Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwadui yarejea Championship, Copco ndo basi tena

Fdyugudg Mwadui yarejea Championship, Copco ndo basi tena

Tue, 21 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Timu ya Mwadui FC imefanikiwa kupanda daraja kwenda Championship baada ya kuifunga Copco FC kwa jumla ya mabao 5-2 kwenye mchezo wa mtoano (play off) kusaka nafasi ya kupanda na kubaki Championship.

Mwadui iliyoshuka daraja kutoka Championship msimu wa mwaka 2020/2021 imepanda daraja leo Mei 21, 2024 baada ya sare ya mabao 2-2 na Copco FC kwenye mchezo wa marudiano ambao umechezwa katika Uwanja wa Nyamagana, Mwanza.

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Mei 17, mwaka huu katika Uwanja wa Nyankumbu, Geita, wenyeji Mwadui FC walipata ushindi wa mabao 3-0. Mwadui ambayo iko First League imepata nafasi hiyo baada ya kumaliza katika nafasi ya nne.

Copco FC ambayo ilimaliza nafasi ya 14 kwenye Ligi ya Championship, ilifungwa kwa jumla ya mabao 3-2 na Stand United ya Shinyanga kwenye mchezo wa mchujo ya kwanza.

Kwa matokeo ya leo Copco FC ambayo imedumu kwenye Championship kwa misimu miwili imeshuka daraja na itacheza First League msimu ujao.

Kushuka daraja kwa Copco FC inamaanisha msimu ujao Jiji na Mkoa wa Mwanza hautakuwa na timu yoyote kwenye Ligi ya Championship baada ya Pamba Jiji kupanda Ligi Kuu. Mwanza itakuwa na timu tatu za Copco, Mapinduzi na Alliance FC kwenye First League.

Nahodha wa Mwadui FC, Salum Chuku ndiyo amekuwa shujaa baada ya kuifungia timu yake mabao mawili leo na kuzima ndoto za wenyeji Copco FC kusalia Championship.

Chuku amefunga mabao hayo dakika ya 24 kwa shuti la mguu wa kushoto akiunganisha mpira uliookolewa na mabeki wa Copco FC kwenye pigo la kona. Amefunga bao la pili dakika ya 90 kwa shuti kali la mguu wa kushoto.

Dalili mbaya kwa Copco FC katika mchezo huo zimeonekana mapema dakika ya 16 ambapo timu hiyo imepata penalti kufutia kipa wa Mwadui, Hamza Mohamed kumuangusha straika, Kelvin John lakini Khalid Kabailo mkwaju wake ukaokolewa na kipa.

Copco wamepata bao la kwanza dakika ya 55 baada ya kipa wa Mwadui, Hamza Mohamed kujifunga wakati akiokoa hatari langoni kwake. Timu hiyo imepata bao la pili dakika ya 90+7 kupitia kwa Shaffih Adam kwa faulo ya moja kwa moja.

Shujaa wa Mwadui, Salum Chuku, amesema, ”nashukuru Mungu timu imefanikiwa kuingia Championship na mimi kuisaidia timu yangu kuifikia hatua hii ni jambo la faraja kwangu, kwa wachezaji wenzangu na timu kwa ujumla.”

Kocha wa Mwadui, Salhina Mjengwa amewapongeza wachezaji wake kwa kufanikisha hatua hiyo na kutimiza malengo waliyodhamiria kwani mchezo huo haukuwa rahisi kucheza na timu inayopambania kutoshuka daraja.

Chanzo: Mwanaspoti