Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtibwa kusaka rekodi ya miaka minne Yanga

Sumu Ya Mtibwa (18).jpeg Mtibwa kusaka rekodi ya miaka minne Yanga

Sat, 16 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yanga na Mtibwa Sugar zinakutana Dar es Salaam leo katika pambano la Ligi Kuu Bara, huku kila upande ukijinadi umejiandaa kushinda ukiahidi soka tamu litakalowapa burudani mashabiki.

Timu hizo zitakuwa katika  Uwanja wa Azam Complex kusaka pointi tatu katika mchezo wa 10 msimu huu kwa Yanga inayosaka kupungua pengo la pointi nne dhidi ya vinara Azam wenye 28 waliocheza mechi 12, tatu zaidi ya ilizocheza Yanga yenye alama 24.

Timu hizo zinakutana zikiwa kwenye hali mbili tofauti, Yanga ikionekana kuimarika zaidi, huku Mtibwa ikiwa hoi kwani inaburuza mkia kwenye msimamo ikikusanya pointi tano katika michezo 12 ikishinda mmoja.

Licha ya Mtibwa kuwa kwenye hali mbaya kocha wa timu hiyo, Zubery Katwila ametamba watashuka kwenye mchezo huo utakaopigwa kuanzia saa 12:30 jioni wakijua wana presha, lakini hata wapinzani wao wanayo kubwa na kiu yao ni kupata alama tatu ugenini.

Mchezo wa leo ni wa sita kwa  Yanga ikiwa nyumbani msimu huu na hakuna timu iliyofanikiwa kuambulia japo pointi moja, kwani imeshinda zote na kuvuna mabao 16 ikiruhusu mawili, kitu kitakachoipa wakati mgumu Mtibwa kwenye mechi hiyo.

Rekodi zinaonyesha katika mechi tano baina ya timu hizo kwenye ligi, Mtibwa haijawahi kushinda wala kupata sare zaidi ya kufungwa na Yanga, na ushindi wa mwisho kwa timu hiyo mbele ya wababe hao ni ule wa Aprili 17, 2019 ilipoitungua mjini Morogoro kwa bao 1-0 lililofungwa na Riffat Khamis katika dakika ya 52.

Katika mchezo wa leo mabeki wa Mtibwa watakuwa na kazi ya kuwazuia nyota wa Yanga wakiongozwa na vinara wa mabao wa ligi, Maxi Nzengeli na Stephane Aziz Ki sambamba na kiungo mshambuliaji, Pacome Zouzioua ambao mara ya mwisho waliifanyia kitu mbaya Simba kwa kuifunga mabao 5-1 katika mechi ya Kariakoo Derby.

Pia washambuliaji wa Mtibwa wakiongozwa na Matteo Antony, Vitalis Mayanga, Ladack Chasambi, Juma Liuzio na wengine wanapaswa wajipange kupenya mbele ya ukuta wa Yanga ulio chini ya nahodha Bakar Mwamnyeto, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Yao Kouassi na kipa Diarra Djigui ulioruhusu mabao matano katika ligi.

Licha ya rekodi kuibeba zaidi Yanga, Kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi alisema watashuka uwanjani wakiiheshimu Mtibwa ili kuhakikisha wanakusanya pointi wajiweke pazuri, na kuna uwezekano mkubwa akafanya mabadiliko kwenye kikosi kwa ajili ya kutunza nguvu za mechi ijayo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga inatarajiwa kuikaribisha Medeama ya Ghana katika mechi ya marudiano ya Kundi D ya Ligi ya Mabingwa baada ya kutoka nayo sare ya 1-1 ugenini mjini Kumasi wikiendi iliyopita.

Katika mechi tisa za Yanga katika Ligi Kuu imepoteza moja ugenini mbele ya Ihefu iliyoifunga mabao 2-1, Oktoba 4, timu hiyo ikinolewa na Katwila ambaye kwa sasa yupo Mtibwa Sugar.

Hadi mazoezi ya juzi, Gamondi alikuwa akijaribu silaha zote, huku habari njema kwa Yanga ikiwa ni kuanza mazoezi kwa beki Joyce Lomalisa aliyeumia kwenye mchezo wa CAF dhidi ya Al Ahly ya Misri.

Gamondi alisema hataki kuwadharau Mtibwa ambapo mazoezi ya wiki hii amekuwa bize kuwapa mbinu za ubora vijana wake akifichua pia wamepata muda mzuri wa kupumzika baada ya kutoka safari ndefu na mechi ngumu dhidi ya Medeama.

“Tunaingia kucheza na Mtibwa Sugar tukiwa na shauku na morali ya kupambana kupata pointi tatu lakini wakati huohuo akili zetu zikiwa katika mechi ngumu itakayochezwa siku ya Jumatano,” alisema.

Kocha wa Mtibwa, Zuberi Katwila alisema: “Mechi haizoeleki hata Yanga lazima iwe na presha ya kucheza hata kama na timu ndogo, hivyo tunakwenda kutafuta alama tatu za ushindi.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live