Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwisho wa tambo ni leo Kwa Mkapa

MUDATHIRI FEI TOTO Mwisho wa tambo ni leo Kwa Mkapa

Sun, 17 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kuanzia saa 2:30 usiku wa leo, pale kwa Mkapa kutakuwa na vita ya kusaka pointi tatu itakayowakutanisha wanaume 22 wa timu za Azam FC na Yanga katika pambano la Ligi Kuu Bara.

Pambano hilo la 32 kwa timu hizo katika ligi hiyo tangu Azam ilipopanda daraja msimu wa 2008-2009 ni la kumaliza tambo na majigambo baina ya mashabiki wa klabu hiyo na pia zitatoa picha halisi ya mbio za ubingwa kwa msimu huu.

Yanga inaongoza msimamo ikiwa na pointi 52 baada ya mechi 19, ikifuatiwa na Simba iliyopata ushindi wa mabao 2-0 juzi mbele ya Mashujaa inafuata ikiwa na alama 45, huku Azam ikifuatia nafasi ya tatu ikiwa na 44, japo ina mchezo mmoja mbele tofauti na vigogo hivyo.

Ushindi kwa Yanga itaifanya iende mapumziko ikiwa na pointi 55 kupitia mechi 20, huku Azam ikisalia nafasi ya tatu na alama zao, lakini matokeo yakiwa kinyume ina maana Azam itarejea nafasi ya pili ikifikisha pointi 47, huku Simba ikirudia nafasi ya tatu ikiwa na mechi moja mkononi.

Mchezo wa leo unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka ili kutaka kuona kama Azam itavuta unyonge iliyonayo mbele ya Yanga, kwani katika mechi sita zilizopita, imeshinda mara moja tu April 25, 2021, huku ikifungwa mara nne na mara moja kutoka sare, lakini kwa ujumla Wanalambalamba wamekuwa wakiburuzwa na Wananchi.

Katika mechi 31 zilizopita Azam imeshinda mara tisa na kupoteza 13, huku tisa ikitoka sare na Yanga iliyofunga jumla ya mabao 41 dhidi ya 37 za Matajiri hao wa Chamazi inayojivunia kuwa na nyota kama Feisal Salum, Kipre Junior, Idd Seleman ‘Nado’ na Gjibril Sillah waliyoichachya Yanga katika mechi ya kwanza licha ya kupoteza 3-2 ikiwa ugenini.

Ikicheza kama wenyeji wa mchezo Azam itakuwa na kazi ya kuwachunga nyota wa Yanga wenye uchu ya mabao akiwamo kinara wa Wafungaji wa Ligi, Stephane Aziz KI mwenye mabao 13, Maxi Nzengeli mwenye tisa na Mudathir Yahya aliyefunga manane mbali na Pacome Zouzoua na Kennedy Musonda.

Kocha wa Azam, Youssouf Dabo alisema benchi la ufundi limefanya kazi kwa usahihi kilichobaki ni wachezaji kufanya yao huku akiwatakiwa wasirudie makosa ya mechi iliyopita waliolala 3-2.

“Tunahitaji pointi tatu, sio rahisi ila tumejiandaa tuwe imara kuhakikisha tunashinda kurudi katika mbio za ubingwa,” alisema Dabo na kuongeza;

“Yanga ni timu nzuri ina wachezaji bora tutawaheshimu, ila hatutowaogopa, kwani tumejiandaa kwa ushindani wa mechi zetu zote na dakika 90 zitaamua nani bora.”

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema utakuwa mchezo mzuri wa kuutazama kutokana na timu zote kuwa na bora na Azam imeimarika tofauti na duru la kwanza.

‘’Tumetoka kucheza mechi ngumu mfululizo, wachezaji wana uchovu, ila hilo halitawazuia kupambana,” alisema Gamondi na kuongeza;

‘’Wapo tayari kwa mchezo tunahitaji ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kutetea taji, natarajia mabadiliko ya kikosi baada ya baadhi kuwapumzisha mchezo uliopita.

Mara baada ya mechi hiyo, ligi itasimama hadi Aprili 12 ili kupisha michezo ya kimataifa kwa timu za taifa kwa mujibu wa kalenda ya Fifa, kwa nyota wa timu hizo watakapoungana na timu za taifa ikiwamo Taifa Stars inayoenda Azerbaijan.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: