Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mudathir ana siri nzito Azam Complex

Mudathir Yahya Chamzi Goals Mudathir ana siri nzito Azam Complex

Fri, 9 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mabao stita, pointi tisa kwenye uwanja mmoja. Nani anaweza hiyo. Mudathir Yahya kafanya hivyo peke yake kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi akiwa na kikosi cha Yanga tangu ajiunge nayo msimu uliopita akitoka kuwa mchezaji huru.

Sasa kapachikwa jina 'Mfalme wa Chamazi', si kwa kubahatisha. Amefanya makubwa kwenye uwanja huo na tangu ligi irudi ameifungia Yanga mabao mawili katika uwanja huo (Azam Complex) na kuipa pointi sita muhimu ikiendelea kusalia kwenye usukani wa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikifikisha pointi 37 baada ya michezo 14.

Mechi ambazo aliipa Yanga pointi tisa ni dhidi ya Mashujaa FC akifunga bao la pili dakika ya 85 (juzi Alhamisi, Februari 8), Dodoma Jiji dakika 86 (Februari 5, 2024) na Namungo FC dakika 88 (Septemba 2023).   Ukiachana na mechi hizo, alifunga bao dakika ya 76 timu yake ikishinda mabao 5-0 dhidi ya KMC (Agosti 23, 2023) na msimu uliopita Yanga ikitangaza ubingwa kwenye uwanja huo, alifunga bao dakika 90+.

Hata hivyo, unajua siri ya mafanikio ya kiungo huyu wa zamani wa Azam FC kwenye uwanja huo?

Mudathir ambaye amekuwa akiwaadhibu makipa wa ligi kuu kwenye uwanja huo, anasema sababu kubwa ni 'Anaufahamu vizuri uwanja huo'.

"Naufahamu vizuri sana Uwanja wa Azam Complex, kabla ya kujiunga Yanga nimecheza Azam FC kwa muda mrefu."

Muda ni mmoja wa wachezaji ambao wanavifaidi viwanja walivyovizoea kama ilivyo kwa Azam Complex. iwe ameanza mechi au anatokea benchi, anasema kwake freshi tu na kutokana na kuujulia uwanja huo haoni shida kufunga.

"Nimefanya mazoezi hapo, nimecheza mechi hapo, sasa hakuna kitu kigeni sana kwangu, ukiachana na hilo kama nimeanzia benchi nakuwa naangalia kitu gani kinatakiwa pia nazingatia maelekezo ya kocha."

Unajua kupambana? Kiungo huyu wa kati fundi kweli kweli katika mambo yanayomfanya asikose nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga ni namna anavyopambana, hata mabao yake hayaji kirahisi na mbali na kuujulia na kuuzoea Uwanja wa Azam Complex, kujituma na kuipigania timu ndivyo kipaumbele vyake kuhakikisha timu inapata ushindi.

"Jambo lingine la msingi ni uzalendo kwa timu, sichezi pekee yangu tunacheza 11 kwa 11, lengo likiwa ni  kuhakikisha tunapata pointi tatu, ndio maana hata wachezaji wengine wamefunga kwenye uwanja huo." 

MAKIPA ALIOWAFUNGA Kipa wa Namungo FC, Deogratius Munishi 'Dida' alisema Mudathir ni mchezaji mwenye maamuzi ya haraka pindi anapoona kuna mwanya wa kufunga, pia kwenye Uwanja wa Azam Complex ni kama nyumbani kwao.

"Anajua anapiga wapi na kwa wakati gani, pia akiwa benchi anatulia kuusoma mchezo, ili akiingia anajua anafanya kitu gani, ameipa Yanga pointi dhidi yetu, maana ile mechi ilikuwa ngumu sana, akatufunga bao la jioni," alisema.

Kwa upande wa kipa wa KMC, Wilbol Maseke alisema "Kwenye mchezo wetu na Yanga, Mudathir alihusika na mipira mingi iliyozaa mabao na kwangu ndiye alikuwa nyota wa mchezo,pia anajua vipimo vya uwanja huo kacheza kwa muda mrefu akiwa na Azam FC."

Mbali na makipa hao, straika wa zamani wa Yanga, Mohamed Hussein 'Mmachinga' alisema, "Mudathir anatoa somo kwa wachezaji wanapokuwa benchi, akili zao kuwa uwanjani, ili wanapoingia wanakuwa wanakwenda kutibu tatizo."

Wakati staa wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel mtazamo wake anaona tayari wapinzani wakimuona Mudathir kwenye uwanja huo, wanakuwa hawajiamini.

"Wakati mwingine saikolojia zinakuwa zimeathirika ni faida kwa Mudathir kujijengea jina lake ndani ya uwanjani huo, ila makipa wanapaswa kumsoma zaidi ili na wao wajue jinsi ya kuokoa mashuti yake," alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live