Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtibwa Sugar yazindukia jijini Mwanza, waichapa Singida

Mtibwa Mwanza.jpeg Mtibwa Sugar yazindukia jijini Mwanza, waichapa Singida

Sun, 3 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya kucheza mechi zaidi ya saba bila kupata ushindi, hatimaye jana jioni Mtibwa Sugar imezindukia ikiwa jijini Mwanza kwa kuinyoosha Singida Fountain Gate kwa mabao 2-0 katika pambano la Ligi Kuu lililochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Ushindi huo wa kwanza kwa Mtibwa tangu iliposhinda mara ya mwisho Desemba 19 mwaka jana dhidi ya Mashujaa iliyokufa mabao 2-1, umeifanya mabingwa hao wa zamani wa Tanzania kwa msimu wa mwaka 1999 na 2000 kufikisha pointi 12 na kuzipa presha timu zilizopo juu yake kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Ushindi huo ni wa kwanza ugenini msimu huu, kwani kabla ya leo, timu hiyo ilikuwa imevuna pointi moja tu ugenini kati ya mechi nane ilizocheza huku ikifungwa saba mfululizo. Katika mechi hizo za ugenini ilikuwa imefunga mabao matano na kuruhusu 18.

Katika mchezo wa leo, shujaa wa Mtibwa amekuwa ni mshambuliaji Omary Marungu aliyefunga bao moja na kusababisha lingine baada ya kuingia kipindi cha pili dakika ya 65 akichukua nafasi ya Seif Karihe na kuwa tishio katika safu ya ulinzi ya Singida.

Marungu amehusika katika bao la kwanza ambalo limefungwa na Abdul Hilaly dakika ya 69 kwa mkwaju wa penalti, baada ya mshambuliaji huyo kuangushwa eneo la hatari na kipa wa Singida, Beno Kakolanya wakati akiwa kwenye jaribio la kufunga bao.

Katika dakika ya 76 mshambuliaji huyo aliendelea kuitesa Singida kwa kufunga bao la pili la Mtibwa baada ya kumpiga chenga kipa Kakolanya na kupasia mpira kambani akiipa timu yake ushindi wa tatu msimu huu.

Licha ya ushindi huo, Mtibwa Sugar inaendelea kushika mkia kwenye nafasi ya 16 ikiwa na pointi 12 baada ya kushinda mechi tatu, sare tatu na kupoteza 12, huku Singida Fountain Gate ikikamata nafasi ya nane na pointi zao 21.

Kipa wa Singida, Kakolanya ameruhusu mfululizo mabao katika mechi nne tangu atoke nchini Ivory Coast kwenye Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) akifungwa 3-1 na Tanzania Prisons, 1-1 na Tabora United, 1-0 na Azam FC na 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila, amesema ushindi wa leo unawapa kujiamini na morali kuelekea michezo ijayo, huku akiwasifu wachezaji wake kwa kutotoka kwenye mstari na kuendelea kupokea maelekezo yake ya kiufundi licha ya kupitia kipindi kigumu cha kutopata matokeo ya ushindi.

Huo ni ushindi wa tatu kwa Katwila tangu ajiunge na Mtibwa Oktoba 23, mwaka jana akiwa ameiongoza katika michezo 12, amepoteza minne na kutoka sare moja.

Chanzo: Mwanaspoti