Moja ya mtambo wa kazi kwenye eneo la ukabaji kwenye kikosi cha Simba ni huyu jamaa anaitwa Mzamiru Yassin, kiungo mpole ukimuona lakini ana balaa uwanjani kwa namna anavyowadhibiti wapinzani huku anavuja jasho.
Mechi 22 za ligi amecheza akitumia dakika 1,686 katupia mabao mawili yote akiwa ndani ya 18 huku moja akitumia mguu wa kulia na moja kwa mguu wa kushoto.
Kiungo huyu alikuwa mhimili mkubwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kilichoivaa Uganda nyumbani na ugenini, kwote alipiga kazi ya maana.
Balaa lake kalinukisha namna hii hapa Championi Ijumaa tunakudondoshea baadhi namna hii. Takwimu zake ni za ligi kuu pekee.
MIKATO NA KADI
Ukatili wake ni kwenye mpira namna anavyopambana kutimiza majukumu yake jambo linalomfanya kuwa tofauti awapo ndani ya uwanja.
Mikato hiyo imekuwa ikimgharimu na wakati mwingine amekuwa akionyeshwa kadi za njano, hadi sasa amepata kadi nyingi kwenye mechi tofauti.
Miongoni mwa mechi ambazo alionyeshwa kadi ya njano ilikuwa dakika ya 90 dhidi ya Tanzania Prisons Uwanja wa Sokoine Septemba 14 mwamuzi alikuwa ni Ahmed Arajiga.
Mchezo mwingine ilikuwa dhidi ya Dodoma Jiji uliochezwa Uwanja wa Mkapa Oktoba 2, 2022 alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 86 na mwamuzi alikuwa Ramadhan Kayoko.
Kariakoo Dabi iliyochezwa Uwanja wa Mkapa ubao uliposoma Yanga 1-1 Simba hakuachwa salama na Ramadhan Kayoko alimuonyesha kadi ya njano dakika ya 26 baada ya kumchezea faulo Jesus Moloko.
Omary Mdoe kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba KMC 1-3 Simba ilikuwa Desemba 26 alimuonyesha kadi ya njano dakika ya 57.
Kitabu cha mwamuzi Ester Albert Januari 18 Uwanja wa Mkapa, Simba 3-2 Mbeya City kina kumbukumbu ya Mzamiru alipoonyeshwa kadi ya njano dakika ya 56.
Alipoibukia Manungu, Machi 11, 2023 alionyeshwa pia kadi ya njano dakika ya 77.
Simba ikiwa ni imara kwenye kutupia ni 58 kibindoni wamefunga kwenye mechi 24 Mzamiru kahusika kwenye mabao 7 akiwa ametupia mabao mawili na asisti tano kibindoni.
HIZI ALIZITUNGUA
Alianza kwa kuwatungua Mtibwa Sugar dakika ya 38 Uwanja wa Mkapa ilikuwa Oktoba 30, mwaka jana. Mbeya City nao aliwachapa pale Uwanja wa Sokoine dakika ya 14, Novemba 18 hapo akagotea kwenye ukurasa wa kufunga.
MIPANGO ALITENGENEZA HAPA
Asisti ya kwanza alitoa kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Dimba la Mkapa. Pasi nyingine alitoa mbele ya Ruvu Shooting Uwanja wa Mkapa ambapo ilikuwa ni Novemba 19.
Dhidi ya Geita Gold alitoa pasi moja ilikuwa dakika ya 40 Uwanja wa Kirumba, Mwanza. Aidha alitoa pasi mbili kwenye mchezo dhidi ya Tanzania Prisons ilikuwa dakika ya 64 na 69.
CHAGUO LA KWANZA
Mzamiru kwenye eneo la kiungo ndani ya Simba ni chaguo la kwanza akiwa na uhakika wa kuanza na kuzima mwanzo mwisho.
Iwe ni kwenye mechi za kitaifa na kimataifa yupo imara katika kutimiza majukumu yake.
TAIFA LINAMTAZAMA KIJANA
Mzamiru kwenye timu ya Taifa ya Tanzania anatazamwa na makocha kwenye eneo la ukabaji pamoja na Watanzania namna anavyotimiza majukumu yake.
Kwenye mchezo wa ugeni kuwania kufuzu Afcon alizima kama kawa mbele ya Uganda na ule wa pili uliochezwa Uwanja wa Mkapa pia alianza kikosi cha kwanza.
MRITHI WAKE PASUA KICHWA
Bado mrithi wake ni pasua kichwa kwa upande wa wazawa kutokana na aina ya uchezaji wake kuonekana kuwa tofauti jambo linalopasua kichwa sio ndani ya Simba pekee hata timu ya taifa pale tu atakapoamua kutundika daruga.