Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtoko wa kila kocha atakapotua Nou Camp

Mtokooooo Mtoko wa kila kocha atakapotua Nou Camp

Wed, 31 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kwenye kauli iliyoshtua wengi, Xavi amethibitisha ataachia ngazi mwishoni mwa msimu huu kwenye kibarua cha kuinoa Barcelona.Pengine hilo limempa ujasiri baada ya uamuzi wa Jurgen Klopp kutangaza ataachana na Liverpool mwishoni mwa msimu huu pia.

Matokeo yasiyoridhisha ndiyo yanayomsukuma Xavi ajiondoe mwenyewe kwenye kibarua cha kuinoa Barcelona. Gwiji huyo wa Nou Camp alikabidhiwa mikoba ya kuinoa timu hiyo Novemba 2021.

Msimu wake wa kwanza ulikuwa mtamu, ambapo aliongoza ligi kwa tofauti ya pointi 10 na kunyakua taji la La Liga katika kipindi ambacho Barca imekuwa na ukata mkubwa wa kifedha.

Msimu huu mambo si mambo, Barca imeachwa mbali na timu inayoongoza msimamo wa La Liga, pointi zisizopungua 11.

Kipigo cha mabao 5-3 kutoka kwa Villarreal wikiendi iliyopita ndicho kilichotibua zaidi, maana Barcelona ilikuwa mbele kwa mabao 3-2 hadi dakika 10 za mwisho, kabla ya mambo kutibuka na kupoteza mechi.

Baada ya tangazo hilo la Xavi, makocha wengi sasa wameanza kuhusishwa na kibarua hicho cha Nou Camp.

Lakini, makocha hao watakapofika Barcelona na kukabidhiwa mikoba ya kuinoa timu hiyo, watafanya nini? Watakuja na mtoko gani?

Mikel Arteta

Moja ya jina ambalo limekuwa likitajwa sana na kuhusishwa na kibarua cha kuinoa Barcelona ni Mikel Arteta. Staa huyo wa zamani wa Barca, Arteta amejitengeneza na kuwa kocha mahiri, huku akijifunza mengi kutoka kwa fundi Pep Guardiola.

Arteta alikuwa chini ya Guardiola huko Manchester City kabla ya kukabidhiwa mikoba ya kuinoa Arsenal, ambayo ameibadili na kuifanya kuwa moja ya timu inayoshindania ubingwa kwenye Ligi Kuu England. Mtindo wa kiuchezaji wa Xavi hauna tofauti na Arteta, licha ya kwamba Xavi mara kwa mara amekuwa akitumikia fomesheni ya 4-2-3-1 na Arteta 4-3-3. Kama ilivyo kwa Guardiola, Arteta anapenda kuwatumia mabeki wa pembeni kama viungo wa kati, timu yake inapokuwa na mpira.

Anaweza kufanya usajili wa mastaa wachache, lakini kama pesa itakuwa shida, Arteta anaweza kuendelea kuwatumia wachezaji waliopo na kikosi chake kikafanya kweli ndani ya uwanja na kuvuna matokeo matamu.

Rafael Marquez

Staa mwingine wa zamani wa Barcelona, Rafael Marquez. Huyu anaweza kufuata nyayo za Guardiola kwa maana ya kuibukia kwenye timu hiyo kutokea kwenye Barcelona B. Staa huyo wa Mexico mfumo wote wa Barca ni kama upo kwenye damu yake.

Akiwa sehemu ya kikosi cha Barcelona, Marquez anajaribu kuambukiza falsafa za timu hiyo kuanzia kwenye timu ya watoto, hivyo haitakuwa kazi kubwa kwake atakapoanza kukinoa kikosi cha wakubwa.

Mtindo wake wa kiuchezaji ni ule wa 4-3-3 unaofanana kabisa na Arteta na kwamba Marquez atapita kwenye nyayo za Xavi, ambapo atamtegemea Robert Lewandowski kuongoza safu yake ya ushambuliaji. Kwenye kiungo bila ya shaka atahitaji kuwa na huduma ya mchezaji mwenye uzoefu mkubwa kama Mjerumani, Ilkay Gundogan.

