Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtumbuka, mkali wa gesi anayemzimia Maxi Nzengeli

Arduyfys Mtumbuka, mkali wa gesi anayemzimia Maxi Nzengeli

Fri, 12 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Nyota ya Emmanuel Mtumbuka inaendelea kung’ara baada ya kumwaga wino kuichezea timu ya Ligi Kuu Bara, Mashujaa FC ya mkoani Kigoma.

Mashujaa imemsajili mshambuliaji huyo kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Stand United inayoshiriki Ligi ya Championship.

Akiwa Stand United, Mtumbuka amefunga mabao saba na kutoa pasi tano za mwisho zilizozaa mabao kwenye mechi 12 alizocheza.

Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, Mtumbuka amezungumzia mambo mbalimbali huku akimtaja Ulimboka Mwakingwe (mchezaji wa zamani wa Simba) na Maxi Nzengeli wa Yanga kuwa ndio mastaa anaowakubali.

“Nilivutiwa na Ulimboka kutokana na umahiri wake wa kucheza pia alikuwa ni mchezaji anayezungumziwa na kila mtu, nikajikuta natamani kupata umaarufu kama wake kupitia soka.

“Hivyo niliingia kwenye soka baada ya kuvutiwa naye lakini kwasasa namtazama zaidi Maxi, ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa anajua kuuchezea mpira anaufanya uonekane rahisi,” anasema.

Anasema ubora wa kiungo huyo wa Yanga umekuwa ukimfanya ajifunze mambo mengi kutoka kwake kwani ni mchezaji ambaye amekuwa akimtazama sana kwa sasa.

MTAALAM WA MAFUTA NA GESI

Licha ya kuwekeza nguvu kwenye soka mambo yake kielimu yalikwenda sawa kama wazazi wake walivyokuwa wanataka hii ni baada ya kumaliza elimu ya sekondari na kupata Diploma ya Mafuta na Gesi.

“Wazazi wangu walikuwa hawapendi nicheze soka, walitaka nguvu zangu zote niwekeze kwenye elimu nashukuru Mungu huko pia nilikuwa vizuri kwani nimehitimu elimu ya sekondari na kwenda chuo ambapo nimepata diploma ya mafuta na gesi.

“Baada ya kufanya kile wazazi wangu walichokuwa wanatamani kuona mwanao nafanya walikuwa upande wangu na kunipa ushirikiano kwaajili ya kuendeleza kipaji changu,” anasema.

USHINDANI, UKATA

Wachezaji waliofanikiwa kucheza Ligi Kuu na kushuka madaraja ya chini wamekuwa wakifunguka suala la ushindani sambamba na ukata wa mshahara kwa wakati na wakati mwingine kukosa kabisa kama anavyothibitisha Mtumbuka.

“Championship kwanza kuna ushindani mkali baina ya wachezaji na wachezaji, pia timu na timu lakini kule inahitaji kujitolea zaidi ili kuendeleza kipaji chako kwani hali ya kiuchumi ni mbaya nilikuwa nacheza bila kulipwa.

“Kitu kizuri kutoka huko ni kucheza kwa uwezo kwani huwezi kupata nafasi ya kucheza kama huna uwezo kutokana na ushindani uliopo ikiwa ni pamoja na kujijenga kwa ubora na kuwa mchezaji mkubwa,” anasema Mtumbuka

SIO SOKA TU HADI KILIMO

Wakati wachezaji wengi wakiwekeza nguvu kwenye soka kuhakikisha wanajijengea heshima kwa kulinda ubora wao ni tofauti upande wa mshambuliaji huyo ambaye amesema licha ya kuamini katika kipaji amewekeza nguvu kwenye kilimo.

“Mpira wa miguu una muda, unaweza kuwa bora kipindi fulani na kukubalika na kila kocha na baada ya hapo umri kadiri unavyozidi kwenda unaweza kupoteza ubora nimeamua kujiandaa mapema kuwezeka kwenye kilimo.

“Nalima mpunga, matikiti na nyanya kutokana na msimu nashukuru Mungu uwekezaji wangu huko umekuwa ukinisaidia hasa kipindi ambacho nilikuwa timu ya daraja la chini ambayo ilikuwa inalipa mshahara kwa kusuasua na wakati mwingine kukosa kabisa.”

KILICHOMNG’OA SIMBA HIKI

Wadau wa soka hasa mashabiki wa Simba jina la Mtumbuka si geni kwao kutokana na kipaji chake kukuzwa na timu yao ya vijana hadi kupandishwa timu ya wakubwa lakini hakupata nafasi ya kucheza.

“Nimekuzwa timu ya vijana, nilipata bahati ya kupandishwa timu ya wakubwa msimu wa 2015/16 lakini sikupata bahati ya kucheza mchezo hata mmoja kutokana na kuumia mguu tukiwa kambini Kisiwani Zanzibar.

“Nakumbuka nilikaa nje ya uwanja bila kujihusisha na mpira msimu mzima na huo ndio ulikuwa mwisho wangu wa kucheza Simba kwani nilipotea msimu mzima na mkataba ulimalizika nikaanza maisha mengine nje ya timu huyo,” anasema mshambuliaji huyo ambaye amecheza timu sita tofauti hadi sasa African Sports, Mawenzi, Dodoma Jiji, Fountain Gate, Stand United, Mbao, Simba na sasa Mashujaa.

BOCCO NI MMOJA TU

Tanzania imebarikiwa kuwa na washambuliaji wengi ambao wamefanya makubwa lakini hakuna aliyemfikia John Bocco hivyo ndivyo anavyosema Mtumbuka akimzungumzia nahodha huyo wa Simba.

“Washambuliaji wengi wamekuwa bora kwa nyakati zao lakini kwa Bocco hakuna mshindani kwani yeye ni bora nyakati zote anaweza akapotea leo lakini kesho anaibuka na misimu yote lazima afunge.

“Lakini ukifuatilia washambuliaji wengi wazawa wao wakifanya vizuri msimu huu basi msimu unaofuata hawasikiki tena hili kwa Bocco halipo yeye anaweza asivunje rekodi yake lakini atazungumzwa kutokana na uwezo wake wa kufunga.”

Bocco ukiachana na kucheza katika michuano ya madaraja ya chini na kuipandisha Azam FC msimu wa 2008/09, amecheza misimu 16 akiwa amefunga jumla ya mabao 153 huku akiwa amechezea timu mbili pekee, Azam FC na Simba hadi sasa.

Mtumbuka anasema mipango yake ni kuifanya vizuri Mashujaa kwa kushirikiana na wachezaji wenzake.

“Tunataka tushike nafasi za juu kwenye Ligi Kuu,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live