Hospitali ya Taifa Muhimbili imefuzu kuwa na uwezo wa kushughulikia dharura za kiafya zinazoweza kujitokeza katika michuano ya Mpira wa Miguu Barani Afrika (AFCON 2027) ikiwa Afrika Mashariki itapewa ridhaa ya kuwa mwenyeji wa michuano hiyo.
Haya yameelezwa na Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Saidi Yakub ambaye aliambatana na jopo la Wakaguzi kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) ambao wapo nchini kukagua miundombinu muhimu ikiwemo viwanja vya michezo, Hoteli, Viwanja vya ndege na Hospitali.
Katika kukagua leo wamefika hapa hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo wamekagua Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali, mashine za kisasa za uchunguzi lakini pia wamepata maelezo mazuri kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed ambaye ameeleza uwezo na utayari wa MNH katika kutatua dharura zozote zinazoweza kujitokeza” amesema Bw. Yakub
Amesema ukaguzi unakwenda vizuri na kwamba Muhimbili imekidhi vigezo vilivyotakiwa na zinasubiriwa tu baadhi ya nyaraka ambazo wakaguzi hao wameziomba
Awali akiwasilisha mada kwa wakaguzi hao, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Mohamed Janabi alisema kuwa Muhimbili ndio hospitali kubwa nchini, ikiwa na vitanda 2,150 katika kampasi zake za Upanga na Mloganzila huku ikiwa na wataalamu bingwa wa kada zote, ina mashine za vipimo vya uchunguzi ikiwemo MRI 3, CT Scan 3, Angio Suit 1 pamoja na Idara ya Magonjwa ya Dharura yenye uwezo wa kuhudumia watu wapatao 250 kwa siku.
“Kijiografika katika eneo iliyopo Hospitali yetu kuna Hospitali mbili za Ubingwa wa Juu ambazo ni Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI) ambazo kwa pamoja zina uwezo wa kutatua changamoto yoyote inayoweza kujitokeza” ameeleza Prof. Janabi
Tanzania imeomba kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Mpira wa Miguu barani Afrika (AFCON 2027) kwa kushirikiana na nchi jirani ambazo ni Kenya na Uganda.