Jurgen Klopp

Itakuwa ngumu kupata huduma ya Jurgen Klopp mwishoni mwa msimu huu, lakini kama hilo litafanikiwa basi Barcelona itakuwa imenasa jembe le maana na pengine kuteseka kutakwisha.

Klopp ataachana na Liverpool mwishoni mwa msimu huu, hivyo atakuwa sokoni. Mtindo wa kiuchezaji wa Klopp ni 4-3-3, lakini yeye staili yake ikiwa tofauti, ambapo amekuwa akitengeneza kikosi ambacho mabao yanafungwa kutokea kwa mawinga.

Klopp anaweza kufanana na Arteta kwenye uteuzi wa mshambuliaji wa kati, kwamba kuna uwezekano mkubwa akaanza na Roque badala ya Lewandowski kutokana na mikimbio ya mchezaji huyo, ambaye anaweza kuwa Mohamed Salah wa Barcelona.

Barcelona bado ina wachezaji wa kutosha wa kumpa Klopp uchaguzi wa kutosha wa kupanga kikosi chake na kupata matokeo matamu ndani ya uwanja na kuifanya timu hiyo kuwa tishio.

Mtindo wa Klopp pia amekuwa akiwatumia sana mabeki wa pembeni kutengeneza nafasi za mashambulizi na katika kikosi cha Barcelona wachezaji wa aina hiyo wapo wa kutosha, hatakuwa na shida yoyote.

Hansi Flick

Hansi Flick amekuwa hana kazi tangu alipoachana na timu ya taifa ya Ujerumani mwaka jana na sasa jina lake linahusishwa na mpango wa kutua Barcelona.

Licha ya mara kadhaa kutumia mtindo wa kutumia mabeki wa kati wa tatu, Flick mfumo wake pendwa ni 4-2-3-1, ambao kwa wachezaji waliopo kwenye kikosi cha Barcelona ni kitu walichozoea kukifanya mara kwa mara uwanjani. Kwenye kikosi cha Barca kuna wachezaji makini kama Pedri, ambao wanampa kocha uhakika wa kutosha kwenye sehemu ya kiungo Namba 10.

Xavi alipokuwa akicheza fomesheni ya 4-2-3-1, amekuwa akitumia huduma ya Pedri kwenye Namba 10, kitu ambacho Flick anaweza kukiiga huku kwenye kiungo akitoa nafasi kwa wakali kama Gundogan na De Jong kutawala kwenye eneo hilo, wakicheza pacha huku wakimruhusu Pedri kuwa na kazi moja tu ya kuwa kiunganisha cha viungo na washambuliaji.

Jose Mourinho

Jose Mourinho aliwahi kuwa Barcelona kwa miaka minne alipokuwa mkalimani wa kocha Bobby Robson na baadaye Louis van Gaal, ambapo alijifunza mengi kupitia kwa makocha hao.

Lakini, hana ugeni pia na soka la Hispania, kwani aliwahi kuinoa Real Madrid, timu hamasimu wa Barcelona na alifanya mashabiki wa timu hizo kuwa maadui.

Wakati Mourinho alipokuwa Real Madrid, mechi zao na Barcelona ilikuw akama vita. Lakini, sasa akiwa hana kazi, anaweza kuvutiwa na kibarua cha kwenda kuinoa Barcelona, ambayo pia itafurahi kuwa na huduma ya kocha mwenye mbinu za kutosha za kubeba mataji.

Mourinho alipokuwa AS Roma alikuwa akitumia fomesheni mbili, kama sio 3-5-2 basi 3-4-2-1 na hilo haliwezi kuwa tatizo atakapokwenda Barcelona, kwa sababu kwenye timu hiyo kuna wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kumudu mtindo wake wa kiuchezaji.

Hata ile aina ya wachezaji wapiga kazi nzito ambao Mourinho amekuwa akiwataka kwenye kikosi cha Barca wapo akiwamo Gundogan, huku staa kama Pedri na Gabi wakiwa na uhakika mkubwa wa kupata nafasi kwenye fomesheni ya 3-4-2-1, wakicheza nyuma ya mshambuliaji Lewandowski au Roque.

Chanzo: Mwanaspoti