Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mudathir Yahaya ahofia hiki Yanga

Yahaya Mudathir Mudathir Yahaya ahofia hiki Yanga

Thu, 5 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kiungo mpya wa Yanga, Mudathir Yahya, amekisoma vema kikosi cha timu hiyo nakusema ana kazi kubwa ya kuonyesha kiwango kizuri ili kumshawishi Kocha Nasreddine Nabi kumpa nafasi katika kikosi cha kwanza.

Mudathir amesaini mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia Yanga na kuungana na kikosi cha timu hiyo moja kwa moja visiwani Zanzibar, kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea katika Uwanja wa Amaan.

Kiungo huyo mkabaji aliwahi kuichezea Azam FC kabla ya kuachana na miamba hiyo ya Chamazi katika usajili wa dirisha kubwa na kisha kujiunga na KMKM kwa ajili ya kufanya mazoezi kulinda kiwango chake.

Akizungumza na gazeti hili jana katika mazoezi yake ya kwanza na timu yake hiyo mpya kwenye Uwanja wa Mao visiwani hapa, Mudathir alisema amefurahi kuwa sehemu ya kikosi cha Yanga na anapaswa kuongeza juhudi mazoezini ili kuingia katika kikosi cha kwanza.

Alisema anatambua amesajiliwa katika timu yenye wachezaji wazuri na anakutana na ushindani mkubwa wa namba, hivyo anapaswa kujituma zaidi ili kutowaangusha waliomsajili.

"Ni kweli kocha Nabi, amependekeza usajili wangu, natakiwa kupambana na nina majukumu makubwa ya kuwashawishi benchi la ufundi kunipa nafasi katika kikosi cha kwanza, lazima nionyeshe kitu tofauti katika mazoezi," alisema Mudathir.

Alisema alipoondoka Azam FC alirejea kwao Zanzibar na kujiunga na timu ya KMKM kwa ajili ya kufanya mazoezi ili kulinda kiwango chake, hivyo kwa sasa yuko fiti na tayari kuitumikia Yanga muda wowote katika mechi.

Naye Ofisa Habari wa Yanga,  Ally Kamwe, alisema ujio wa nyota huyo ndani ya Yanga ni usajili wa ubingwa kwa sababu ni miongoni mwa wachezaji ambao kocha wao, Nabi  amependekeza.

"Benchi la ufundi limefanya tathmini kubwa ya mechi 19 za ligi tulizocheza na kuona tunahitaji mtu kama Mudathir atakayekuja kuongeza nguvu kikosini na kufanikiwa katika malengo yetu ikiwamo kutetea taji letu la ubingwa," alisema Kamwe.

Yanga imeboresha kikosi chake katika usajili wa dirisha dogo kwa ajili ya kujiandaa na raundi ya 20 ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho Afrika.

Mudathir atakuwa na kibarua kigumu cha kuwania namba sambamba na viungo wawili mahiri wa Yanga, Khalid Aucho na Salum Abubakar Sure Boy, ambao wamekuwa na kiwango kizuri katika timu hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live