Mshambuliaji wa Klabu ya Yanga, Keneddy Musonda ametoa neno la shukrani kwa aliyekuwa Kocha Mkuu wa Timu hiyo, Nassreddine Nabi ambaye ameachana na Yanga tangu jana usiku baada ya kataba wake kumalizika.
Musonda ambaye ni raia wa Zambia aliyesajiliwa Yanga katika dirisha dogo amesema kuwa Nabi ni mwalimu ambaye amemfundisha shauku ya kushinda na amemsaidia mambo mengi.
"Profesa nataka kusema asante kwa kila kitu ulichofanya kwa ajili yangu kwa miezi michache iliyopita. Umenifundisha sana kuhusu mchezo na kunisaidia mimi kuwa Mchezaji mzuri.
"Pia, nafahamu kwa namna gani ulinionyesha namna ya kushinda kwa shauku na kuwa na msimamo endelevu, najihisi nimekuwa imara chini ya muongozo wako na kwa hakika nakushukuru kwa hili.
"Nitakwenda kukumbuka kucheza kwaajili yako, lakini kila mara nitakumbuka masomo uliyonifundisha. Asante tena kwa kila kitu," ameandika Musonda.