Baada ya malalamiko mengi ya waamuzi wanaochezesha michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024, Kamati ya Waamuzi Zanzibar michuano hiyo imetoa tamko huku ikitangaza maamuzi mazito kwa kula vichwa vya waamuzi wawili.
Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi Zanzibar, Waziri Shekha amesema wanafahamu kuna malalamiko ya waamuzi wanaochezesha mashindano hayo.
Shekha alisema katika tathmini yao wamegundua kwamba wapo waamuzi wanaofanya makosa, lakini wapo wengine wanaolaumiwa kimakosa kwa sababu wadau kukosa ufahamu wa sheria za soka.
Shekha aliweka wazi kuwa kamati yao imemfungia mwamuzi wa kwanza msaidizi Yusuf Shombe Issa kwa kushindwa kutafsiri vizuri sheria kwa kuruhusu bao la kwanza la Azam na baadaye Singida Fountain Gate ambayo hayakuwa halali kwenye mchezo wa robo fainali.
Mbali na Issa, pia Shekha ameweka wazi mwamuzi wa pili waliyemfungia ni Mohamed Mwadini aliyekuwa mwamuzi wa kwanza msaidizi kwa hatua ya kuruhusu bao katika mchezo wa makundi kati ya JKU na APR akidai mpira ulivuka mstari wa goli wakati haikuwa hivyo.
"Hao waamuzi tumeona kabisa walishindwa kufanya kazi yao sawasawa kama hilo bao la Azam lilikuwa wazi kabisa kwamba mfungaji ameotea, lakini unaona mwamuzi anashindwa kufanya maamuzi hivyo, tumewafungia na kuwaondoa kabisa," alisema Shekha na kuongeza;
"Waamuzi wengine tunaona wanaonewa tu kama hawa wa mechi za jana (juzi) mabao yote yalikuwa halali kukataliwa kwa kuwa kulikuwa na kuotea sasa wengi hawajui hizi sheria. Wengine tunawasamehe hasa wale waliopo uwanjani wao wanaona mara moja tu, lakini ukija kuangalia marudio ndio unapoona waamuzi walikuwa sahihi tunazisihi timu zinazoshiriki na wao asiwe kama mashabiki."
Shekha aliongeza ingekuwa vyema, wasubiri wajiridhishe kabla ya kuja kutoa shutuma kali katika vyombo vya habari kuna makosa tunakiri, ndio kama hivi tunachukua hatua stahiki kwa wote wanaofanya vibaya."