Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muuaji wa Uganda atamba kuimaliza tena kwa Mkapa

TAIFA STARS MISRI 1 1140x640 Wachezaji wa Taifa Stars

Mon, 27 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mfungaji wa bao pekee la timu ya taifa, Taifa Stars dhidi ya Uganda The Cranes kwenye mechi ya Kundi F ya kuwania Fainali za Afcon 2023, Simon Msuva amesema amefurahi kutimiza ahadi yake ya kuitungua Uganda nchini Misri, lakini akisisitiza hata watakaporudiana nao watawapiga tena.

Msuva aliyefunga bao hilo kwenye Uwanja wa Suez Canal, Ismailia na kumfanya afikishe jumla ya mabao 20 kupitia mechi 77, kabla ya mchezo huo nyota huyo anayekipiga Saudi Arabia alisema alitamani sana kuifunga Uganda na kuahidi kupambana kutimiza lengo ili kuivusha Stars.

Ushindi wa juzi ulikuwa wa kwanza kwa Stars katika kundi hilo kwani ilianza na sare ya 1-1 na Niger ugenini kabla ya kucharazwa mabao 2-0 nyumbani na kinara, Algeria na keshokutwa Jumanne itarudiana na The Cranes ili kufufua matumaini ya kwenda Afcon kwa mara ya tatu.

"Nimefurahi kuwa sehemu ya matokeo tuliyoyahitaji, sote tunafahamu ubora wa Uganda, hivyo sherehe ya matokeo ya mchezo huu imemalizika na sasa tunaelekeza nguvu kwenye mchezo wa nyumbani, nikiamini tukikomaa tena tunawapiga The Cranes," alisema Msuva nyota wa zamani wa Moro United, Yanga, Difaa el Jadida na Wydad Casablanca za Morocco.

Msuva alisema anaamini Stars itapata ushindi nyumbani na kukusanya pointi za kuiwezesha kwenda Ivory Coast na kuwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kuipa nguvu timu hiyo ambayo ilishiriki fainali za Afcon 1980 zilizofanyika Nigeria na ilienda Misri mwaka 2019.

"Sisi tupo kwa ajili ya nchi, tunahitaji sapoti ya mashabiki kwa sababu wao wana mchango mkubwa, muda mwingine mashabiki wanaweza kuwavuruga wapinzani kwa kuwatoa nje ya mchezo na kutufanya tuwe na kazi nyepesi," alisema, huku beki Dickson Job, aliye asisti bao hilo alikazia kwa kusema;

"Tunatakiwa kufanya vizuri kwenye michezo yetu yote miwili iliyosalia tukiwa nyumbani (Kwa Mkapa) kwa kufanya hivyo tunaweza kwenda Ivory Coast."

Ushindi wa juzi umeifanya Stars ichupe hadi nafasi ya pili ikifikisha pointi nne ikiishusha Niger yenye alama mbili iliyofumuliwa na vinara wa kundi hilo, Algeria yenye pointi tisa kwa sasa, huku Uganda ikiburuza mkia ikiwa na alama moja tu kila timu ikicheza michezo mitatu kwa sasa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live