Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwamuzi aliefeli Mtihani wa FIFA kuchezesha Ligi Kuu

Jonesia Rukyaaa Jonesia Rukyaa

Mon, 14 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya kelele nyingi mtandaoni baada ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) kutangaza marefa waliochezesha pambano la watani lililopigwa jana jijini Tanga, hasa Jonesia Rukyaa, shirikisho hilo limekata mzizi wa fitina likieleza sababu ya kumpa nafasi.

Jonesia alichezesha mechi ya fainali ya Ngao ya Jamii 2023 kati ya Simba na Yanga iliyopigwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga lakini mapema jina lake lilipotajwa atahukumu pambano hilo kelele zilikuwa nyingi kwa madai ni kati ya marefa waliofeli.

Wadau walikuwa wakipinga mwamuzi huyo kupewa mchezo huo wakidai hakupaswa kuchezesha kwa sababu alifeli mtihani wa utimamu wa mwili ulioandaliwa na FIFA, mtihani uliofanyika wiki mbili zilizopita jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF, Nassor Hamdun jana asubuhi aliliambia Mwanaspoti ni kawaida kwa waamuzi kufeli mtihani huo duniani kote na hupewa nafasi ya kurudia sehemu yoyote ile na hiyo haizuii mwamuzi kuchezesha mechi.

Hamduni alisema Jonesia na wenzake watatu walifeli mtihani huo wa kimataifa, ingawa mtihani wa darasani walifanya vizuri hivyo wataurudia huo wa utimamu wa mwili.

“Watu wanakuza sana mambo pasipo kuelewa, mtihani ambao hakufanya vizuri ni wa utimamu wa mwili unaosimamiwa na wakufunzi wa FIFA na wana nafasi ya kurudia hapo baadaye FIFA watakapopanga kipindi cha kuurudia, wakishindwa basi ndio wanaondolewa kwenye kuchezesha mashindano ya kimataifa chini ya FIFA,” alisema Hamdun na kuongeza;

“Ingekuwa ni hii ‘cooper test’ yetu ya ndani huwa wanarudia baada ya wiki moja, hata hawa ambao wamemaliza juzi kuna waliofeli na wanarudia wiki ijayo, hivyo Jonesia ana haki ya kuchezesha mechi hiyo na ni mwamuzi bora msimu uliopita, hii ni kawaida katika maisha ya binadamu na hata waamuzi wengine duniani kote ila wanapewa nafasi nyingine.”

Alisema hata wale waamuzi zaidi ya 20 waliofungiwa msimu uliopita tayari wameombewa kuchezesha mechi msimu huu na wanachosubiri ni kibali kutoka Bodi ya Ligi.

“Hivyo basi wadau wasishangae hata kuwaona wale waliokuwa wamefungiwa msimu uliopita wakichezesha, wamekubaliwa kinachosubiriwa ni kibali tu,” alisema Hamduni.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: