Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtibwa yatuliza mashabiki wake

Ce84eb39bc0b52d946c8ee54b7430b21 Mtibwa yatuliza mashabiki wake

Mon, 12 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KOCHA wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo na kuwaambia muda bado upo wa kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu Bara.

Mtibwa Sugar, moja ya timu za muda mrefu kwenye ligi hiyo, imekuwa na msimu mbaya baada ya kushinda mechi moja kati ya tano huku ikitoka sare mbili na kupoteza mbili.

Akizungumza na gazeti hili, Katwila aliyewahi kuichezea timu hiyo kwa mafanikio alisema kinachotokea ni hali ya kimchezo lakini si kwamba kikosi chake kibaya.

“Nina timu nzuri na nimefanya usajili mzuri, kinachotokea ni hali ya kimchezo tu, lakini mashabiki wetu wasiwe na hofu, tutakaa sawa tu na kutoa ushindani unaotakiwa,” alisema.

Mabingwa hao wa msimu wa mwaka 1999/2000 wako nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 5.

“Kwa hali ilivyo, najua tunawakatisha tamaa mashabiki wetu, lakini wasijali hiyo ndio soka, tutakwenda sawa tu na kutoa ushindani.”

Mtibwa iliyokuwa kwenye ushindani wa Simba na Yanga mwanzoni mwa miaka ya 2000, imekuwa haina mwenendo mzuri kwa zaidi ya misimu mitano sasa na msimu uliopita iliponea chupuchupu kucheza play off.

“Kuna makosa kidogo ambayo ni kawaida kutokea kwenye mpira, kwa wakati huu wa mapumziko mafupi na benchi langu la ufundi tunayafanyia kazi,” alisema Katwila.

Mechi mbili ilizopoteza ni dhidi ya Yanga na Biashara United ambazo zote ilifungwa bao 1-0.

Hata hivyo, bado jinamizi la matokeo mabaya linaendelea kuiandama Mtibwa kwani hata juzi ilipocheza mechi ya kujipima nguvu na timu ya daraja la kwanza ya Geita Gold bado ikafungwa kwa bao 1-0.

Chanzo: habarileo.co.tz