Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtibwa dozi kutwa mara mbili

Mtibwa Sss Mtibwa dozi kutwa mara mbili

Mon, 25 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati Ligi Kuu ikiwa bado imesimama kupisha kalenda ya FIFA, timu ya Mtibwa Sugar ya mkoani hapa imeendelea na maandalizi makali ambapo kwa sasa timu hiyo inafanya mazoezi asubuhi na jioni kwa lengo la kutengeneza utimamu wa mwili kwa wachezaji kabla ya ligi kurejea.

Mtibwa Sugar kwa sasa haiko katika nafasi nzuri kwenye msimamo baada ya kucheza michezo 20 na kuambilia pointi 16 ambapo wanapaswa kupigana ili timu yao isishuke daraja.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila alisema timu hiyo kwa sasa inafanya mazoezi mara mbili kwa siku lengo likiwa ni kujenga utimamu wa mwili kwa wachezaji baada ya kupewa mapumziko.

"Kama mnavyojua wiki kadhaa nyuma tulitoa mapumziko kwa wachezaji wetu baada ya ligi kuwa imesimama na sasa wamerudi, kinachoendelea ni kufanya mazoezi asubuhi na jioni ili tuweze kuwa na wachezaji waliotimamu kimwili kabla ya ligi kuanza," alisema na kuongeza:

"Mazoezi haya ya mara mbili kwa siku yanatusaidia kugawanya programu za kiufundi maana kama asubuhi tutafanya mazoezi ya fiziki, jioni lazima tuingize ufundi kwao kulingana na mazoezi tuliyokuwa nayo asubuhi na lengo ni kuona tunashinda kila mchezo ligi itakaporejea ili timu ibaki Ligi Kuu."

Kwa upande wake, kiungo wa timu hiyo, Juma Nyangi anayemudu kucheza kiungo wa ukabaji na na ushambuliaji, alisema wao kama wachezaji wameshajiapiza kupambana kwenye michezo iliyobaki ili timu yao ibaki Ligi Kuu msimu ujao.

"Kwa sasa tunafanya mazoezi mara mbili kwa siku hili linatuongezea kujiamini na kupata ufundi zaidi kutoka kwa makocha wetu na kwa sasa tumejiapiza kwamba ligi ikianza tujitoe ili tushinde michezo iliyobaki maana hatutaki kuwa sehemu ya historia kwa timu hii kushuka mikononi mwetu.

"Tunawaomba mashabiki wetu waendelee kutuunga mkono kwakuwa tunajiandaa kuipigania timu kwa mechi zilizobaki na tunaamini tutaibakiza timu yetu kwenye ligi."

Chanzo: Mwanaspoti