewana vizuri na wenzake,” alisema Mgunda na kuongeza;
“Sifa nyingine ya kipekee kwa Mzamiru anaweza kukaba na kuchezesha pia ana pumzi na nguvu kubwa na nilivyofika nilimwambia anahitaji kuonyesha alichonacho na kucheza kwa kujiamini zaidi ndio maana kwa sasa unamuona kwenye ubora huo.”
Mzamiru amekuwa akicheza kama kiungo namba nane na amepangwa na Sadio Kanoute katika eneo la kati na muunganiko wao umeonekana kuwa bora zaidi na kuziunganisha vyema safu za ulinzi, kiungo na ushambuliaji za Simba. Hadi sasa Mzamiru yupo kwenye orodha ya mastaa watano wa juu wanaoongoza kwa kutoa pasi za mabao ‘Asisti’, akiwa nazo tano nyuma ya Clatous.