Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwamuzi wa kwanza mwanamke nchini

MWAMUZI Mwamuzi wa kwanza mwanamke nchini

Fri, 22 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ni mwendo wa saa 14 kutoka jijini Dar es Salaam hadi Mbeya na ni kwa kutumia usafiri wa barabara ambapo ni kilometa 822.2.

Ilikuwa ni safari ya kumfuata mwamuzi wa kwanza mwanamke kwenye soka la Tanzania na Afrika Mashariki na Kati, Elizabeth Kalinga.

Elizabeth anaishi jijini Mbeya na ndiko makazi yake tangu hapo awali na hata alipokuwa anajishughulisha na soka bado aliishi huko ingawaje Dar es Salaam ndipo kulikuwepo na shughuli nyingi za soka kwa ujumla.

Mwanaspoti lilifunga safari hadi jijini Mbeya na kufanya naye mahojiano maalumu ambapo alizungumzia mambo mbalimbali katika maisha yake.

Elizabeth naweza kusema ni mwanamke wa shoka, amekutana na misukosuko mingi ndani na nje ya soka lakini alikabiliana nayo hadi sasa yupo imara. Anaanza kusimulia namna alivyoanza kujishughulisha na kazi hiyo ya uamuzi ambayo awali ilionekana mwanamke kuchezesha soka ni uhuni.

“Kwanza kabla ya yote napenda kusema mimi ndiye niliyeifufua Mbeya City ambayo mwanzo kabisa iliitwa Hamambi ilikuwa timu ya Jiji la Mbeya.

“Niliandika dokezo la kwanza la kuifufua timu hiyo na nilipoandika ilikuwa halijafanyiwa kazi ndipo akaja Emmanuel Kimbe ambaye ni mtendaji mkuu wa timu hiyo akapita nalo na kuitengeneza Mbeya City hii na wakati huo ndio alikuwa anafikafika kazini maana alinikuta.

“Nikiandika kitu kinatiki, hivyo nashukuru Mungu mawazo yangu yanakubalika mahala popote pale,” anasema Elizabeth.

MIAKA 22 YA UAMUZI

“Ni kweli nimekuwa mwamuzi wa kwanza wa kike Tanzania, nilianza kazi hii mwaka 1980 nikiwa Lusaka, Zambia ambako niliishi na binamu yangu ingawaje wazazi wangu pia waliishi huko. Na nilistaafu mwaka 2002 hivyo nimeifanya kazi hiyo kwa miaka 22.

“Kwanza nilikuwa mchezaji wa mpira wa netiboli na kikapu, waamuzi waliokuwa wakituchezesha ni wa kiume, sikupenda kitendo cha kuchezeshwa na wanaume, akili yangu ilihisi wanatuchungulia tunavyoruka na visketi vyetu vifupi.

“Kile kitendo kiliniudhi sana, nikasema ni lazima na niwe mwamuzi ili niwachezeshe wao kama wanavyotuchezesha sisi,” anasema na kuongeza;

“Nilimfuata mtu mmoja aliitwa Mr Phiri wakati huo alikuwa mwamuzi, nikamweleza kusudio langu na kunikaribisha kwenye darasa la mafunzo ya uamuzi, nilienda pia mazoezini kwenye Chuo cha Evarine Collage kilichopo Lusaka wakati huo sikuzidi umri wa miaka 23.

“Darasa zima tulikuwa wanawake watatu, mimi, Marry na Anna hiyo ni kati ya 1981-1982. Nilipanda daraja hadi daraja la pili, 1985 nilirudi nyumbani, baba hakustaafu ila mimi nilirudi, nilijua mawazo yangu ya uamuzi yameishia kulekule Lusaka, maana nilikuwa sijui wapi naanzia hapa nchini ikumbukwe nilisoma mambo ya Ustawi wa Jamii.

“Nakumbuka kuna siku nikiwa kwenye mihangaiko yangu hapa mjini niliwakuta watu wanabishana kijiweni juu ya sheria za soka, nilisimama kuwasikiliza na wote walichokuwa wanabishana walikosea.

“Hivyo nikasogea na kuwasaidia kuwapa ufafanuzi, sasa kumbe kwenye hicho kijiwe alikuwepo mwenyekiti wa chama cha soka Mkoa wa Mbeya, alishangaa sana na hapo ndipo aliponikaribisha kwenye kikao cha chama, ukawa mwanzo wangu wa kutimiza ndoto, maana nilijua ndio imekufa.

“Mwenyekiti ndiye aliyenisogeza kwenye soka la Tanzania, nikaenda kwenye hicho kikao Uwanja wa Sokoine, nilitambulishwa na kuanza kualikwa kwenye vikao mbalimbali.

“Kipindi hicho nilikuwa najifunza mambo ya urefarii, nilikuwa nacheza kikapu, maana napenda mambo yanayotumia nguvu, niliichezea Timu ya Flames ya hapa Mbeya chini ya Kocha Boliva na baadaye akaja John Bandiye.

“Ukiniangalia mwilini nina makova ya mchezo wa kikapu, maana uwanja wetu ulikuwa mbovu sana. Tulikuwa na timu mbili ya wanawake na wanaume ila sikutaka kucheza ya wanawake nilicheza ya wanaume,” anasema na kuongeza;

“Sikutaka kucheza na wanawake maana ni watu wanaolalamika sana hata wakigongana kidogo ni kelele, nilipenda tuburuzane, tukisafiri ilikuwa lazima waombe kuwa tuna mtoto wa kike, Mbeya Flames imetoka mbali na tumeipambani sana, wanaocheza hiyo timu kwasasa watambue hilo, tulipambana na Pazi kwenye mchezo huo.

