Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwenye bahati na bahati yake

Fdxghy Mwenye bahati na bahati yake

Thu, 13 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Erik ten Hag anabaki Manchester United baada ya klabu hiyo ya Old Trafford kusitisha mpango wa kusaka kocha mpya.

Miamba hiyo ya Ligi Kuu England sasa imeamua kubaki na Mdachi huyo na tayari mazungumzo ya mkataba mpya yameanza licha ya jitihada kadhaa za kutafuta makocha wapya wakati msimu ulipomalizika.

Mabosi wa Man United walikuwa wanafanya mchakato wa kuleta kocha mpya baada ya timu hiyo kumaliza katika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, lakini sasa kinachoelezwa ni kwamba ushindi kwenye fainali ya Kombe la FA dhidi ya mahasimu wao Manchester City ilikuwa kete ya turufu kwa Ten Hag na kufanikiwa kubaki kwenye ajira yake huko Old Trafford.

Mmiliki wa klabu ya Man United, bilionea Sir Jim Ratcliffe amebadili mawazo na kuamua kuendelea kubaki na Ten Hag akiamini atafanya jambo.

Kocha huyo wa zamani wa Ajax, Ten Hag alipewa dole gumba kwamba anabaki Old Trafford baada ya wiki mbili za kufanya tathmini ya msimu ulivyokuwa. Ndani ya muda huo, Man United ilizungumza na makocha wengine kwa ajili ya kwenda kuwapa kazi hiyo.

Tajiri Ratcliffe alikutana na kocha Thomas Tuchel wikiendi iliyopita, lakini bosi huyo wa zamani wa Bayern Munich alikataa ofa ya kwenda kuinoa Man United, akidai kwamba anahitaji siku kadhaa za kujiweka mbali na presha za soka, anataka kupumzika.

Na sasa, Man United imethibitisha Ten Hag, ambaye amebakisha miezi 12 kwenye mkataba wake, ataendelea kuinoa timu hiyo kwa msimu mwingine.

Ten Hag, 54, ajira yake ilikuwa kwenye shaka kubwa baada ya kikosi hicho kumaliza ligi kwenye namba nane, nafasi ya hovyo zaidi kuwahi kushika kwenye Ligi Kuu England na hivyo kukosa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Lakini, Mdachi huyo aliongoza Man United kushinda taji la Kombe la FA kwa ushindi wao mbele ya Man City uwanjani Wembley, mwezi uliopita.

Licha ya kushinda taji la pili katika msimu wa pili katika miaka yake miwili klabuni Man United, Ten Hag, alisema “nakwenda kubeba mataji kwingineko” alikuwa akisubiri hatima yake juu ya usalama wa ajira ya kwenye kikosi hicho.

Makocha waliokuwa kwenye rada za Man United kwenye mchakato huo ni pamoja na Tuchel, Gareth Southgate, Mauricio Pochettino, Graham Potter, Kieran McKenna, Roberto De Zerbi na Thomas Frank.

Lakini, kampuni ya bilionea Ratcliffe, Ineos ambayo ndiyo inayomiliki hisa kwenye klabu hiyo ya Man United imemaliza utata na kufichua Ten Hag ndiye mtu sahihi kwao hivyo ataendelea na majukumu yake ya kukinoa kikosi hicho. Na kocha, Ten Hag, ambaye juzi alipigwa picha akiwa na mkewe kwenye likizo yake huko Ibiza, alifanya mazungumzo ya namna ya kuifuma upya Man United na mabosi wake Jumanne iliyopita.

Na taarifa zaidi zinadai kwamba kocha huyo atakutana tena na mabosi wake ili kupanga namna kikosi cha timu hiyo kitakavyokuwa msimu ujao.

Tajiri Ratcliffe ameshafanya mabadiliko kwenye mabosi wa ngazi za juu ambapo Omar Berrarda ataanza kazi mwezi ujao, sambamba na mkurugenzi wa soka. Dan Ashworth, ambaye atatua Old Trafford akitokea Newcastle United.

Mkurugenzi wa ufundi, Jason Wilcox tayari yupo kabisa akifanya kazi na Ratcliffe, Sir David Brailsford na Jean Claude Blanc.

Taarifa za Ten Hag kubaki zitapokewa kwa shangwe na mashabiki wa timu hiyo wanaoamini msimu uliopita kufanya kwao vibaya kulichangiwa na kikosi chao kuandamwa na majeruhi wengi. Kocha huyo alishinda Kombe la Ligi kwenye msimu wake wa kwanza alipowachana Newcastle kwenye mechi ya fainali kabla ya msimu wake wa pili kushinda Kombe la FA kwa kuwachapa Man City.

Mashabiki wa United wanaamini Ten Hag anarekodi nzuri za misimu yake ya kwanza kwenye kikosi cha United, ukilinganisha na Mikel Arteta kwenye misimu yake miwili ya kwanza huko Arsenal na bado alivumiliwa kabla ya sasa kufanya vyema Emirates.

Chanzo: Mwanaspoti