Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwadui, Kagera Sugar vita ya ndugu

Mwadui Pic 1 Data Mwadui, Kagera Sugar vita ya ndugu

Tue, 11 May 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Wakati Ligi Kuu ikiendelea leo Jumanne Mei 11, 2021 kwa mchezo mmoja tu, itashuhudiwa vibonde wa michuano hiyo kutoka Kanda ya Ziwa, Mwadui na Kagera Sugar wakinyukana kusaka alama tatu ili kujinasua mkiani.

Hadi sasa Mwadui ambao ni wenyeji wa mchezo huo ndio wanaburuza mkia kwa pointi 19, huku Kagera Sugar wakiwa nafasi ya 17 kwa alama 27 baada ya kila timu kushuka uwanjani mara 28.

Mwadui wanaingia dimbani wakikumbuka rekodi nzuri ya kushinda mechi mbili mfululizo wakianzia ugenini walipoilaza Gwambina mabao 2-1 kisha kuilalua Coastal Union mabao 3-0 katika mchezo wa kombe la shirikisho.

Kwa upande wa Kagera Sugar wao, wanawakabili wapinzani wakikumbuka kupoteza mechi tatu za mwisho wakianza kufa dhidi ya Biasharan United mabao 2-1 kisha kuchakazwa mbele ya Simba mabao 2-0 katika mechi ya ligi kisha wakalizwa 2-1 kwenye FA.

Mchezo wa leo ambao utapigwa Mwadui Compex mkoani Shinyanga, unatarajia kuwa na upinzani mkali ikiwa wenyeji wanasaka mwendelezo wa ushindi na kujipa heshima, huku wapinzani wakisaka alama tatu ambazo wamezikosa kwa muda mrefu.

Pia mchezo huo utakuwa ni mtihani mwingine kwa Kocha wa Kagera Sugar, Francis Baraza ambaye tangu aajiriwe kikosini humo kuchukua mikoba ya Mecky Maxime hajaonja ushindi wowote katika michezo sita.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz