Aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans, Fredrerick Mwakalebela amewataka viongozi na Benchi la Ufundi la klabu hiyo, kuutumia mchezo kati ya Simba SC dhidi ya Al Ahly kuwasoma wapinzani wao watakaokutana nao katika hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba SC itacheza dhidi ya Al Ahly katika michuano ya African Football League, mchezo utakaopigwa Oktoba 20, mwaka huu kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam.
Young Africans watakutana Al Ahly katika michuano hiyo ya kimataifa, ambao wamepangwa Kundi moja wakiwa na timu nyingine Medeama ya Ghana na CR Belouzdad ya Algeria.
Mwakalebela amesema kuwa ni nafasi pekee kuutumia mchezo huo dhidi ya Simba SC kuwasoma wapinzani wao kwa kuangalia ubora na udhaifu wao uwanjani.
Aliongeza kuwa Young Africans hawatakiwi kuogopa historia yao ambayo inawabeba katika ukanda wa Afrika, na badala yake kuandaa mikakati ya ushindi wa nyumbani kabla ya kurudiana ugenini.
“Sasa hivi imebakia historia pekee kwa Al Ahly, kwani soka la Afrika limebadilika hivi sasa, Young Africans ina uwezo wa kwenda kucheza soka na timu za Urabuni na kupata ushindi nyumbani na ugenini.”
“Na hiyo imejitokeza katika msimu uliopita ambao tulicheza Kombe la Shirikisho Barani Afrika, tumefanikiwa kupata ushindi ugenini, kikubwa viongozi kujipanga na kuachana na historia.”
“Benchi la Ufundi na Viongozi itakuwa nafasi nzuri kwao, kuwaangalia Al Ahly watakapocheza mchezo wao dhidi ya Simba SC kwenye Uwanja wa Mkapa kwa lengo la kujua ubora na udhaifu wao uwanjani,” amesema Mwakalebela