Idara ya Habari na Mawasilino ya Mtibwa Sugar imewatoa hofu Mashabiki wa klabu hiyo, baada ya kikosi chao kufanikisha azma ya kusalia Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu ujao (2022/23).
Mtibwa Sugar imebaki Ligi Kuu kwa kupata ushindi wa jumla wa 3-2, baada ya kucheza michezo miwili ya hatua ya mtoano (Play Off), katika viwanja wa Sokoine (Mbeya) na Manungu Complex (Morogoro).
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Mtibwa Sugar Thobias Kifaru amesema, baada ya kukamilisha mpango wa kubaki Ligi Kuu, Uongozi utakutana na Benchi la Ufundi, ili kupanga mikakati mizuri ya kuboresha kikosi.
Amesema kikao cha pande hizo mbili kitajikita katika ripoti ya Benchi la Ufundi linaloongozwa na Kocha mzawa Salum Shaban Mayanga, ili kuangalia namna ya kuyafanyia kazi mapungufu yaliyoorodheshwa kwenye ripoti hiyo.
“Tumefanikiwa kubaki Ligi Kuu kwa msimu ujao, tutakaa chini tuone namna ya kuondoa changamoto zilizotukumba na kutufikisha katika mchezo wa ‘Play Off’, Viongozi na Benchi la Ufundi watakutana haraka iwezkanavyo ili kuifanyia kazi ripoti ya kiufundi.”
“Tunaamini kikosi chetu kuanzia msimu ujao kitarudisha hadi ya Mtibwa Sugar, baada ya kupata wakati mgumu kwa misimu miwili mfululizo, hapa tunasema ni mwisho kucheza ‘Play Off’.” Amesema Kifaru
Mtibwa Sugar ilimaliza katika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2021/22, ikifuatiwa na Tanzania Prisons iliyoshika nafasi ya 14, hivyo kanuni zilizoelekeza timu hizo kucheza mchezo wa ‘Play Off’ wa Ligi Kuu ili kupata timu moja itakayobaki na nyingine itakayocheza dhidi ya mshindi wa ‘Play Off’ ya Ligi Daraja la Kwanza ambaye ni JKT Tanzania.