Licha ya kufanya kazi timu mbalimbali na kwa mafanikio, Kocha Juma Mwambusi amesema kushuka daraja kwa Mbeya City imeimsononesha sana na kama watakubaliana na masharti yake yupo tayari kurejea kukisuka upya kikosi hicho na kurejesha heshima.
Kocha huyo mwenye heshima zake kwenye soka nchini kutokana na kile alichofanya kwenye timu kadhaa zikiwamo kubwa, kwa sasa hana timu baada ya kuachana na Ihefu aliyoiongoza msimu uliopita kwa mechi nane tu.
Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, kocha huyo anafunguka tamu na chungu kwenye kazi yake ya ukocha, hatma yake msimu ujao, heshima kwa wachezaji na makocha wazawa na nini wafanye Yanga, Simba, Azam na Singida Fountain Gate kimataifa.
Matokeo ya Mbeya City
Mwambusi anasema hadi sasa moyo wake umebeba maumivu baada ya kusikia timu yake ya zamani kushuka daraja akisema haelewi kilichoifikisha hatua hiyo licha ya kuanza vyema msimu.
Anasema enzi zake wakati anaipandisha ligi kuu msimu 2013/14 aliamini zaidi kwenye kuwapa nafasi vijana chipukizi kutoka mikoa ya nyanda za juu kusini na wachache wenye uzoefu wa maeneo mengine.
“Katika misimu minne niliyodumu Mbeya City nikianza kuipandisha, kisha msimu wa kwanza ligi kuu tunamaliza nafasi ya tatu, uliofuata tukahitimisha nafasi ya nne niliamini na kuheshimu vipaji vya vijana nikawapa nafasi,” anasema.
Anabainisha siri ya mafanikio kipindi akiitumikia City ni uongozi uliokuwapo chini ya aliyekuwa mkurugenzi wa Jiji, Idd Juma na katibu mkuu, Emanuel Kimbe ambao walimpa alichohitaji.
Anasema hakuna diwani au mtu mwingine aliweza kuingilia majukumu yake huku akipewa sapoti tu na waliokuwa viongozi wa timu hali ambayo ilimpa ufanisi mzuri.
“Enzi hizo mkurugenzi alikuwa Juma, katibu huu huyu Kimbe, hakuna mtu aliingilia majukumu yetu kwenye benchi la ufundi, nilichoomba nilipewa na timu ilifanikiwa kupata matokeo mazuri hadi tukapata heshima.”
Kilichomng’oa
Pamoja na mafanikio yote kwa misimu minne, lakini Mwambusi alishtua wengi alipotangaza kung’oka kikosini na kujiunga na Yanga na anaeleza mbali na ofa aliyoipata nje ya City, lakini mambo yalimbadilikia.
Anasema alichukizwa na baadhi ya waliokuwa madiwani kuanza kuhoji, kufuatilia na kuingia majukumu yake hali ambayo aliona itaweza kumchafua na kuamua kutimka.
Anaeleza badala ya vikao vijadili namna ya timu kuiboreshea mazingira wanaanza kuhoji, huku kila mmoja akitamani kuleta mchezaji wake ili asajiliwe hatua iliyomfanya kung’atuka.
“Sasa itakuaje kama kila mmoja anataka kuwa kocha, meneja au wakala… kuna diwani mmoja anataka alete mchezaji wake asajiliwe, kwenye kikao badala mtu achangie wazo la kusapoti yeye anashinikiza mchezaji wake acheze.”
“Nilipoona hali inazidi kukua, nikaona niondoke japokuwa Yanga waliniita wao na kunipa ofa nzuri na kuona nitafute changamoto mpya nje ya Mbeya City na ninafurahi nilifanya vizuri,” anasema Mwambusi.
Kuhusu Ihefu
Hadi sasa huenda baadhi ya wadau wa soka hawajajua sababu kubwa iliyomng’oa Mwambusi kwa muda mfupi baada ya kukabidhiwa mikoba Ihefu kuiongoza kama kocha mkuu akisaidiwa na Zuberi Katwila.
Mwambusi anabainisha yeye aliingia Ihefu kwa makubaliano maalumu ya kuwapa mbinu za muda mfupi na mrefu ili kuinusuru timu isishuke daraja, jambo ambalo lilifanikiwa kwani matokeo ya mwisho yalionyesha uhalisia.
