Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtibwa ni rahisi kushuka kuliko kubaki Ligi Kuu

Mtibwa Sss Mtibwa ni rahisi kushuka kuliko kubaki Ligi Kuu

Fri, 1 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Imepita miaka 25 tangu Mtibwa Sugar ilipoishtua Tanzania kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambao kwa muda mrefu taji hilo limekuwa likienda kwa vigogo Yanga na Simba.

Mtibwa ilitwaa ubingwa huo kwa mara ya kwanza msimu wa 1999 ikiwa ni miaka mitatu tu baada ya kupanda Ligi Kuu ikifanya hivyo mwaka 1996 na kuifanya iingie katika historia ya kuwa miongoni mwa timu chache zilizoacha alama kwenye ligi hiyo tofauti na Simba na Yanga.

Kuonyesha haikubahatisha kuondoka na taji hilo, msimu uliofuata yaani 2000, timu hiyo ilibeba tena kwa kulitetea kwa mara ya pili ikiwa ni historia kwa klabu za soka nchini, nje ya Simba na Yanga.

Baadhi ya wachezaji waliokuwemo katika kikosi cha Mtibwa kilichotwaa ubingwa huo kwa misimu hiyo miwili mfululizo ni pamoja na; Mecky Mexime, Hassan Mbarouk, Odo Nombo, Reuben Mgaza, Kassim Mwabuda, Mao Mkami ‘Ball Dancer’, Vincent Peter, Rajabu Msoma, Zubery Katwila, John Mabula, Steven Nemes, Monja Liseki, Godfrey Kikumbizi, Salhina Mjengwa, Ally Yusuph ‘Tigana’, Yusuph Macho ‘Musso’, Mwanamtwa Kihwelo, Dua Said, Kassim Issah, Ramadhan Hamza ‘Kidilu’, Kamba Luffo na Abubakar Mkangwa.

Hata hivyo, ikiwa ni zaidi ya robo karne tangu ilipoanza kucheza Ligi Kuu na kubeba mataji hayo mawili ya Bara, Mtibwa inapitia katika kipindi kigumu kutokana na kumaliza duru la kwanza na kulianza pia duru la pili ikiwa mkiani mwa msimamo wa ligi hiyo kwa kukusanya pointi tisa tu.

Pointi hizo nane imekusanya baada ya kupata ushindi katika mechi mbili, sare tatu na kupoteza mechi 11, ikifunga mabao 16 huku yenyewe ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 32 katika mechi 17 ilizocheza hadi sasa.

Kwa hali ilivyo, Mtibwa inakabiliwa na mtihani mzito katika mechi 13 zilizosalia za duru la pili inazopaswa kuchanga vyema karata ili ibaki Ligi Kuu vinginevyo itazidi kuwapa hofu wengi kuwa, huenda msimu huu ukawa wa mwisho kwao kushiriki ligi hiyo baada ya kuicheza kwa miaka 28 mtawalia.

PENGO LA POINTI Kuna namna mbili ambazo zinaweza kuiokoa Mtibwa isishuke daraja ambazo ni kumaliza ikiwa juu ya nafasi ya 13 ambapo itabaki moja kwa moja ama kumaliza juu ya nafasi ya 15 ili iweze kupambana kubaki kupitia mechi za mchujo (play-off).

Katika hali ya kushangaza, kwa sasa imezidiwa kwa tofauti ya pointi tisa na timu iliyo katika nafasi ya 12 hivyo ili ikae hapo inapaswa kushinda mechi tatu na kuombea timu iliyopo katika nafasi hiyo ipoteze mechi tatu.

Lakini imezidiwa pia kwa pointi nane na Geita Gold ambayo ipo katika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 17.

Kama inazidiwa kwa pengo kubwa la pointi na timu ambazo iko nazo chini, kuna kazi kubwa ambayo Mtibwa inapaswa kufanya ili ibakie Ligi Kuu msimu vinginevyo itakuwa kwaheri ya kuonana.

UDHAIFU NYUMBANI Mechi za nyumbani zimekuwa silaha kubwa ya timu nyingi zinazoshiriki Ligi Kuu Bara katika kutimiza malengo kwa msimu na idadi kubwa ya timu ambazo zimekuwa hazitambi nyumbani, huwa zinakutana na janga la kushuka daraja.

