Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwenye Simba yake kasema...Tunataka sura mpya Try Again apata mtetezi

Try Again 01 Mwenye Simba yake kasema...Tunataka sura mpya Try Again apata mtetezi

Sun, 9 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Saa chache tangu kuwepo kwa taarifa za kujiuzulu kwa baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba, huku ikielezwa huo ni mwanzo wa kuisafisha klabu hiyo ili iingie msimu mpya wa mashindano ikiwa kivingine, mmoja ya wazee wa klabu hiyo, Hamis Kilomoni ameamua kuvunja ukimya na kutoa neno.

Kilomoni ambaye ni kama mwenye Simba yake kutokana na kuwa miongoni mwa walioiasisi muda mrefu alikuwa kimya, lakini ghafla jana mara baada ya kuenea kwa taarifa ya baadhi ya viongozi wa Simba kujiuzulu, aliamua kufunguka kwa kueleza kwa hali ilivyo Msimbazi, sasa inahitaji sura mpya kabisa.

Mwenyekiti huyo wa zamani wa Baraza la Wadhamini wa klabu hiyo, alisema ili Simba iwe na mabadiliko ya kweli lazima watakaowekwa kuongoza wawe na uchungu na timu na sio kibiashara, pia akisema hata kwa kikosi cha timu nacho kinahitaji kujengwa vyema zaidi ili kuzima ufalme uliopo sasa wa Yanga.

Kilomoni ameyasema hayo jana ikiwa ni saa chache zimepita baada ya Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi upande wa mwekezaji, Mohamed ‘Mo’ Dewji kujiuzulu nafasi zao.

Kuachia ngazi kwa wajumbe hao kumeelezwa kumekuja baada ya Mo Dewji kuwaomba kufanya hivyo, huku ikielezwa ni moja ya mikakati ya kupanga upya safu ya uongozi kwa lengo la kurejesha heshima ya Simba iliyopotea misimu mitatu mfululizo iliyopita huku Yanga ikitawala.

Akizungumza na Mwanaspoti mapema jana, Mzee Kilomoni alisema; “Watu ambao sasa hivi wanaitaka Simba ndio haohao waliokuwa pembeni kipindi tunaijenga klabu, wameona hivi sasa ipo vizuri kila mtu anaitaka. Nasema hivi, ili Simba irudi katika mstari kama zamani basi ikabidhiwe kwa watu sahihi wenye uchungu na klabu na sio kuwaweka watu ambao wapo kibiashara zaidi.”

“Kujiuzulu kwa hao watu haitasaidia kama watakuja wengine wenye mrengo ule ule, Simba inahitaji sura na watu wapya kuirejeshea heshima yake. Kama nilivyosema kinachotakiwa kufanyika ni kuwaweka watu wenye uchungu na timu na si vinginevyo,” aliongeza Mzee Kilomoni.

Kuhusu timu kwa jumla, alisema inahitaji pia kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa watakaomudu vishindo vya timu pinzani iwe kwa michuano ya ndani au ile ya kimataifa ambayo Msimbazi imekuwa na rekodi tamu ikiwemo ya kuwa klabu pekee Tanzania kufika nusu fainali ya Klabu Bingwa (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika), pia kuwa ya kwanza kucheza fainali ya Kombe la CAF (michuano iliyokuja kuunganishwa na Kombe la Washindi na kuwa Shirikisho Afrika la sasa.

Watani wa Simba, vijana wa Jangwani msimu uliopita iliifikia rekodi hiyo ya kucheza fainali ya michuano hiyo ya Shirikisho Afrika, ikiwa klabu ya kwanza kufanya hivyo tangu michuano hiyo ilipobadilishwa mwaka 2004.

Simba pia imekuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kucheza hatua ya robo fainali ya michuano ya CAF kwa mara tano mfululizo kati ya misimu sita ikiwamo msimu huu ilipofika hatua hiyo kama iliyoishia Yanga pia.

Hata hivyo, Simba kwa misimu mitatu mfululizo sasa haijatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara wala Kombe la Shirikisho iliyiotawaliwa na Yanga na inaelezwa hilo limemfanya Rais wa Heshima wa klabu hiyo, Mo Dewji kuingia mstari wa mbele kuweka mambo sawa klabuni ikiwemo kulazimisha wajumbe aliowateua kujiuzulu.

Wajumbe walioteuliwa na Mo ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Salum Abdallah ‘Try Again’, Hamza Johari, Dk. Raphael Chageni, Zulfikar Chandoo na Rashid Shangazi wanaodaiwa wameshajiuzulu, huku ikielezwa bilionea huyo amekomalia pia ishu za usajili akisimamia mwenyewe kwa asilimia zote kuijenga Simba mpya.

Kabla ya sekeseke la sasa na kuyumba kwa Simba, timu hiyo ilitawala kwa misimu minne Ligi Kuu Bara ikitwaa mataji tangu msimu wa 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021, ndipo Yanga ikapindua meza misimu mitatu mfululizo iliyopita, jambo lililowachefua wanachama na mashabiki wa klabu hiyo.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: