STRAIKA wa Simba, Mkongomani Chriss Mugalu amerudi kwao akipambana na tiba ili akae sawa kwa haraka. Staa huyo aliumia nyama za paja hivi karibuni na hajacheza mchezo wowote wa Ligi.
Akiwa kwao DR Congo Mugalu, ameliambia Mwanaspoti anaendelea vizuri na matibabu kama alivyoelekezwa na madaktari ambao walianza kumtibia hapa nchini.
Mugalu alisema hata matibabu ambayo anayafanya huko DR Congo madaktari wake wamekuwa wakiwasiliana ili kubadilisha maarifa na kujua anatakiwa kufanya jambo gani kutokana na maendeleo yake ingawa hakuweka wazi anatibiwa na wataalam gani wa kiwango gani.
Lakini ameweka wazi kwamba kwa sasa yupo vizuri kuliko alivyokuwa hapa nchini.
“Bado sijafahamu naweza kurejea kwa wakati gani uwanjani lakini matibabu ambayo nayafanya sasa ni hali ya juu na natakiwa kupumzika muda mwingi ndio maana nimerudi nyumbani,” alisema na kuongeza;
“Nikiwa hapo Tanzania nikiona wachezaji wanzangu wanaenda mazoezini, kambini au uwanjani kucheza mechi huwa naumia mno jambo ambalo huenda lingefanya akili yangu kutokuwa sawa na kuchelewa kupona kwa haraka,” aliongeza
“Nitarudi Tanzania baada ya maendeleo yangu kuwa fiti na muda ambao nitatakiwa kufanya yale mazoezi madogo madogo kabla ya kujiunga pamoja na wenzangu,” alisema
Msimu uliopita mbali ya kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara Mugalu alicheza mechi chache katika kikosi cha Simba za Ligi Kuu Bara na kumaliza na mabao 15 nyuma moja ya John Bocco ambaye alikuwa mfungaji bora.