Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwaka 2023 utabaki katika vitabu

Mwaka 2023 Mwaka 2023 utabaki katika vitabu

Sun, 17 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Zimebaki siku 15 tu kabla ya kumalizika mwaka 2023 yapo mambo mazuri yaliyoteka hisia za wengi kwenye soka hapa nchini na hata nje ya mipaka ya kwetu ambayo yatabaki kama kumbukumbu au alama kubwa ndani ya mwaka huu.

SAKATA LA FEI TOTO

Miezi mitatu ndani ya mwaka huu tukio ambalo liliteka hisia za wengi ilikuwa ni juu ya aliyekuwa kiungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuandika barua rasmi ya kutaka kuondoka klabuni hapo.

Fei Toto aliandika barua hiyo Machi 6 akiitaka Yanga kupokea fedha za kuununua mkataba wake kisha atimkie klabu nyingine lakini viongozi wa klabu hiyo walilikataa na kulifanya sakata hilo kuwa refu na kuburuzana Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Hata hivyo, baada ya mvutano mrefu huku Fei akigonga mwamba kwenye kamati za sheria pale TFF hatimaye mkombozi akaja kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Juni 5 akiitaka Yanga kumaliza mzozo huo na mchezaji wao na klabu hiyo kufanya kweli kwa kumuuza mchezaji huyo kwa timu iliyokuwa ikituhumiwa kumshawishi ya Azam FC.

YANGA FAINALI CAF

Mwaka huu ukawa na rekodi kubwa kwa klabu ya Yanga baada ya kuweka rekodi kubwa ya kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa ni mara ya kwanza kwenye historia yao.

Yanga ilicheza fainali hiyo Mei 28 dhidi ya USM Alger ikianzia hapa nyumbani ilipopoteza kwa mabao 2-1 kisha waliporudiana Juni 3 wakapindua meza na kushinda kwa bao 1-0 kule Algeria na kulikosa kombe hilo kupitia kanuni ya mabao mengi zaidi ya ugenini.

MAYELE AUZWA PYRAMIDS

Julai 30 klabu ya Pyramids ya Misri ilitangaza rasmi taarifa iliyowanyong’onyeza mashabiki wa Yanga ya kwamba wamefanikiwa kumsajili kwa kumnunua mshambuliaji Fiston Mayele.

Mshambuliaji huyo Mkongomani ambaye ndani ya miaka miwili alikuwa na jina kubwa kufuatia ubora wake wa uwanjani na hata shangilia yake ya kutetema, alifanikiwa kutengeneza jina kubwa tangu asajiliwe akitokea AS Vita ya kwao DR Congo.

Akiwa hapa nchini Mayele kwenye msimu wake wa kwanza alimaliza wa pili kwa ufungaji bora akipachika mabao 16 huku mfungaji bora akiibuka George Mpole aliyefunga mabao 17.

Msimu uliofuata Mayele aliibuka mfungaji bora kwa ligi ya ndani akifunga mabao 17 akifungana na Said Ntibazonkiza ‘Saido’ wa Simba huku pia akiibuka mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho Afrika akifunga mabao 7.

YANGA YAIPIGA SIMBA 5-1

Bado ulikuwa mwaka wenye neema kwa Yanga baada ya kufanikiwa kupata ushindi mkubwa ulioshtua wakiwachapa watani wao Simba kwa mabao 5-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu msimu huu.

Hakuna ambaye alitarajia ushindi mkubwa kama huo kwa timu zote kipigo ambacho kiliifanya Simba imtimue aliyekuwa kocha wao Robert Oliveira ‘Robertinho’ baada ya matokeo hayo huku pia kusababisha presha kubwa kwa viongozi wa klabu hiyo.

STARS YAFUZU AFCON

Septemba 8 ikaja habari njema kwa taifa ya Tanzania baada ya Taifa Strs kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Ivory Coast.

Stars ilifuzu ushiriki wa fainali hizo kwa tiketi iliyokatiwa nchini Algeria ilipolazimisha suluhu dhidi ya miamba hiyo ya Afrika, na kuwa ni mara ya tatu katika historia kwa Tanzania kufuzu Afcon baada ya kufanya hivyo pia 1980 na 2019.

NOVATUS ACHEZA UEFA

Kiungo Novatus Dismas Miroshi naye akaipa heshima kubwa Tanzania baada ya Septemba 19 kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na klabu yake mpya ya FC Shakhtar Donetsk ya Ukraine.

Miroshi alicheza mchezo huo dhidi ya Porto ya Ureno ambao licha ya kupoteza kwa mabao 3-1 kiungo huyo alimudu kucheza kwa dakika 90 za mechi hiyo akiwa ni mchezaji wa tatu wa Kitanzania kucheza mashindano hayo makubwa Ulaya akitanguliwa na Kassim Manara na Mbwana Samatta.

TANZANIA KUANDAA AFCON

Habari kubwa nyingine iliyoshtua ikaja Septemba 27 baada ya Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutangaza Tanzania kuwa kati ya nchi tatu zitakazoandaa fainali za Mataifa Afrika.

Tanzania itaandaa fainali hizo za mwaka 2027 sambamba na mataifa ya Uganda na Kenya baada ya nchi hizo tatu kushirikiana kuomba nafasi ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo kwa mara ya kwanza.

SIMBA NA AFL

Simba ikawa mwenyeji wa mashindano mapya ya African Football League baada ya kuandaa ufunguzi wa mashindano hayo makubwa na mapya kabisa hapa Afrika kwa ngazi ya klabu.

Ufunguzi huo ulifanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kufana vilivyo ukihudhuriwa na watu wengi wazito akiwamo Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi, Rais wa Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino na mwenzake wa Afrika Dk Patrice Motsepe pamoja na kocha wa zamani wa Arsenal ya England, Arsenhe Wenger.

Katika ufunguzi huo uliofana kwa mashabiki 60,000 kujaa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kupambwa na burudani za aina yake, Simba na Al Ahly ya Misri zilitoka 2-2.

Chanzo: Mwanaspoti