Kiungo wa Yanga, Mudathir Yahya Abbas amesema sababu ya kushangilia kwa kusimama kwenye moja ya nguzo zilizopo katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi ilikuwa ni kuonyesha kuwa yeye amekulia Azam FC kisoka kwa hiyo uwanja ule ni kama nyumbani kwao.
Mudathir aliweka pozi hilo la kushangilia mara baada ya kufunga bao la nne na la ushindi dhidi ya Dodoma Jiji na kuisaidia timu yake ya Yanga kushinda ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Katika mchezo huo, uliopigwa Jumamosi iliyopita, Yanga walishinda bao 4-2 huku Mudathir akifunga mabao mawili katika mchezo huo muhimu na kumfanya aingie kwenye historia muhimu ya klabu hiyo kongwe Barani Afrika.
“Kushangilia vile ilikuwa kwenye kichwa changu, nilisema nikifunga bao lazima niende nikapande pale inaashiria katika ule uwanja, mimi nimekulia Azam.
“Nilitoka Zanzibar nikaja kufanya majaribio Azam mwaka 2011, nikafanikiwa kubaki pale, kwa hiyo mimi naujua ule uwanja. Wakati nikiwa Timu B wachezaji wa Timu kubwa wakiwa likizo nilikuwa nashinda pale uwanjani, hata nilipopandishwa timu kubwa, saa 7 mchana nipo uwanjani.
“Hakuna mtu anayeweza kupanda pale, ama huamini mtu afunge bao akapande pale moja kwa moja. Kwa sababu pale pana kama waya mbili na waya mmoja umekatika. Ukitoka ghafla huwezi kupanda.
“Mimi nimepanda pale kuonyesha kwamba mimi nimekuwa hapa Azam, napajua wala sio kwamba kwa vile nimeondoka Azam nina ugomvi nao hapana. Hapa mimi ni nyumbani, najiona kama mfalme wa ule uwanja.
“Kuna watu wanaabudu mizimu, mimi nilikuwa nauabudu ule uwanja. Ukitoka chumbani kwangu uwanja uko pale. Nilikuwa naingia pale uwanjani napiga mashuti, sasa hivi sipigi mashuti.
“Nilipopewa ule mpira na Mayele niliwaza nikiunganisha shuti nikakosa itakuwa zogo kwa mashabiki, nikaamua kupiga tachi mbili nikauweka mpira kwenye mguu wangu sahihi wa kulia, nikaona beki anakuja ikabidi nimpinde, mpira ukakaa mguu wangu wa kushoto, kumuangalia kipa amehama na mimi, wakati naurudisha akahama tena, nikasema hapa naweka kidogo tu, chuma.
“Hii picha lazima niitengenezee fremu kubwa nikaiweke ndani kwangu na aliyeipiga nitamtafuta nimpe pesa yake ananidai huyu,” amesema Mudathir.