Hata hivyo, imekuwa tofauti kwa Mtibwa inayoonekana kushindwa kuutumia vyema uwanja wake wa nyumbani wa Manungu Complex kupata matokeo mazuri ambayo angalau yangeisaidia iwe katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.

Hadi sasa timu hiyo imecheza mechi tisa katika uwanja huo wa nyumbani na imepata ushindi mara mbili tu, kutoka sare mbili na kupoteza mechi tano, huku ikifunga mabao 11 na kufungwa 13.

Kwa sasa imebakiza mechi sita tu za nyumbani ambazo zitakuwa dhidi ya timu za Tanzania Prisons, KMC, Tabora United, Azam FC, Yanga na Namungo FC.

UGENINI HOI Mtibwa imevuna pointi moja tu ugenini msimu huu kati ya nane ilizocheza hadi sasa huku ikipoteza mechi saba tena mfululizo.

Katika mechi hizo za ugenini imefunga mabao matano tu na yenyewe imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 18.

Mwenendo wake wa mechi zilizopita ambazo ilicheza ugenini unaonyesha ugumu ambao timu hiyo inakabiliana nao katika mechi zilizosalia hasa ukizingatia imebakiza mechi saba dhidi ya timu ambazo zimekuwa hazifungiki kirahisi zinapokuwa kwao, Singida Fountain Gate, Kagera Sugar, Geita Gold, JKT Tanzania, Mashujaa FC, Ihefu na Simba.

MATUMAINI YAPO Kimahesabu ikitokea Mtibwa, ikishinda mechi nne mfululizo itakuwa na pointi 21 zitakazoipa unafuu huenda ikaangukia kucheza mchujo kama ilivyokuwa misimu miwili iliyopita ambapo ilicheza dhidi ya Prisons na kusalia hata hivyo maafande hao na walijinasua.

Mechi nne zilizopo mbele yao ni dhidi ya Singida Fountain Gate, Prisons, Kagera Sugar na Geita Gold, tatu kati ya hizo ni ugenini na moja nyumbani.

Kwa pointi tisa ilizonazo Mtibwa kwenye mechi 17, alikuwa nazo Polisi Tanzania (2022/23) duru la kwanza kwenye mechi 15 ilishinda mbili, sare tatu, ilifungwa mechi 10 na ikamaliza Ligi ikiwa na pointi 25 na ikashuka daraja.

Ukiachana na Ligi Kuu inayoendelea (2023/24), ndani ya misimu mtatui nyuma Mtibwa haikuwa kwenye kiwango cha ushindani na iliponea chupu chupu kushuka daraja.

KUNUSURIKA Hii si mara ya kwanza kwa Mtibwa kupambana kujinusuru kuepuka kushuka daraja, kwani hata misimu minne ya nyuma ilinusurika kushuka dakika za mwisho.

Msimu uliopita wa 2022/23 katika duru la kwanza la ilishika nafasi ya sita, ikiwa na pointi 22, katika mechi 15 ilishinda sita, sare nne, ilifungwa mitano, ilifunga mabao 21, ilitikiswa nyavuni mara 25.

Jumla ya mechi 30 ilishinda mechi tisa, sare nane na ilifungwa 13,ilimaliza msimu nafasi ya 10, ikiwa na jumla ya pointi 35, zilizoifanya ikacheze play-off dhidi ya Mbeya City na kutoboa ikiiachia msala City iliyoenda kukutana na Mashujaa na kushushwa daraja kuzifuata Polisi Tanzania na Ruvu Shooting zilizoteremka moja kwa moja.

Pia katika msimu wa 2021/22, duru la kwanza, Mtibwa ilimaliza nafasi ya 15, ikiwa na pointi pointi 12,kwenye mechi 15 ilishinda ilishinda mbili, sare sita, ilifungwa sita, mabao ya kufunga manane ya kufungwa 15.

Hadi Ligi Kuu inamalizika ilishika nafasi ya 13 katika mechi 30 ilishinda saba, sare 10, ikafungwa 13,mabao ya kufunga 25 ya kufungwa 34, hivyo ilivuna pointi 22 mzunguko wa pili.

