Wakati Ihefu ikishuka uwanjani leo Jumatano kuwakabili Singida Big Stars, mtihani mkubwa utakuwa kwa kocha wao mkuu, Moses Basena kusaka ushindi wake wa kwanza Ligi Kuu.
Basena raia wa Uganda alitambulishwa hivi karibuni kuchukua mikoba ya mtangulizi wake, Zuberi Katwila ambaye kwa sasa anakinoa kikosi cha Mtibwa Sugar na tayari ameanza kazi kwa kishindo.
Kocha huyo aliyewahi kuiongoza Simba mwaka 2011, tayari amesimamia michezo miwili akianza na Coastal Union nyumbani kwa suluhu kisha kuchapwa 2-1 dhidi ya Simba.
Katika mechi hizo alizosimamia kocha huyo Ihefu imeruhusu mabao mawili na kufunga moja na kumfanya leo kuumiza kichwa kuongeza idadi ya mabao, lakini kutoruhusu wavu wake kuguswa.
Timu hizo zinakutana uwanja wa CCM Liti ikiwa kila upande umetoka kuchezea kipigo na Singida BS ililazwa mabao 2-0 dhidi ya Yanga, huku Ihefu ikifa 2-1 mbele ya Simba na sasa kila upande unahitaji ushindi kufuta maumivu.
Hadi sasa Singida BS wapo nafasi ya 10 kwa pointi nane, huku wapinzani wakiwa nafasi ya 11 kwa alama saba baada ya timu zote kushuka uwanjani mara saba.
Basena alisema, “Tunajua mechi haitakuwa rahisi lakini tumejipanga kushinda, makosa yaliyoonekana mechi zilizopita tumeyafanyia kazi, kimsingi ni vijana kufuata maelekezo ili kufikia malengo,” alisema.