Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtibwa yawadunda wababe wa Simba

Mitbwaaaaaaaaa Mtibwa yawadunda wababe wa Simba

Sat, 9 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu Bara, Mtibwa Sugar inaendelea kujitafuta mdogomdogo baada ya jioni hii kuifumua Tanzania Prisons kwa mabao 2-1, iliyotoka kuinyoosha Simba katika mechi iliyopita ya ligi hiyo.

Prisons iliyoitungua Simba kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini hapa katika pambano la leo lililopigwa Uwanja wa Manungu Complex ilishindwa kabisa kuonyesha lile soka ililopiga Jumatano ilipomkimbiza Mnyama huku wenyeji wakionekana kupania mchezo huo.

Licha ya mashambulizi makali kwa timu zote na kuwepo kwa kosa kosa, hakuna timu iliyofanikiwa bao mapema hadi sekunde chache kabla ya mapumziko wakati maafande wa Magereza, walipopata bao la kuongoza lililowekwa kimiani na Benjamin Asukile.

Tangu mwanzo wa mchezo Mtibwa ilionekana kusaka ushindi kwani nyota wa timu hiyo walitengeneza nafasi nyingi lakini zilipotezwa ikiwamo ile ya mshambuliaji Charles Ilanfya aliposalia na kipa Yona Amos na kushindwa kukwamisha mpira nyavuni.

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko na kuongeza kasi ya mchezo na ilionekana kama Prisons ingeondoka na pointi zote tatu kabla ya Omary Marungu kufunga bao la kusawazisha dakika ya 85 na dakika tatu baadae, Rashid Seif Karihe alipigilia msumari wa mwisho uliowanyamazisha maafande akimalizia pasi ya Marungu.

Huo ulikuwa ushindi wa pili mfululizo kwa Mtibwa baada ya awali kuinyoa Singida Fontain Gate kwa mabao 2-0 katika mechi iliyopita na sasa kuifanya ifikishe pointi 15 baada ya mechi 19 ikiwa na kiporo chake na Simba, japo imeendelea kusalia mkiani ikizibeba timu nyingine 15 za ligi hiyo kwa msimu huu, wakati Prisons imesalia nafasi ya tano ikiwa na pointi 27 baada ya mechi 20.

Mabingwa hao wa zamani wa Bara kwa msimu wa 1999 na 2000 kupitia kocha Zuberi Katwila aliyewapongeza wachezaji kwa kujituma na kupata matokeo ya kushangaza, bado ina kibarua cha kujinasua mkiani kwa mechi 11 ilizobakia nazo kabla ya kufunga msimu huu.

"Kiukweli nawapongeza wachezaji wangu kwa kujituma na kupata matokeo ya kushangaza kwenye huu mchezo, kama mlivyoona tulifanya mabadiliko ya wachezaji kadhaa ambao walienda kubadilisha mchezo na tukapata matokeo tunawashukuru mashabiki wetu kwa kujitoa kutushangilia kwa wakati wote," amesema Katwila, nyota wa zamani wa timu hiyo aliyeongeza;

"Bado tuna jukumu la kuhakikisha timu inabaki ligi kuu na ili tufanikiwe lazima tushinde michezo mingi zaidi hivyo ninawaomba mashabiki wasikate tamaa kutusapoti tutapambana mpaka mwisho maana malengo yetu ni kushinda kila mchezo."

Kwa upande wa kocha wa Prisons, Hamad Ally amewapongeza wapinzani kwa kushinda mchezo huo huku akikiri kuzidiwa katika mchezo huo.

"Hatukucheza katika ubora wetu kwa muda mwingi, kitendo hicho kimewapa nafasi wapinzani wetu kutushambulia muda mwingi licha ya kwamba tulitangulia kupata bao, lakini yote kwa yote tumeyapokea matokeo na tutafanyia kazi dosari zote zilizojitokeza ili kuendelea wimbi la ushindi tuliolokuwa nalo tangu ligi iliporejea," amesema Hamad.

Chanzo: Mwanaspoti