Mkongwe wa soka Paul Merson, anaamini usajili wa Mykhailo Mudryk sio wa Graham Potter bali umetokana na mabosi wa klabu ya Chelsea.
Chelsea ilimsajili Mudryk kwa kitita cha Pauni 88 milioni akitokea Shakhtar Donetsk lakini kwa mujibu wa mkongwe huyo Potter hakuhusika.
Licha ya Mudryk kusajiliwa kwa pesa ndefu, bado hajaonyesha ubora wake Stamford Bridge, Potter akimchezesha akitokea benchini, tofauti na matarajio ya wengi.
Merson aliweka wazi kupitia kituo cha televisheni cha Sky Sports akidai kama Mudryk angesajiliwa na Potter basi angecheza kikosi cha kwanza.
“Mudryk anakaa benchi licha ya kusajiliwa kwa pesa ndefu, ni wazi tu si mchezaji wa Potter, kama angekuwa mchezaji wake asingekaa benchi, kuna utofauti mkubwa sana, nadhani bodi ndio ilihitaji saini yake na sio Potter,” alisema Merson
Vile vile mkongwe huyo alishangazwa na kipigo walichopata dhidi ya Tottenham wikiendi iliyopita kwenye mchezo wao mwingine wa Ligi Kuu England.
“Chelsea ilipofungwa dhidi ya Borussia Dortmund nikadhani watatoka na ushindi kipindi cha pili, sikuona kama walikuwa na uwezo wa kufunga mabao mawili, hivyo hivyo ilipokuwa dhidi ya Spurs, hawapo kiushindani kabisa, wanacheza kidhaifu mno, hawajitumi kabisa,” aliongeza.
Hata hivyo, Mudryk bado ana matuamini makubwa ya kufanikiwa kwenye ligi hiyo atakapotulia baada ya uhamisho wake kutoka Shakhtar.