Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtoko wa KenGold twenzetu Ligi Kuu Bara

Kengold Pic Mtoko wa KenGold twenzetu Ligi Kuu Bara

Sun, 21 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati Ken Gold ikishuka uwanjani leo Jumapili dhidi ya FGA Talents, Jiji la Mbeya litasimama kwa muda kushangilia historia ya mafanikio kwa timu hiyo kupanda Ligi Kuu.

Hii ni baada ya kudumu misimu minne mfululizo wakiisaka ladha ya Ligi Kuu bila mafanikio, lakini hatimaye ndoto imetimia ambapo wadau na mashabiki wa soka itakuwa ni furaha isiyo ya kifani.

Ikumbukwe kuwa msimu uliopita Mbeya ilikuwa na timu tatu za Ligi Kuu, lakini ilijikuta ikipoteza moja - Mbeya City iliyoshuka daraja kupitia mchujo ikitolewa na Mashujaa kwa jumla ya mabao 3-1.

Hata hivyo, hadi sasa ni Tanzania Prisons pekee waliosalia Ligi Kuu kufuatia Ihefu kuuzwa na kuhamishiwa mkoani Singida.

Leo mashabiki jijini hapa wataamua wao kuingia uwanjani na suti za aina moja ikiwa ni ishara ya kuiunga mkono timu hiyo itakapotangazwa kupanda Ligi Kuu.

HESABU ZILIVYO

Hadi sasa Ken Gold ndio vinara wa Championship kwa pointi 64, ambapo wamebakiza michezo miwili yote wakicheza Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya ambapo pointi mbili tu zinatosha kupanda.

Katika mechi hizo iwapo leo itashinda itafikisha pointi 67, ambapo ni rasmi zitairuhusu kucheza Ligi Kuu msimu ujao, kwani kati ya timu nne zinazowania kupanda ni moja tu yenye kufikisha alama hizo.

Timu zinazopambania kucheza Ligi Kuu msimu ujao ni Pamba Jiji walio nafasi ya pili kwa alama 61, ambapo kama watashinda michezo miwili dhidi ya TMA na Mbuni huko Arusha watafikisha pointi 67.

Kwa upande wa Biashara United na Mbeya Kwanza iwapo watashinda michezo miwili iliyobaki wataishia alama 65, hivyo kuifanya KenGold kutangaza kupanda Ligi Kuu.

Kama haitoshi, KenGold inao uhakika wa kupanda daraja kwani rekodi zake ikiwa Sokoine haijapoteza mchezo wowote zaidi ya sare tatu dhidi ya Stand United, Pamba Jiji na Mbeya Kwanza.

Pia timu hiyo ya wilayani Chunya ndio imekuwa na rekodi tamu hadi sasa ikipoteza idadi ndogo ya mechi mbili tu, ikifungwa jijini Mwanza na Pamba Jiji, kisha kulazwa na Mbeya Kwanza kule Mtwara.

HISTORIA YAO

KenGold haijashiriki ligi ya wilaya, mkoa, ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) na First League isipokuwa ilibadilishwa jina kutoka Gipco FC iliyokuwa mkoani Geita baada ya kuuzwa kwa wachimba dhahabu wa Chunya. Gipco iliyokuwa Daraja la Kwanza msimu huo (kwa sasa Championship), ilimaliza nafasi ya tano ambapo ilidaiwa kukosa gharama za uendeshaji na kuuzwa. Makubaliano ya pande zote yalifanyika baada ya kumalizika msimu wa 2019/20 na kuhamishiwa Mbeya huku makao yake yakiwa wilayani Chunya. Kuanzia msimu wa 2020/21 timu hiyo ilitumia Uwanja wa Sokoine Mbeya kwa mechi zote za nyumbani, ambapo kwa sasa ni miaka minne tangu imilikiwe na uongozi mpya.

KIUCHUMI

Timu hii sio mali ya wanachama, bali inamilikiwa na mtu binafsi mwenye vyanzo vyake vya mapato ikiwa ni shule na machimbo ya dhahabu vilivyopo Chunya.

