Kiungo wa Yanga, Mudathir Yahaya, amesema Kocha Mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi, aliwataka wachezaji kutumia akili zaidi katika mchezo wao wa fainali ya Kombe la FA dhidi ya Azam FC ili kubeba taji hilo, imeelezwa.
Juzi Yanga ilifanikiwa kutetea ubingwa wa mashindano hayo kwa ushindi wa penalti 6-5 baada ya mchezo huo kumalizika kwa suluhu ndani ya dakika 120.
Mudathir alisema Gamondi aliwaambia wapinzani wao pia wamejiandaa vizuri kwa ajili ya fainali hiyo hivyo ni akili ya kila mchezaji ndio itaamua mechi.
Aliongeza Gamondi alifahamu mchezo huo usingekuwa mwepesi hivyo lazima nguvu za ziada za kupambana zihitajike.
"Mbali na maelekezo hayo ya kocha, lakini pia ubora wa kikosi chetu umesaidia kuchukua huu ubingwa, tumekuwa na kikosi bora na kila mchezaji yupo katika kiwango kikubwa,'" alisema kiungo wa Timu ya Taifa (Taifa Stars).
Aliongeza kwa wanaenda mapumziko na baadaye watarejea kujiandaa na msimu mpya wa mashindano ambayo pia wanahitaji kufikia malengo.
"Tunamshukuru Mungu msimu huu tumefanikiwa kile tulichokipanga, tumecheza robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika, tumetetea Kombe la Ligi Kuu na hili la FA, tunaenda kujipanga kwa ajili ya msimu ujao wa ligi na mshindano ya kimataifa," alisema Mudathir.