Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mutale awataka Yanga, Balua aahidi mabao

Mutale Simba Apr Mutale awataka Yanga, Balua aahidi mabao

Tue, 6 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya APR ya Rwanda, katika Tamasha la Simba Day, winga mchachari wa timu hiyo, Mzambia, Joshua Mutale, amesema wamesahau hilo na sasa akili na nguvu zote wanazielekeza katika mechi inayofuata dhidi ya Yanga.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mutale, mmoja wa wachezaji wapya, waliosajiliwa msimu huu akitokea Power Dynamos ya Zambia, alisema baada ya kupata ushindi huo, wamekuwa na ari na kujiamini kiasi cha kutaka kuendeleza ushindi katika mechi ijayo ili kuwapa furaha mashabiki wao ambao walijitokeza kwa wingi Jumamosi kuwasapoti.

"Tumewaonyesha mashabiki ni kitu gani tunataka kufanya kuelekea msimu ujao, kizuri ni kwamba tumeanza kilele cha Simba Day kwa ushindi, na sasa tunaangalia mechi inayofuata dhidi ya Yanga, tunajiandaa na hilo na tutapambana," alisema winga huyo ambaye alionesha kiwango kikubwa katika mchezo huo.

Mchezaji huyo ameonesha kushangazwa na umati mkubwa uliojitokeza akisema ni kitu cha ajabu sana kukiona kwa macho.

"Ni kitu cha ajabu sana kwangu hiki nilichokiona, umati mkubwa kama ule, ulitufanya wachezaji kupambana uwanjani, kwangu ilikuwa ni mechi ya kwanza kubwa ya aina yake nikiwa na Simba," alisema Mutale.

Mfungaji wa bao la pili katika mechi hiyo, Edwin Balua, aliwaahidi wanachama na mashabiki wa timu hiyo kuwa msimu huu atafunga sana mabao ya faulo kuliko uliopita.

Balua, aliyesajiliwa dirisha dogo la usajili akitokea Prisons, alisema msimu uliopita alifunga machache kutokana na kutokuwa chaguo la kwanza kwa makocha kwenye upigaji wa mipira iliyokufa.

"Nimefunga bao la mkwaju wa faulo katika mechi dhidi ya APR si kwa bahati mbaya, kwa sababu huwa nafanyia mazoezi kupiga mipira ya aina hii.

Msimu uliopita sikupiga sana kwa sababu ilikuwa ni mipango ya mwalimu kwani niliwakuta wapigaji wengi wazuri, ingawa na mimi nimeshafunga mabao ya aina ile, nilifanya hivyo na Namungo, wakati nipo Prisons niliifunga Simba, kwa hiyo si kitu kigeni sana.

Nawaambia mashabiki wa Simba tegemeeni mabao mengi ya faulo msimu huu, tunawashukuru sana kwa kujaza uwanjani, sasa wachezaji tunataka kuwalipa kwa kuwapa furaha," alisema.

Naye Awesu Awesu, aliyesajiliwa msimu huu akitokea KMC, alisema hatimaye ndoto yake imetimia, kwani alikuwa anataka siku moja awe mmoja wa wachezaji watakaotangazwa kwenye tamasha kubwa hilo, akiwa na kikosi cha Simba.

"Ni siku ambayo ilikuwa kwenye ndoto yangu, nilikuwa nafikiria na mimi kuwa mmoja wa watu watakaokuwa kwenye tamasha kubwa kama hili, nashukuru Mungu nimetimiza kwa kitu ambacho nilikuwa nakipenda.

Nilipotambulishwa hisia zangu nilikuwa kali sana, unajua kila mchezaji yoyote nchini anapenda kucheza timu kubwa kama hizi, narudia kusema hii ni ndoto niliyokuwa naisubiria maishani, kupambana kwangu kote nilikuwa nataka siku moja nicheze kwenye klabu ya Simba," alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live