Mmiliki wa timu hiyo, Kenneth Mwambungu siyo mzungumzaji sana na huenda ukapishana naye njiani bila kujua kama ndiye bosi kutokana na maisha aliyochagua.

Hata jina KenGold inatafsiri jina lake ikimaanisha Kenneth na Gold ikimaanisha shughuli zake za uchimbaji madini na kutengeneza muunganiko wa KenGold.

Pia mbali na uchimbaji, timu hiyo inategemea mapato mengine kutoka kwenye shule za Ken Gold zilizopo wilayani humo, lakini habari za ndani zinaeleza kuwa wapo pia vigogo wanaoipa nguvu.

KAZI IPO LEO

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Jumanne Challe anasema walichelewa muda mrefu kukamilisha kazi, hivyo leo ndio wanahitimisha shughuli akisema hawataki kufanya makosa.

Challe anaongeza kuwa anataka kurejea rekodi yake ya kuzipandisha timu Ligi Kuu ikiwamo African Lyon, RTC Kagera na Singida United akiwa na Fredi Felix ‘Minziro’.

Kocha huyo anaeleza kuwa baada ya misimu minne ya jasho sasa kazi inapaswa kuisha leo dhidi ya FGA Talents akiwaomba mashabiki na wadau wa Mbeya kutinga suti.

“Naweza kuwaruhusu mashabiki waje na suti zao, hatufanyi makosa, kama tumeshinda zote tutakwamaje leo..vijana wapo fiti na tunasubiri mechi hiyo ili kuandika historia,” anasema kocha huyo.

Katibu Mkuu wa timu hiyo, Benson Mkocha anasema wataandaa jezi maalumu za kujipongeza kupanda Ligi Kuu kabla ya suti ya mchezo wao wa mwisho kumaliza vinara wa ligi.

Anasema haikuwa kazi nyepesi kupenya kutokana na upinzani walioupata kwenye championship, akieleza kuwa umoja, mshikamano na kujituma kwa wachezaji ndio imewapa mafanikio hayo.

“Tunajua ligi haijaisha lakini kwa maandalizi na ubora wa timu tunayo matumaini kuwa mchezo ujao tutashinda ili kujihakikishia kucheza Ligi Kuu na uongozi tumeandaa jezi maalumu.

“Hatuishii kupanda Ligi Kuu tunataka kumaliza vinara wa ligi kwani pointi 67 zinaweza kufikiwa na Pamba Jiji kama watashinda mechi zote, hivyo tunataka alama tatu za Polisi Tanzania mechi ya mwsho,” anasema Mkocha.

Staa wa timu hiyo na kinara wa mabao wa Ligi ya Championship, Willy Edgar anasema licha ya mipango ya kupandisha tena timu baada ya kufanya hivyo kwa Mbeya Kwanza, anasaka heshima ya kiatu cha mfungaji bora wa ligi.

Anasema pamoja na ushindani wa tuzo hiyo kuwa mkali, lakini kasi yake haitaisha bali kuhakikisha mechi zilizobaki anaendelea kutupia ili kufikia malengo yake.

“Kwa sasa hesabu ni moja kwanza, kupandisha timu kisha kuangalia uwezekano wa kubeba ufungaji bora, yote haya yanawezekana kwani tupo kwenye mipango mizuri,” anasema winga huyo kinara wa mabao 20.

MECHI NYINGINE

Ukiachana na mechi hiyo, leo pia kuna michezo mingine ambapo TMA itaikaribisha Pamba jijini Arusha, Pan Africans ni wenyeji wa Biashara United na Mbeya Kwanza dhidi ya Green Warriors. Polisi Tanzania watawaalika Mbeya City, Mbuni wakiwavaa Copco, Cosmopolitan dhidi ya Stand United na Ruvu Shooting ambao wameshashuka daraja wakiwapokea Transit Camp.

Chanzo: Mwanaspoti