Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwijaku, Baba Levo wapewe Taifa Stars

WhatsApp Image 2022 06 21 At 12.jpeg Mwijaku, Baba Levo wapewe Taifa Stars

Thu, 11 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Hakuna kundi gumu duniani kama watu wa soka. Kuna wanaojiona wao ndiyo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wanamiliki Taifa Stars. Hawa kwa pamoja wanajiita watu wa soka. Simba kuna wanaojiona ni kama wana hatimiliki ya klabu na Yanga kuna wanaoamini wao ndiyo Yanga zaidi kuliko wengine. Hawa ndiyo watu wa soka.

Huwa hawataki mtu mwingine yeyote awasogelee wala kuona sura mpya zikiingia kwenye mzunguko. Hivi karibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro alitangaza wajumbe wa Kamati ya Hamasa ya timu za Taifa. Kazi ya kamati ni kuhamasisha Watanzania kupenda timu na kuzichangia. Haya ndiyo malengo makuu. Hakuna lingine lolote na ni kazi isiyokuwa na malipo.

Oscar Oscar ambaye ndiye mwandishi wa makala haya ni miongoni mwa wajumbe wa kamati, lakini gumzo kubwa ni majina ya Mwijaku na Baba Levo ambao wanaonekana sio watu wa soka. Ni ‘chawa’ tu.

Kutajwa kwenye jambo linalohusu soka kumekuwa na maoni tofauti na wengi wakiamini hawakustahili kujumuishwa. Hapa watu wa soka huwa wanajiona ni kama wao ndiyo wamiliki wa timu ya Taifa na kusahau hii mali ya kila mtu. Kila mtu ana haki sawa na hasa inapohitaji msaada.

Mambo ya Kamati za Hamasa yako duniani kote sema kwa mitindo tofauti. Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) hutumia zaidi wachezaji nguli wa zamani kuleta hamasa kwenye michuano iliyo chini Fifa. Ndiyo maana watu kama David Beckham huwezi kuwakosa kwenye Kombe la Dunia. Shirikisho la Soka Afrika hutumia zaidi wachezaji wa zamani kina Didier Drogba, John Obi Mikel, Samuel Eto’o na wengine.

Hali ni tofauti kidogo na hapa kwetu. Bahati mbaya malejendari wetu wengi hawana ushawishi kwa jamii. Wengi hawana nguvu nje ya kile walichofanya uwanjani enzi zao. Ni vigumu kuwatumia malejendari kuleta hamasa. Sio kwa kuwakosea heshima, lakini sehemu yao kubwa hata kujieleza tu kwenye vyombo vya habari ni changamoto.

Uwezo wa kushawishi kampuni kuwekeza wengi hawana. Tunawaheshimu kwa kile walichofanya uwanjani, lakini nje ya hapo wengi hawana ushawishi.

Tazama vyombo vya habari vya wenzetu wachambuzi wengi na watangazaji wa soka ni wachezaji wa zamani. Hapa kwetu hali ni tofauti, wengi hawawezi hata kuuelezea vizuri mpira walioucheza kwa mafanikio.

Tulihitaji kuwa na watu kama Ally Mayay na Amri Kiemba wengi hapa nchini. Hakuna ubishi soka likichambuliwa na aliyelicheza linaleta maana, lakini hatuna watu wengi wenye uwezo.

Kwa ambao hawakucheza wala kufundisha soka ndiyo wana maarifa zaidi kuliko waliocheza. Usishangae Baba Levo akawa na uwezo mkubwa wa kuelezea soka kuliko lejendari mkubwa wa soka nchini. Usishangae Mwijaku akawa na uwezo mkubwa wa kuwaleta Watanzania uwanjani kuliko lejendari wetu.

Kuna mahali soka letu linapita kwenye njia zake. Tukitaka kila kitu kiwe kama Ulaya, hatutoboi. Hatuna watu hao. Taratibu tunaweza kuja kuanza kubadilika lakini kwa wakongwe wetu wengi hawana tena ushawishi mbele ya jamiii.

Wanachofanya Mwijaku na Baba Levo ni kama sanaa. Ni watu na akili zao, lakini wameamua kutumia mtindo wa ‘upambe’ kufikisha ujumbe kwa jamii.

