Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwaka wa Afrika Mashariki Afcon

48732 AFCON+PIC

Wed, 27 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ni mwaka wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Afcon. Ndivyo tunavyoweza kusema baada ya nchi nne kati ya sita zinazounda EAC kufanikiwa kuweka historia kwa kupata tiketi ya kushiriki mashindano ya Afcon mwaka huu.

Fainali za Afcon kwa mwaka huu, zitafanyika kuanzia Juni hadi Julai nchini Misri na kwa mara ya kwanza zitashirikisha mataifa 24 badala ya 16 kama ilivyozoeleka huko nyuma.

Ushindi wa Stars wa magoli matatu katika Uwanja wa Taifa juzi, umeifanya iungane na majirani zake Burundi iliyofanikiwa kupata fursa hiyo baada ya kutoka sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Gabon iliyomjumuisha kikosini nyota wake anayekipiga katika kikosi cha Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang.

Nchi zingine za Afrika Mashariki zilizofuzu ni Kenya iliyokuwa Kundi F na Uganda ambayo licha ya kufungwa na Tanzania imeongoza Kundi L.

Katika mchezo wa mwisho mwishoni mwa wiki, goli la Burundi lilifungwa na Cedric Amissi katika dakika ya 76 kabla ya Gabon kusawazisha kupitia goli la kujifunga la Omar Ngando zikiwa zimesalia dakika nane mpira kumalizika.

Kwa matokeo hayo Burundi imemaliza ya pili katika Kundi C, hivyo kuungana na vinara Mali waliotangulia kukata tiketi ya fainali hizo.

Kupita kwa Tanzania iliyo nafasi ya 137 katika viwango vya Fifa kabla ya mechi ya Jumapili, haikuwa kazi rahisi kutokana na upinzani uliopo kati yake na Uganda katika soka.

Iwe isiwe ilikuwa ni lazima kwa Taifa Stars kupata ushindi ili kujihakikishia nafasi hiyo iliyoisubiri kwa miaka 38 tangu iliposhiriki kwa mara ya kwanza na ya mwisho mwaka 1980 mashindano hayo yalipofanyika Nigeria.

Stars imefuzu fainali hizo baada ya kupata alama nane katika kundi lake huku wapinzani wao Lesotho waliokuwa wamefungana alama kabla ya mchezo wa juzi, wakitoka suluhu ya bila kufungana na Cape Vede na kufikisha alama sita. Cape Verde wamemaliza wa mwisho wakiwa na alama tano.

Kufuatia ushindi huo, mashabiki wa soka wa Tanzania wakiwamo viongozi wametoa kauli mbalimbali, kupongeza na kushauri mambo muhimu kufanyika ili ushiriki wa timu hiyo uwe wa mafanikio zaidi katika fainali hizo.

Baadhi ya mashabiki akiwamo Rais John Magufuli hawakusita kuimwagia sifa Stars ambapo katika taarifa yake ya video fupi iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii, mkuu huyo wa nchi anasema “Kwa kweli leo nimefurahi sana kwa jinsi walivyoshinda, sasa angalau Stars wameipa heshima nchi yetu.

“Taifa Stars oyee...Tanzania oyee…leo nimeona mpira siyo ule uliopita mliocheza siku za nyuma, ndio maana leo sikutaka kwenda uwanjani niliangalia hapa hapa (Ikulu). Nawapongeza sana Watanzania na wote waliohamasisha ushindi huu mkubwa,” anasema.

Mbali na hilo, Rais Magufuli anasema amefurahia namna ambavyo timu za Lesotho na Cape Verde zilivyotoka suluhu huku akisema hivi sasa mambo yanakwenda vizuri.

Namna zilivyopita katika makundi

Timu zote za EAC zimemaliza zikiwa nafasi ya pili katika makundi yao kasoro Uganda iliyoongoza kundi L ikiwa na alama 13 na kufuatiwa na Taifa Stars iliyomaliza ya pili.

Katika kundi hilo, Uganda ilicheza mechi sita ikashinda nne kwa kuwafunga Cape Verde na Lesotho nyumbani na ugenini, kutoka sare moja na kupoteza moja zote zikiwa ni mbele ya Taifa stars wakianzia Kampala na baadaye Dar es Salaam, juzi.

Kenya ikiwa na alama saba katika Kundi F ilimaliza nyuma ya vigogo vya soka la Afrika, Ghana, iliyoongoza baada ya kukusanya alama tisa kwa kushinda michezo mitatu na kupotza mmoja.

Majirani hao ndani ya EAC walishinda michezo miwili, kutoka sare mmoja na kupoteza mmoja na kuiacha Ethiopia iliyoshika nafasi ya tatu ikiwa na alama moja. Katika kundi lao timu ya Sierra Leone iliondolewa.

Kwa upande wake Burundi ilimaliza ya pili ikiwa na alama 10 katika Kundi C lililoongozwa na Mali iliyokusanya alama 14, kutokana na michezo sita ambapo ilishinda minne na kutoka sare miwili, huku wakiziacha Gabon iliyopata alama nane na Sudan Kusini ambayo haikupata hata alama moja.

Majirani wengine wa Tanzania waliofuzu kucheza fainali hizo ni Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), iliyoungana na Zimbabwe kutoka Kundi G kwenda kwenye fainali hizo.

Pia, Msumbiji imepata nafasi ya kushiriki fainali hizo kutoka Kundi K nyuma ya Guinea-Bissau iliyoongoza kundi lao lililozihusisha pia Namibia na Zambia.

Hata hivyo, Rwanda na Sudan Kusini ambazo pia ni miongoni mwa nchi zinazounda EAC zimeshindwa kufuzu katika makundi yao.



Chanzo: mwananchi.co.tz