Anasema yeye kufundisha na kutoa mbinu ni kazi yake, hivyo Ihefu baada ya kupitia kipindi kigumu mwanzoni mwa msimu walimpa jukumu la kuiwekea msingi imara ili kuondokana na mzimu wa matokeo yasiyoridhisha.
“Kama unakumbuka Ihefu licha ya kuanza vibaya ligi, ilikuwa ya kwanza kuifunga Yanga iliyokuwa imecheza zaidi ya mechi 45 bila kupoteza, lakini hata baada ya pale haikuyumba, unajua ni kwa nini?
“Niliingia pale kwa makubaliano maalumu kuisuka na kutengeneza mfumo wa kucheza soka la ushindani na la kuvutia ikiwa ni mbinu za muda mfupi na mrefu na timu ikaelewa na ikafanya vizuri,” anasema kocha huyo.
Yanga nayo
Anasema kutokana na kazi bora aliyoifanya Mbeya City, vigogo wa Yanga walimvutia simu wakitaka kufanya naye kazi na aliona asikatae ofa hiyo kwani soka ndiyo maisha yake.
Anasema msimu wa 2014/15 alijiunga na timu hiyo na kudumu miaka miwili na baadaye aliondoka kisha kurejea tena msimu wa 2016/17 na waliweza kufanya vizuri.
Anasema akiiongoza Yanga ndio walitwaa taji la kwanza la Kombe la Shirikisho (ASFC) walipoichapa Azam FC mabao 3-1, lakini mengine mawili ya ligi kuu ikiwa ni matokeo mazuri kwake.
Hata hivyo, anasema msimu uliofuata alitimka na kujiunga na Azam FC na hata huko akiwa na George Lwandamina waliweza kutwaa ubingwa kombe la Kagame na Mapinduzi ikiwa ni heshima kwake anayojivunia hadi sasa.
“Yanga nilienjoi sana kuliko sehemu nyingine yoyote, kwanza ndani na nje ya uwanja, japokuwa hata Prisons yalikuwa mazuri sana, kwa jumla najivunia mafanikio hayo,” anasema Mwambusi.
Mafanikio
Kocha huyo anasema moja ya furaha yake ni kuona timu nyingi alizotumikia kuwa na mafanikio makubwa kwani mbali na Mbeya City na Yanga, zipo nyingine zilinufaika naye ndani ya uwanja.
Anasema akiifundisha Tanzania Prisons walimaliza nafasi ya pili na kuipa tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika, lakini hata Azam aliipa mataji mawili, huku Tukuyu Stars ikiingia sita bora mwaka 2002 kwenye Tuscer Cup.
Awacharua viongozi
Kocha huyo mwenye misimamo yake anasema pamoja na kazi kubwa wanayoifanya makocha, wapo baadhi ya viongozi wanaokuwa mzigo kwenye timu hadi kusababisha matokeo yasiyoridhisha.
Anasema kama haitoshi mashabiki nao huwa kazi yao ni kuponda pale timu inapokosa matokeo mazuri huku viongozi wakiwa kimya bila kukemea tabia hizo na kumfanya kocha kukata tamaa.
“Kiongozi anakupangia timu, anaingia kwenye benchi la ufundi huku anashindwa kukemea mashabiki wanapomtukana kocha pale timu ikikosa matokeo mazuri kwa kukosa uvumilivu, kwa jumla hali hiyo hukatisha tamaa.”
Atetea wazawa
Mwambusi anasema tatizo kubwa linaloiathiri nchi yetu, wadau na mashabiki wengi wa soka wakiwamo viongozi ni kuwathamini wachezaji na makocha wa nje tofauti na wazawa.
Anasema thamani na heshima wanayoipata makocha au wachezaji wa kigeni haifanani wala kuendana na ya wazawa, hali ambayo kwa namna fulani inarudisha nyuma soka la Tanzania.
“Siongei kana kwamba sitaki makocha wa kigeni waje kufanya kazi hapa nchini, lakini hata sisi wazawa tupewe heshima sawa na hao wa nje sambamba na wachezaji wetu nchini wawe na thamani.”