“Nina miaka 66 nautafuta wa 67, namshukuru Mungu kunipa umri huu na bado nipo imara, wengi wanauliza ninafanya nini hadi nipo imara hivi, ila nina shughuli zangu ngumu, ukakamavu sijaanza leo.

“Nilikuwa nikitoka kwenye kikapu nahamia mazoezi ya Tukuyu Stars walikuwa wanakuja kufanya hapa Sokoine, maana uwanja mdogo nilikuwa sijisikii kama nimefanya mazoezi ya kutosha.”

FRAT/TFF WAMKATAA

Anasema uongozi wa Mkoa wa Mbeya, ulitoa taarifa Chama cha Waamuzi Tanzania (FRAT) na Shirikisho la Soka Tanzania (FAT sasa TFF) kuwa kuna mwamuzi wa kike, ila hawakumkubali.

“Mkoa walinipokea nao walitoa taarifa kwenye chama cha taifa kuwa kuna mwamuzi wa daraja la pili, kipindi hicho Mzee El Maamry alikuwa anamaliza muda wake anaingia Ndolanga, walinikataa kuwa hawajawahi kuona mwanamke mwamuzi hadi wanipe mafunzo.

“Walinirudisha daraja hadi daraja 3P hilo halikunipa shida, kikubwa wanitambue nikasema nitawaonyesha jambo. Ila nikawa napewa mechi ngumu ambazo wanaona wengine hawazimudu, iwe imevunjika ama mwamuzi kupigwa ndo walinipa mimi.

“Nilipewa kwasababu hata ubabe ulikuwemo maana kule Lusaka nilijifunza hata mambo ya karate na judo, nilijua kuwa kwenye soka wanapiga hivyo nilijilinda mapema. Wengi wananifahamu vizuri maana ilikuwa ukinisogelea tu vibaya inakula kwako maana hata kupiga nilikuwa napiga, anasema

“Niliwahi kupewa onyo la kutorudia kufanya vitendo vile, ila sina rekodi ya kuharibu mchezo hata mmoja, kama nitakuwa nimesahau nikumbushwe.”

KARIAKOO DABI

Hadi anastaafu hakuwahi kuchezea Kariakoo Dabi (Simba na Yanga) yeye anasimulia;

“Niliwahi kupangiwa dabi moja 1988 Simba ilitaka kushuka daraja, ilikuwa mkiani ambapo wangepoteza wangeshuka, nilipangwa kabisa ratiba wakati huo ilikuwa inapangwa mapema , nilienda hadi Dar es Salaam, Simba walibembeleza sana TFF wakati huo FAT ili nisichezeshe mechi hiyo, maana walijua sitawabeba.

“Nilivyofika walinibadilishia mtu wakanituma niende Shinyanga nikachezesha Taifa Cup, ni mechi ambayo Yanga waliionea huruma Simba na kweli wangeshuka maana uwezo wao ulikuwa mdogo na mimi kwa vile ni mnyoofu ningefuata sheria uwanjani na nisingepindisha.

“Hivyo Yanga waliona mpira bila Simba hautanoga kwenye ligi na walifanya vizuri. Wangeshuka Simba na mimi ningeshuka hawakuwa vizuri kabisa kufungwa ilikuwa lazima, Yanga walikuwa bora sana.”

“Hivyo katika maisha yangu dabi pekee niliyopangwa kuchezesha ni hiyo ila mechi za Simba na timu nyingine ama Yanga na nyingine nimechezesha sana.”

NI YANGA DAM’DAMU

Hakusita kuficha mapenzi yake juu ya timu anayoipenda;

“Kiukweli kiasili naipenda Yanga lakini nikiwa uwanjani nasimamia sheria na kanuni na misinngi yangu ili nisiharibu sifa yangu na kumuonea mtu, mwenye haki apewe haki yake.

“Yanga nao walikuwa wananifahamu vizuri kuwa sitaki utani kwenye kazi yangu, Yanga waliwahi kucheza na Tukuyu Stars hapa Sokoine halafu kuna mtu akamwibia kadi mwamuzi, mimi nilikuwa mezani, nilisimama na kumwita refarii kumwambia.

“Nilimwambia mtu fulani kaiba kadi na hapo walikuwa wamemlamba kweli mitama Mr Sanga wa Dodoma, ndo hapo walijua sio mwenzao maana sehemu yoyote ambayo mwenzako amewekeza nguvu na pesa yake hutakiwi kuharibu, pia umesomea hiyo kazi kwanini ujiharibie, unapaswa kutenda haki na umeaminika.

“Niliona wanavyoiba kadi, niliona wanavyompiga nisingeweza kunyamaza, chochote kinachokwenda kinyume napaswa kukitambua na kukitolea maamuzi. Mwamuzi wa pembeni hakutoa ushirikiano ndo maana niliingilia kati.”

MISUKOSUKO MARA TATU

“Nilijaribu kupungukiwa na ujasiri mara tatu, moja baada ya mchezo kumalizika, tukio hili nililifanya Uwanja wa Sokoine 1993, kuna timu iliitwa Red Angles ya hapa Mbeya, ilikuwa haimalizi mchezo bila kumpiga mwamuzi, washinde wasishinde.

Huo mchezo mwamuzi alikuwa anaitwa Nchimbi mara ya mwisho ndo alichezesha, mchezo haukumalizika, walikaa wakaniteua, waliniamini nitamaliza mchezo, walifungwa.

“Nilipokuwa natoka tu, nikasikia wanasema amechezesha vizuri, sasa ndio tumuache huku nawasikia vizuri tu, sikugeuka na nilijifanya sijasikia ila nikawa nawasoma mwelekeo wao.

Chanzo: Mwanaspoti