Hawa watu wana ushawishi mkubwa kwa kampuni na wafanyabiashara kuliko staa yetote wa soka nchini. Kama matajiri wanawatumia kuleta hamasa ya biashara, kuna dhambi gani Serikali ikiwatumia kuleta watu uwanjani? Kuna tatizo gani Serikali ikiwatumia kushawishi wafanyabiashara kuchangia timu zetu za Taifa?

Binafsi sioni tatizo lolote. Hawa watu wana wafuasi wengi sana kwenye mitandao ya kijamii kuliko mkongwe yeyote wa soka nchini. Wanaweza kuingia popote na kuwafikia watu. Sioni tatizo lolote kutumiwa Taifa Stars. Kuna kazi ya hamasa inafanywa na Bongozozo wengi wetu hatuiwezi. Watu wa soka wanatakiwa kupunguza chuki. Wanatakiwa kujua Taifa Stars sio mali ya mtu binafsi. Kila Mtanzania ana haki sawa kwenye timu zetu. Tujifunze kupokea mabadiliko. Tukubali watu wenye uwezo mkubwa wapewe nafasi na wao kutoa mchango.

Idadi kubwa ya Watanzania karibu nusu ni vijana. Ni miaka 18 kushuka chini kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi. Hawa ni vijana wa kidijitali. Huwezi kuwashawishi kuzipenda timu za Taifa kwa mfumo wa analojia. Huwezi. Wanahitajika watu wa kizazi kipya kwenda sawa na kasi yao.

Baba Levo na Mwijaku kama wangekuwa wanasafiri na timu kila mahali kila Mtanzania angekuwa anafuatilia ilipo na kujua nini kinaendelea kuihusu. Hawa watu hawagusi chochote kuhusu ufundi. Kazi yao ni kuwafanya Watanzania waijue timu na kuichangia. Kila Mtanzania akitoa Sh1,000 tutavuna pesa nyingi za kusaidia timu zetu za soka, riadha, ndondi na kadhalika.

Sioni kosa lolote la watu hawa kuwekwa kwenye kamati. Kosa lingekuwa wangekuwa wamewekwa kwenye kamati ya ufundi. Zipo baadhi ya kamati ambazo zinataka sifa za kitaaluma. Mfano kamati ya ufundi na kamati ya fedha na mipango.

Huku kwenye hamasa wanahitajika watu wenye ushawishi kwa jamiii. Hakuna kosa kuwatumia Baba Levo na Mwijaku huku. Hawa watu wanafuatiliwa kutokana na sanaa wanayoitumia kufikisha ujumbe kwa jamii.

Sio lazima kila kinachofanyika Ulaya kifanyike Tanzania. Sisi kuna muda tunahitaji dunia kufikia malengo yetu. Hata kule Misri ilikokuwa timu yetu kabla ya kwenda Ivory Coast kama kungekuwa na Mwijaku na Baba Levo karibu kila Mtanzania angekuwa na taarifa. Tusiwakatae hawa watu wana nguvu kwa jamii. Mpira wetu bado unajipapatua. Kila mwenye uwezo wa kuchangia chochote hasa nje ya uwanja apewa nafasi.

Ukiniuliza mimi dunia inabadilika lakini timu yetu ya Taifa bado haijapata mtu kuisemea sawasawa. Kazi wanazofanya watu wa habari wa Simba na Yanga zinahitajika pia kufanywa pale kwenye timu ya Taifa. Kuna kazi kubwa inafanywa na ofisa habari wa TFF, lakini nadhani anapaswa kuongezewa nguvu na kutengenezewa wasaidizi wengi wenye nguvu kidijitali. Watu kama Baba Levo na Mwijaku, huku nje wanaweza kusaidia kuvutia watu kuipenda timu. Taaluma ifanywe na wanataaluma. Hamasa ifanywe na watu wenye nguvu ya kuhamasisha. Mwijaku na Baba Levo tukiacha chuki watatusaidia kwenye kuleta hamasa katika timu zetu za Taifa.

Chanzo: Mwanaspoti