“Mfano kile alichokuwa anapigania Feisal Salum ni sahihi kwa sababu wanafanya vizuri hata zaidi ya mgeni lakini masilahi kidogo, kwa nini inakuwa hivyo tofauti na wengine?” anahoji kocha huyo.
Soka la ushindani
Kocha huyo anawaasa wachezaji kupambana dhidi ya wapinzani wao kutoka nje ya nchi akieleza kwa sasa ligi ya Tanzania inaendelea kukua, hivyo lazima kila mchezaji kujituma ili kupambania namba.
Anasema hata uwapo wa wachezaji wa kigeni wameongeza ari na mvuto katika soka la Tanzania, akibainisha kujitambua kwao kutawafanya kutoka nje kupata uzoefu zaidi.
“Soka linapiga hatua, hata kuwapo kwa wachezaji wa kigeni kunaamsha ari na morali kwa wazawa hivyo lazima wajitambue nao watoke nje kupata changamoto.”
“Sisi makocha hatutoki kutokana na masilahi huko kwa wenzetu, mfano mimi nilipata ofa huko Rwanda timu ya Kiyovu lakini malipo yao ni madogo sana, niliambiwa laki tano mshahara sasa si bora hapa nyumbani,” anasema Mwambusi.
Simba, Yanga zifanye hivi
Kutokana na mafanikio ya Yanga msimu uliopita ya kucheza fainali Kombe la Shirikisho Afrika, Mwambusi anasema ni matokeo ya heshima kwao na nchi kwa jumla, akisema walijipanga nje na ndani.
Anasema hata akiwa Yanga chini ya Kocha mkuu, Hans Van Pluijm waliifikisha timu hiyo robo fainali japokuwa walishindwa kuvuka hapo kutokana na kukosa wachezaji wenye uwezo na uzoefu.
“Ninawapongeza, walifanya vizuri na sasa Tanzania lazima wanaijua kupitia Yanga kwa mafanikio hayo, mimi nikiwa na Hans tulifikia robo fainali ila tulikosa kuwa na kikosi bora cha wapambanaji,” anasema kocha huyo.
Anaeleza pamoja na mafanikio hayo, Yanga wanapaswa kuwalinda mastaa wao walioonyesha uwezo hadi kufikia mafanikio hayo, lakini kuongeza wachezaji wachache ili kuziba matundu yaliyoonekana.
“Kama wataona wawauze, wajitahidi kuleta wengine wenye uwezo sawa na hao, lakini kikubwa wabaki na nyota wao hasa ambao walifanya vizuri,” anaongeza Simba licha ya kuendeleza rekodi yao ya kufika robo fainali klabu bingwa Afrika kwa misimu minne mfululizo, lakini kuuza wachezaji wake kiliwagharimu lakini hata maandalizi hayakuwa mazuri.
Anasema anaamini msimu ujao Wekundu hao watafanya vizuri kama watafanya usajili wenye kuendana na ukubwa wao ili kuweza kuleta mabadiliko na kuwania ubingwa ndani na nje.
“Waimarishe kikosi, wafanye maandalizi ya kweli, kusahihisha makosa ili kurejesha ile morali na ushindani waliokuwa nayo, naamini wanaweza kuja kivingine msimu ujao.”
“Singida Fountain Gate wajifunze kwa wakubwa wao kuona walifanikiwaje au kukwama vipi ili wanapoenda kushiriki michuano ya kimataifa wasiwe wanyonge, Azam pia wanao uzoefu kikubwa ni kujipanga,” anasema Mwambusi.
Msimu ujao
Kocha huyo anafafanua kwa sasa anaendelea na kilimo cha mpunga na mahindi huko maeneo ya Malawatu wilayani Mbarali na shughuli nyingine nje ya uwanja.
Anasema licha ya majukumu hayo, lakini yuko tayari kufanya kazi na timu yoyote watakayokubaliana kwa masharti yake na anaamini uwezo anao hata akikabidhiwa timu za Taifa.
“Mimi nalima huko shambani, lakini si kwamba nimestaafu soka, niko tayari msimu ujao kwa timu yoyote itakayohitaji huduma kwa makubaliano naweza kufanya kazi,” anasema kocha huyo.