Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwameja: Usajili wa Yanga nusura uniue, Asajiliwa Simba kwa mabati

Mwameja (600 X 400) Mohammed Mwameja

Sun, 20 Feb 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Unamkumbuka huyu Supastaa! Anaitwa Mohammed Mwameja. Kipa mwenye historia ya kipekee kwenye soka la Tanzania na nahodha wa zamani wa Simba.

Japo hakuwahi kucheza Yanga, Mwameja anaeleza namna ambavyo alisajiliwa kihalali na klabu hiyo ya Jangwani mwaka 1993 usajili ambao kama si Mungu, huenda leo hii angebaki historia na angeshatangulia mbele za haki.

“Kuna mashabiki walitaka kunitoa roho sababu ya jambo lile, ni usajili ambao ulinifanya nipitie wakati mgumu sana na kama si Rais Mwinyi (Ali Hassan, rais wa awamu ya pili wa Tanzania) kutuliza upepo aliponiita sijui ingekuwaje? Labda ningeshakufa.”

Anasema kabla ya Rais Mwinyi kutoa tamko, yeye ilikuwa ajiunge na Yanga na tayari alishasaini mkataba na klabu hiyo kumpa Sh 3 Milioni.

“Nilikuwa na mahitaji yangu napaswa kuyakamilisha, Yanga waliponifuata sikuona taabu, wakati ule hatukuwa na mkataba unasaini fomu namba tano na fomu mama.

“Yanga walinifuata nikiwa kambini Arusha na timu ya taifa, wakati ule nilikuwa na mjengo wangu nyumbani Tanga sijaumalizia, nikawaeleza wakanipa Milioni 3, lakini pesa ile ilikuja kuwa sumu kwangu,” anasema.

“Kama sio Mungu kuniwekea mkono wake, huenda ningekufa sababu ya Simba na Yanga, usajili wangu Yanga kidogo usababishe nipoteze maisha, baada ya kugundulika nimesaini mkataba Yanga, nakumbuka ilikuwa usiku nimelala kuna watu walikuja nyumbani na kuniita.

“Ilikuwa mida ya saa nane au tisa hivi usiku, wakasema wao ni mashabiki wangu nitoke tuzungumze, wakati natoka nimefungua mlango wa mbao kabla sijafungua grili kumbe walikuja na tindikali wakanimwagia.

“Walimwaga haraka na kukimbilia kwenye gari yao ilikuwa Toyota Pick-Up’ wakaondoka, ile tindikali haikunifikia, iliishia kwenye grili na mimi kwa uoga nikaufunga ule mlango wa mbao nikarudi ndani, lakini usiku ule niliona kama mlango wa grili unachemka.

“Asubuhi kulipopambazuka nikakuta chuma cha grili chote kimeyeyuka, niliogopa, niliishi kwa tabu sana, ilikuwa ni vurugu sana, hizi timu zetu mbili zina mashabiki wa ajabu kweli kweli kisa tu mpira, kuna watu hawaoni shida kuwadhuru wenzao,” anasema.

Anasema baada ya usajili wake kutikisa na kusababisha amani kutoweka kwa upande wake, wakati huo akiwa tayari amefungiwa ndipo aliitwa na Rais Mwinyi.

“Hiyo ndiyo ilikuwa bahati kwangu, aliniuliza nini shida? nikamwambia mzee mimi kweli nimesajili Yanga, lakini lengo ilikuwa ni kumalizia nyumba yangu na klabu hiyo imenitimizia.

“Akaniuliza mapenzi yako yako wapi, nikamwambia yako Simba, akasema basi sawa baki Simba huko huko ikaja kugundulika na Ken Mkapa pia amesajiliwa Simba, hivyo ikaamuliwa kila mmoja arudi kwenye timu yake, mimi nikarudi Simba na Ken Mkapa akarudi Yanga, tukasamehewa.”

Anasema baada ya tukio lile hakuwahi kufikiria tena kucheza Yanga hadi alipostaafu soka mwaka 2001 akiwa kwenye klabu ya Simba.

FAINALI CAF

Mwaka 1993 Simba ilicheza fainali ya Afrika dhidi ya Stella Abidjan ya Ivory Coast kwa kutoka suluhu mechi ya ugenini kabla ya kupoteza mabao 2-0 Dar es Salaam mbele ya Rais Mwinyi, mabao yote mawili yakitiwa kambani na mwamba anayefahamika kwa jina la Boli Zozo. Hapa ndipo upepo ukageuka kwa Mwameja;

“Kila mtu alizungumza lake, wapo waliosema Mwameja hawezi kufungwa mabao kama yale, wengine walisema huyu baba yake ni Yanga na nyumbani kwao kulikuwa na bendera za Yanga, lakini yote niliyapokea kwa kuwa kuna muda unapaswa uwe na roho ya paka ili uweze kuishi na watu wa mpira,” anasema.

Mwameja aliyefahamika pia kama Tanzania One, aliingia matatani akiwa mmoja wa wachezaji waliotuhumiwa kuihujumu Simba, sambamba na beki George Magere Masatu, Malota Soma na Hussein Marsha, ilipochapwa 2-0 dhidi ya Stella Abdijan.

