Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtihani wa Simba, Yanga kucheza kombe la Dunia 2025

Kumekucha Mapinduzi Cup! Simba, Yanga Ndani! Mtihani wa Simba, Yanga kucheza kombe la Dunia 2025

Wed, 20 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Miamba ya soka nchini, Simba na Yanga ni miongoni mwa timu kutoka Afrika zenye nafasi ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia la Klabu zitakazofanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2025, Marekani baada ya kufanyiwa marekebisho na itashirikisha timu 32.

Shirikisho la Soka duniani (Fifa) lilitangaza rasmi Jumapili iliyopita ujio wa michuano hiyo na itaanza Juni hadi Julai na imetolewa ufafanuzi wa namna itakavyokuwa.

TIMU ZINAVYOFUZU

Kwa mujibu wa taarifa ya namna timu zinavyotakiwa kufuzu michuano hiyo, kuna njia mbili, kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Afika na kukusanya pointi za kukuwezesha kufuzu kwa michuano hiyo.

Kwa upande wa Simba na Yanga, ili zijikatie tiketi hiyo, ni lazima zitumie njia hizo ili zikakutane na miamba ya soka duniani kama Bayern Munich, Chelsea, Real Madrid na Manchester City.

Kwa upande wa kukusanya pointi, itaangaliwa yenye nyingi zaidi kwenye michuano ya kimataifa hali itakayoifanya kuwa katika nafasi za juu kwenye viwango vya ubora vya Caf na hadi sasa Simba ipo nafasi ya tisa na pointi 35 huku Yanga yenyewe ikiwa nafasi ya 18 na pointi 20.

Simba iliyi kwenye nafasi za juu zaidi kwa viwango vya ubora kwa timu za Tanzania kwenye michuano ya kimataifa, inatakiwa kuzishusha CR Belouizdad (36), RS Berkane (37), Zamalek (39), Raja Casablanca (51), Mamelodi Sundowns (51) na Espérance de Tunis (56), huku Al Ahly na Wydad Casablanca zenyewe tayari zimefuzu kwa michuano hiyo.

NAMNA ILIVYO

Mashindano hayo yatakayokuwa yakifanyika kila baada ya miaka minne, yatakuwa yakichezwa kwa mfumo wa makundi (8) yenye timu nne kila moja, na mbili za juu kila kundi zitafuzu hatua ya mtoano, muundo sawa na wa Kombe la Dunia la timu za taifa.

Hii ina maana, kuanzishwa kwa mfumo huu, utasitisha unaotumika wa sasa na umekuwa ukifanyika kila mwaka kwa kushirikisha timu saba.

Kwa mujibu wa taarifa, Ulaya itakuwa na timu 12, Amerika Kusini sita, huku Afrika, Asia na Amerika Kaskazini zitakuwa na timu nne kila moja. Oceania au Australia ina nafasi moja, wakati nafasi ya mwisho itatolewa kwa klabu kutoka nchi mwenyeji.

VIGEZO

Kiwango cha timu kwa miaka minne ni miongoni mwa sifa itakayotumika katika mchakato wa kupata washiriki kwa ajili ya fainali hizo.

Ulaya, mfumo wa UEFA wa uwiano wa klabu utatumika, timu zikipata pointi mbili kwa ushindi, pointi moja kwa sare, pointi nne za kufuzu kwa hatua ya makundi, pointi tano za kufuzu hatua ya 16 bora na pointi moja ya kusonga mbele kila hatua ya mashindano baada ya hapo.

Mabingwa wa mabara kuanzia 2021-2024 zinatiketi ya kucheza Kombe la Dunia la klabu, kumaanisha Chelsea, Real Madrid na washindi wa Ligi ya Mabingwa wa msimu uliopita Manchester City wamefuzu kutoka Ulaya.

Timu nyingine za Ulaya ambazo zimefuzu kulingana na mfumo wa pointi ni Bayern Munich, Paris St Germain, Inter Milan, FC Porto na Benfica.

Timu mbili tu kutoka nchi moja zinaweza kufuzu kwa mashindano isipokuwa kwa itakayobeba ubingwa wa bara lake. Kwa mfano, kwa kuwa Chelsea na City wamefuzu kutoka Uingereza, Arsenal wanaweza kufuzu iwapo tu watashinda Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

Kutoka Amerika Kusini, timu za Brazil Palmeiras, Flamengo na Fluminense zimefuzu kama mabingwa wa Copa Libertadores, huku timu za Asia Al Hilal na Urawa Red Diamonds pia zikifuzu.

Al Ahly na Wydad vile vile zimefuzu kutoka Afrika huku Monterrey, Seattle Sounders na Club Leon zikitoka Amerika Kaskazini.

Auckland City ya Oceania imefanikiwa kusonga mbele kutokana na idadi kubwa ya pointi walizonazo.

POINTI ZENYEWE

CAF iliidhinisha vigezo vya msingi katika upimaji wa viwango vya ubora wa timu katika Karne ya 20 mwaka 2000 kwa kutoa pointi mwaka 2003.

Hili liliboreshwa mwaka 2005 kwa kuongezwa kigezo cha kuwazawadia pointi klabu zinazotinga nusu fainali ya Kombe la Dunia upande wa klabu. Mbinu hii pia imetumika kutengeneza viwango vya wakati wote kwa klabu za CAF na kuongeza pointi ambazo zilikuwa zikikusanywa tangu mwaka 1965.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live