Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtoto wa Nabi awalipua marefa Ligi Kuu

Mtoto Nabi Pic Mtoto wa Nabi awalipua marefa Ligi Kuu

Mon, 5 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha wa Yanga jana Jumapili alianza kuitumikia adhabu yake ya pili ya kusimamishwa kufuatia kuwatolea lugha chafu waamuzi kwenye mchezo dhidi ya Ihefu lakini mwanaye wa kiume amemtetea baba yake akidai kwa anachokiona makocha kibao watafungiwa tu.

Hedi Nabi ambaye anaifuatilia Ligi Kuu Bara kwa ukaribu kupitia mtandaoni moja kwa moja akiwa kwao Ubelgiji ameliambia Mwanaspoti bado anashangaa imekuwaje baba yake anafungiwa mechi tatu hali ya kuwa alishaadhibiwa palepale uwanjani.

Hedi alisema aliongea na baba yake mara baada ya mpira kumalizika ambapo alipomuona anakimbilia vyumbani aliwafuata waamuzi hao na kuwaomba radhi kwa yote yaliyotokea.

“Sijajua kwa nini wamemfungia bado tunashangaa na hata yeye (Nabi) anashangaa tulipomuona anakimbilia vyumbani tulishtuka lakini tulipoongea naye akatuambia alikwenda kuwashukuru na wala hakutoa lugha kali lakini baadaye akaona wamemfungia,”alieleza Hedi.

“Unajua makocha wanaadhibiwa kila sehemu tunaona hata huku Ulaya wanaadhibiwa hakuna shida kama mtu anafanya makosa lakini unaona kocha anapewa kadi palepale uwanjani na bado baadaye anafungiwa kwa kusikiliza upande mmoja pekee, bila hata kutakiwa kujieleza, hii nimeiona Tanzania pekee.

“Tuliona hivi karibuni Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp, alifanya makosa lakini kwanza akatakiwa kujieleza na baadaye akaadhibiwa huo ndio ustaarabu wa kutoa haki lakini bado ni changamoto kwa kuona haki Tanzania.

Aidha Hedi alisema makocha wengi watafungiwa kutokana na makosa mengi ya waamuzi ambapo kwa klabu zenye presha kubwa ni vigumu makocha kuvumilia.

Alisema changamoto nyingine anayoiona waamuzi wanatakiwa kujifunza lugha mbalimbali hasa Kiingereza kutokana na kutafsiri wametolewa lugha mbaya hali ya kuwa ni tofauti.

“Niliangalia mechi ya Ihefu vizuri tu unaona mwamuzi anaitwa na mwamuzi wa mezani anaambiwa na kwenda kutoa kadi haraka na kukimbia, nafikiri wanaoendesha ligi wanaweza kuona yule mwamuzi hakuwa anajiamini.

“Nafahamu kuna shida ya waamuzi kutumia kanuni hizo vibaya lakini wanapaswa kutibu kiini cha tatizo, kusema ukweli hata kama kuna makosa ya kibinadamu lakini Tanzania yanachosha. Kuna vitu vya wazi kabisa kila mtu anaviona bila hata kupata msaada wa marudio kupitia video lakini unakuta mwamuzi anaamua vingine.

“Nadhani makocha wanatakiwa kuthaminika kwanza kuhakikisha waamuzi wanaopewa hizi mechi ni watu sahihi waliofaulu na kumudu kuchezesha mechi, vinginevyo waamuzi wataendelea kufungiwa sana.”

Nabi amefungiwa mechi tatu adhabu iliyotolewa na kamati ya usimamizi na uendeshaji wa ligi iliyotolewa juzi na Bodi ya Ligi Tanzania.

Adhabu hiyo ni ya pili kwa Nabi tangu atue nchini kuanza kuifundisha Yanga ambapo pia msimu uliopita alipewa adhabu kama hiyo.

Chanzo: Mwanaspoti