Kabla ya mechi hiyo ya fainali, mfadhili wa Simba wa wakati huo, Azim Dewji aliwaahidi wachezaji wote zawadi ya magari makubwa ya mizigo aina ya KIA kila mmoja lake, lakini ikatuhumiwa kuwa mfadhili huyo alipoona kutokana na mziki ule wa Simba wangeweza kuwa klabu ya kwanza Tanzania kuwa mabingwa wa Afrika, akaamua kuongea na baadhi ya wachezaji ili ‘awatoe’ wao wachache tu badala ya kubeba gharama kubwa ya kutimiza ahadi hiyo ya kikosi kizima, tuhuma ambazo Mwameja anasema sio za kweli.

Anasema mechi hiyo ilifuta historia, ndoto zake na kuharibu CV yake kisoka.

“Sijawahi kuacha kuikumbuka ile mechi katika maisha yangu yote, huwa nayakumbuka hadi mabao niliyofungwa mbele ya Rais Mwinyi na kukosa kombe.

“Kabla ya mechi tulijiamini kupita kiasi hasa baada ya kutoka sare kwao, viongozi wa mpira na wa nchi walikuwa wanakuja kambini na kupanga njia za kupitisha kombe la ubingwa kabla hata ya mechi kuchezwa, sitaisahau kamwe ile mechi,” anasema.

“Anasema usiku wa siku ya kuamkia mechi wachezaji kambini hawakulala, dua na maombi yalikuwa ni mengi ili mradi kila aliyeonekana anaweza kuisadia Simba ishinde alipelekwa kambini Zanzibar.

“Kuanzia saa 2 usiku hadi saa 9 alfajiri kambini kwetu ilikuwa ni bandika bandua, akitoka huyu kaingia yule, asubuhi saa nne siku ya mechi tumetoka Zanzibar kuja Dar es Salaam wachezaji tumechoka, na mechi ni jioni, kifupi hatukupata nafasi ya kupumzika kabisa.

“Nakumbuka bao la kwanza mabeki wangu watatu walipigwa chenga na Boli Zozo, ilikuwa ni goli la Kaskazini, mimi natoka yule bwana napishana naye anafunga goli.

“Goli la pili ilikuwa ni mpira wa krosi, kama anapiga ndani, akapiga nje ya penalti boksi likapigwa shuti, ile najaribu kuupangua ulikuwa na kasi kidogo, ukanipita, ilikuwa ni siku ngumu sana kwangu.

“Tulifungwa nyumbani tena kwenye mechi ya uamuzi, mechi ambayo ingebadilisha ndoto na historia, ilikuwa ni tofauti kupata matokeo kama yale, mpaka leo huwa naikumbuka, hakuna aliyehongwa, lakini tuliponzwa na kujiamini kupita kiasi,” anasema.

ASAJILIWA SIMBA KWA MABATI

Mwameja anaeleza namna usajili wake kutoka Coastal Union kwenda Simba ulivyotikisa, japo alikutana na changamoto, lakini alipewa mkwanja mrefu.

“Nilipewa laki nane na mabati 80, ilikuwa ni pesa nyingi sana kwa wakati ule, kifupi ulikuwa ni usajili ambao kama ni leo hii basi sijui ni wa staa gani hapa Bongo, japo nilipata changamoto na kukatishwa tamaa sana.”

Kipa huyo anasema kila klabu inapaswa kuwa na makipa watatu wenye ubora sawa na wote wawe na sifa ya kuwa makipa namba moja na ndivyo ilikuwa kwake alipotua Simba na kuwakuta makipa wanaotisha, Idd Pazi na MacKenzie Ramadhan.

“Ikitokea mmoja ana changamoto au kiwango kimepungua basi mwingine anakuwa mbadala, sio kipa namba moja akikosekana timu inahaha.

“Lakini pia wawe na ushindani, ingawa sasa makipa wetu hawana ushindani, kuna waliojiaminisha kuwa nafasi hii ni ya fulani, akiwepo fulani nafasi yangu ya kucheza haipo.

“Wanasahau kwamba siku kipa namba moja akiwa hayupo huyo, mwingine anapaswa achukue namba, kwa makipa wetu wazawa, wapo wazuri wengi na wengi wao ni vijana wadogo, lakini wanakosa kujiamini na kuwa na ndoto za kufika mbali zaidi,” anasema.

Anasema yeye alipowakuta kina Pazi na MacKenzie, hakutaka kujikatia tamaa na kuamini kuwa nafasi hiyo ni ya makipa hao.

“Nilikuwa na imani kuwa nafasi hiyo ni ya mtu yeyote na kila mmoja wetu ana haki kucheza na akili yngu ilikuwa siku nikipata nafasi naitendea haki,” anasema.

Anasema Pazi ni miongoni mwa nyota waliomshawishi yeye kujiunga na Simba, alimueleza kuwa kwa kiwango alichonacho anatamani ajiunge na klabu hiyo ili wasaidiane.

“Nilipotua Simba nakumbuka mechi yangu ya kwanza ya Ligi tulicheza na Pamba, Pazi alikuwa anaumwa, nilipewa nafasi nikaitendea haki, baada ya hapo kocha akawa ananipa nafasi kwa kutubadilisha badilisha, lakini siku zote timu inayoshinda mabadiliko hayafanyiki kwa kiwango kikubwa.”

Anasema makipa wanapaswa kuwa tayari kwa maana nafasi ikitokea unaitendea haki, sio mtu hayupo umepewa nafasi wanamkumbuka kipa ambaye hayupo.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz