Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muda wa kurekebisha viwanja vya kuchezea Ligi Kuu ni sasa

Wanyarwanda Wafurahishwa Na Ukarabati Wa Uwanja Wa Michezo Muda wa kurekebisha viwanja vya kuchezea Ligi Kuu ni sasa

Mon, 29 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara imetolewa, ambapo Agosti 16, mwaka huu, kinyang'anyiro hicho cha kusaka ufalme wa soka nchini kwa msimu wa 2024/25 kitaanza rasmi.

Timu kwa sasa zipo kwenye maandalizi ya msimu mpya (pre seasons), zilijiandaa na mbio hizo za msimu mzima, ambazo mbali na kusaka ubingwa zitakuwa zikiwania nafasi nne ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa.

Hiyo ni kutokana na viwango vya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), Tanzania inaruhusiwa timu nne kucheza michuano ya kimataifa, hivyo zitakazoshika nafasi hizo za juu, zitacheza michuano hiyo, mbili Ligi ya Mabingwa na idadi kama hiyo Kombe la Shirikisho.

Hata hivyo, atakayeshika nafasi ya nne anaweza asicheze Shirikisho, kama bingwa wa Kombe la FA hatotokana na timu tatu zinazomaliza nafasi za juu kwenye Ligi Kuu.

Hivyo kuelekea msimu mpya tunaamini pia waamuzi nao watakuwa wanajinoa ili kuchezesha kwa haki mechi hizo ambazo kwa mara ya kwanza baadhi ya michezo itakuwa na Video ya Kumsaidia Mwamuzi, VAR.

Wakati maandalizi hayo yakiendelea kwa kila idara, rai yetu pia ni kuona wamiliki wa viwanja wakiendelea kuviboresha ili viweze kuwafanya wachezaji kuonyesha vipaji vyao halisi.

Lakini pia waelekeza nguvu zao kuviboresha zaidi kwani viwanja bora huvutia mashabiki kwenda kutazama soka na kuwapa burudani ya kutosha wale wanaoangalia kwenye televisheni.

Ikumbukwe pia hakuna watu wanaopata tabu kuangalia mpira kupitia televisheni halafu uwanja unakuwa mbovu, hautamaniki kabisa, hivyo uboreshwaji wa viwanja ni burudani kwa watazamaji wote lakini pia kutaongeza thamani kwenye ligi yetu ambayo inazidi kukua kila uchwao.

Huu sasa ni wakati wa kufanya marekebisho makubwa hasa upande wa nyasi ziwe za kijani na vipimo sahihi, pamoja na maeneo mengine ambayo huwa yanasahaulika sana kama kwenye vyumba vya kuvalia wachezaji na vyooni.

Tulimsikia Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Wallace Karia, akisema kuelekea msimu ujao watakuwa wakali sana kuhusu viwanja na akabainisha kama isipowezekana ni bora ligi ichezwe kwenye viwanja vichache kuliko kuipeleka katika viwanja vibovu.

Tuseme tu tunampongeza Karia kwani haiwezekani Ligi ya Tanzania ambayo inashika nafasi ya sita Afrika ichezwe kwenye viwanja vyenye ubora hafifu.

Pamoja na hayo kuna tabia ya wamiliki au mameneja wanatengeneza viwanja vinavyokuwa vizuri wakati ligi inaanza lakini baada ya mechi tatu havitamaniki.

Na hii ni kwa sababu ya kuruhusu mechi nyingi za mashindano ya vikombe, pamoja na timu za mkoa husika kufanya mazoezi katika viwanja hivyo.

Tunashauri mameneja kupiga marufuku viwanja hivyo kutumiwa kwenye mazoezi mara kwa mara, badala yake vitumike katika ligi na michezo mikubwa tu hususan za Ligi Kuu na Ligi za Chanpionship, pia zinaweza kufanya mazoezi kwenye viwanja vingine.

Kuchezwa mechi mbili au tatu, halafu timu zinahama uwanja ni kutowatendea haki mashabiki wa mkoa husika wakiwamo wafanyabiashara, lakini pia kuhama kwa timu mwenyeji kunaipotezea mapato mengi kwa kuwa haiwezi kupata mashabiki wengi uwanjani ikiwa ugenini.

Hasa ikizingatiwa kwa mujibu wa Kanuni za Ligi Kuu Bara, timu mwenyeji ndiyo inachukuwa mapato yote ya mlangoni katika mechi husika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live