TATIZO LIPO HAPA Inaelezwa kinachoiangusha Mtibwa kwa sasa ni mabadiliko ya uongozi wa juu hasa baada ya Jamal Bayser kujiweka kando na kuingizwa watu wengine ambao bado wameshindwa kwenda na kasi aliyokuwa akienda nayo chini ya Mratibu huyo wa zamani aliyeigeuza timu hiyo kuwa tishio hasa kwa vigogo Simba na Yanga.

Inaelezwa kwamba pengo la Bayser na hata mfumo wa uendeshaji wa sasa wa Mtibwa iliyoanzishwa mwaka 1988 umechangia kuifanya timu hiyo kuyumba na kama juhudi za haraka hazitafanyika inaweza kuwa ni msimu wa mwisho kwa timu hiyo kuendelea kukamua katika Ligi Kuu iliyoichezea tangu 1996.

Inadaiwa kutegemea wachezaji chipukizi pekee wanaozalishwa na klabu hiyo kwa miaka mingi kumechangia pia kuifanya timu ikose makali.

Pia kuuzwa kwa baadhi ya mastaa waliokuzwa na timu hiyo kwenda klabu nyingine ni sehemu nyingine ya kuondoka kwa ufalme wa Mtibwa iliyowahi kutwaa Kombe la FA/ASFC mara mbili 2000 na 2017-2018, Kombe la Tusker 2008 na Ngao ya Jamii 2009.

WASIKIE WENYEWE Kocha wa timu hiyo, Zubery Katwila anasema bado wana imani ya kubaki Ligi Kuu ingawa sio kazi rahisi. “Tunapaswa kupambana kwani hatupo mahali pazuri, japo uwezekano wa kusogea juu katika msimamo wa ligi upo ikiwa tutafanya vizuri kwenye mechi tulizobaki,” anasema Katwila, huku nahodha, Oscar Masai anaongeza kuwa, wachezaji hawajakata tamaa.

“Ukiangalia timu hazijapishana sana pointi, hivyo kama tukishinda mechi zijazo ni rahisi kutoka tulipo na kusogea juu,” anasema.

Msemaji wa Mtibwa, Thobias Kifaru anakumbushia safari nzima ya timu hiyo akisema “Mwaka 1983 nilihusika kuandika barua kwenda Chama cha Soka Morogoro, ili timu hii tuliyoianzisha kwa ajili ya wafanyakazi wa kampuni, kushiriki Ligi Daraja la Dne.

“Viongozi wa Mtibwa kipindi hicho lilikuwa jopo la watu 15 likiongoza na baba’ake Happiness Magese, wakaomba timu iwe chini ya kiwanda, wakailea tukapanda mwaka 1996 kipindi hicho iliitwa Ligi Daraja la Kwanza.

“Baadaye kiwanda kikabadilishwa kutoka mali ya Umma kuwa cha mtu binafsi, ndipo 1999 Jamal Byser alikuwa mratibu wa kiwanda, akaihudumia hadi ikachukua ubingwa 1999 na 2000 tangu hapo hatujafanikiwa tena, anasema Kifaru na kuongeza;

“Siwezi kuacha kumkumbuka John Simkoko aliyewafundisha kina Salum Mayanga, Zuber Katwila, Mecky Maxime ambao baada ya kuustafu wakasomeshwa ukocha na sasa wanahudumia timu za Ligi Kuu, ni matunda ya Mtibwa.”

Kifaru anasema kwa sasa anapungua uzito kwa presha ya matokeo, ila ana imani na wachezaji, viongozi na makocha watapambana kuibakiza Ligi Kuu. Jamal Bayser alipotafutwa na Mwanaspoti anasema anaamini ni upepo mbaya umepita na timu itakaa sawa kurejea katika ushindani.

“Mtibwa sio ya kwanza kupata changamoto hiyo, ina makocha wazuri kama Zuberi Katwila, hivyo naamini upepo utapita tu, wapambane.”

Nyota wa zamani, Said Bahanuzi anasema; “Mtibwa imekuza vijana wengi nchini, naumia pindi ninapoiona inaburuza mkia, naamini watambana kuiokoa timu.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: